Tuesday, 29 September 2015

MTENGA APINGA VIKALI KUSHAMBULIWA KWA WANACCM KWA MAWE NA WAFUASI WA CHADEMA

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga akiongea na waandishi wa habari jioni hii. (Picha na Friday Simbaya)


Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alaani kitendo cha wafuasi wa Chadema kushambulia wafuasi wake wakati wakitoka kwenye mkutano wa mgombea urais kupitia chama Dkt  John Pombe magufuli jana.

Katibu huyo alitoa kauli wakati akizungumza na wanahabari ofisini kwake baadaye na kuwasihi wafuasi wa Chadema kufanya kampeni za kistaarabu.

Alisema CCM imekuwa ikikumbana na misukosuko ya kutukanwa, kurushiwa mawe na baadhi ya wafuasi wake kupigwa mawe mara kwa mara wanapotokea katika mkiutano yao.

Alisema uvumilivu wa wanaCCM dhidi ya vurugu wanazofanyiwa unaweza kwisha na kusababisha hatari ambayo hawataki itokee.

Mgombea ubunge jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa pamoja na wafuasi wengine 62 wa chama hicho wamelala selo ya kituo cha Polisi cha mjini Iringa wakituhumiwa kuwafanyia vurugu wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na askari wa kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).

Mchungaji huyo na wafuasi hao wanatuhumiwa kuwafanyia vurugu wanaCCM waliokuwa wakitokea katika mkutano wa mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli, jana mjini Iringa, kabla ya kuwarushia mawe askari wa FFU waliofika katika eneo la tukio kutuliza ghasi hiyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 12.30 na saa 1.00 jioni katika eneo kichangani zilipo ofisi za muda za kampeni za mgombea huyo.

Alisema baada ya kuwashikilia kwa takribani saa 15, jeshi la Polisi liliwaachia kwa dhamana majira ya saa saba mchana, huku 14 kati yao akiwemo Mchungaji Msigwa wakitarajia kufikishwa mahakamani pindi uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika.

Mungi alisema vijana hao na mgombea wao walikuwa na mkutano wa ndani katika ofisi hizo zilizopo katika Hoteli ya Sambala wakati mkutano wa Dk Magufuli ukiendelea katika uwanja wa Samora, mjini hapa.

“Majira ya saa 12.30 vijana hao walitoka katika mkutano wao huo huku wakiwa na hamasa, wakaingia barabarani na kuzuia magari yakiwemo yaliyokuwa yamebeba wafuasi wa CCM yasipite,” alisema.

Alisema baada ya kutaarifiwa, FFU walifika katika eneo la tukio kwa lengo la kuwatawanya wafuasi wa chama hicho kwa amani, lakini walikaidi na kuanza kuwarushia mawe askari akiwemo mkuu wa FFU wa Iringa.

“Baada ya kuanza kurusha mawe askari waliwavamia na kufanikiwa kuwakamata vijana 62 huku Mchungaji Msigwa akifanikiwa kutokomea kusikoeleweka kabla hajajisalimisha mwenyewe majira ya saa tatu usiku,” alisema.

Alisema Polisi ililazimika kuwakamata wafuasi wa chama hicho na mgombea wao kwa sababu amani ni kipaumbele cha kwanza kwa jeshi hilo na hawatakubali ivunjike kwa kisingizio cha shughuli za kisiasa.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Iringa Mjini, Frank Nyalusi alisema; “jeshi la Polisi linatumiwa na chama tawala katika kipindi hiki cha kampeni ili kukinufaisha chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao.”

Nyalusi aliwatetea waliokamatwa kwamba hawakufanya vurugu kama inavyoelezwa na jeshi hilo, bali walivamiwa na askari hao wakiwa ndani ya ofisi zao za kampeni wakiendelea na kikao chao.

Alisema ili kuweka rekodi zao vizuri watawatumia wanasheria wao kulishtaki jeshi la Polisi kwa kuwavamia, kuwajeruhi baadhi yao na kuharibu mali za hoteli hiyo.

Nyalusi alisema wafuasi wawili wa chama chao walivunjwa mikono katika tukio hilo, huku wengine sita wakijeruhiwa vibaya, taarifa ambazo RPC Mungi amezikanusha vikali.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...