Tuesday, 15 September 2015

WANAWAKE WA MKOA WA IRINGA WAPATIWA MAFUNZO JUU YA SHERIA YA UMILIKI WA ARDHI NA UONGOZI


Darasa likiendelea

Wanawake wa wilaya za Iringa, Mufindi na Kilolo mkoani Iringa wapatiwa mafunzo juu ya ushawishi na utetezi wa haki za wanawake na sheria ya umiliki wa ardhi ya mwaka 1999.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Shirika la Land O'Lakes chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID). 

Mratibu Msaidizi wa Programu wa Shirika la Land O’Lakes Tanzania, Mary Kafanabo alisema kuwa mafunzo hayo yametolewa kufuatia uelewa mdogo wa sheria za umiliki wa ardhi na sheria ya ardhi kwa ujumla.

Alisema kuwa wanawake wengi nchini wana uelewa mdogo wa sheria za umiliki wa ardhi na sheria ya ardhi, ndio maana shirika hilo likaona umuhimu wakuwapatia mafunzo wanawake ambao ni wazalishaji wakubwa katika kilimo na masuala mengine ya kijamii.

Katika warsha hiyo wawezeshaji kutoka chama cha wanasheria wanawake (TAWLA) ambao ni Latifa Ayubu na Francisca Gasper walitoa mada kuhusu haki za wanawake katika kumiliki ardhi Tanzania.

Walisema kuwa serikali kupitia wizara ya maendeleo ya jamii na watoto ilitunga sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia ya mwaka 1992.

Walisema kuwa serikali katika jitihada za kuwapa wananchi mwelekeo wa maendeleo ya wanawake na jinsia ili kuhakikisha kuwa sera, mipango na shughuli mbalimbali za maendeleo zinazingatia usawa wa jinsia.

Awali, Afisa Kilimo Msaidizi wa Wilaya ya Mufindi, Tinara Nyato wakati akifungua warsha hiyo kuhusu haki za wanawake katika kumiliki ardhi, aliwasihi wanawake kutumia elimu waliopata vizuri pamoja na kupeleka elimu walioipata kwa wanawake wenzao vijijini walikutoka.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Jesca Chibwana kutoka Kijiji cha Igomaa, Kata ya Sadani waliyani Mufindi alisema kuwa baada ya kupata uelewa juu ya sheria ya umiliki wa ardhi atakuwa balozi mzuri wakuwaelimisha wanawake wenzake kijijini. 

Naye Mratibu wa Programu wa Shirika la Land O’Lakes Tanzania, Mary Kabelele alisema kuwa wanawake wengi wana uelewa mdogo kuhusu suala la umiliki wa ardhi ambapo wanadhani mwenye jukumu hilo ni mwanaume pekee.

Alisema kuwa wanawake walikuwa na dhana potofu kwamba kwa kuwa mwanaume ndio msimamizi wa familia, basi umiliki wa ardhi ni haki yake.

“Tunajivunia kwa sasa kuona walengwa wa mradi huu ambao ni wanawake na jamii kwa ujumla wameanza kupata muamko kupitia mafunzo haya na wataanza kudai haki zao, aliongeza Kabelele.

Wakati huohuo, Shirika la Land O'Lakes limewapatia wanawake 25 mafunzo kuhusu uongozi kwa wanawake na wasichana yaliyofanyika Ifunda wilayani Iringa, Mkoa wa Iringa.

Mafunzo hayo yalilenga kubainisha na kutambua mchango wa wananwake katika sekta mbalimbali, ili kuondoa fikra hasi juu na uwezo na mchango wa wananwake katika maendeleo.

Mratibu wa Programu wa Shirika la Land O’Lakes Tanzania, Mary Kabelele alisema kuwa kipimo cha uongozi ni kuona kiongozi anavyoweza kuhamasisha na kuleta ushawishi kwa watu na kufikia maendeleo yaliyotarajiwa.

“Wanawake wana nafasi na jukumu kubwa katika kuongoza mabadiliko kwa vile wanatumia muda mwingi na kuchangia kiasi kikubwa cha nguvu kazi katika kilimo na masuala mengine ya kijamii,” alisema.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...