Kaimu wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Selemani Mzee (katikati) ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo akifungua mdahalo wa wazi juu ya amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu unaofanyika katika ukumbi wa chuo Kikuu Huria (OUT)mjini Iringa. Kutoka kushoto walioketi na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilolo Martin Mlwafu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa ACP Ramadhani Mungi, Mwenyekiti wa ICISO Alexander Kisinini na Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Iringa, Wilfred Myuyu. Mdahalo huo uliandaliwa na Iringa civil society organization (ICISO-Umbrella) kwa kushirikiana na Asasi ya Foundation for Civil Society (FCS) jana. (Picha na Friday Simbaya)
Na Friday Simbaya, Iringa
WAKATI zimebaki siku chache kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Oktoba mwaka huu, Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Iringa, Wilfred Myuyu amesema ameanza kupokea vifaa vya uchaguzi.
Mratibu huyo alisema hayo wakati wa mdahalo wa wazi juu ya amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria (OUT) mjini Iringa jana.
Mdahalo huo uliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Iringa Civil Society Organization (ICISO-Umbrella) kwa kushirikiana na asasi ya ‘The Foundation for Civil Society (FCS).’
Myuyu ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi (Sehemu ya Serikali za Mitaa) alisema kuwa baadhi ya vifaa vilivyopokelewa ni pamoja na maboksi 5,995 ya kupigiakura, taa mbalimbali na daftari la kudumu la wapigakura.
Alisema kuwa uchaguzi ni mchakato na tayari Mkoa wa Iringa umeanza maandalizi na utakuwa na jumla ya vituo vya kupigiakura 1,641 na kuongeza kuwa kila kituo kitakuwa na wapigakura wasiozidi 500.
Wilfred Myuyu alisema kuwa mkoa umeandikisha jumla ya wapigakura 526,006 kwa kuvuka lengo la matarajio la 521,491 na kufikia asilimia 100.8.
“Vituo vile vilivyotumika kujiandikisha wapigakura ndivyo vitakavyokuwa vituo vya kupigiakura na kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na wapigakura wasiopungua 500 na kama kituo kile kilikuwa na wapigakura 1,000, basi kituo hicho kitagawanywa na kuwa vituo viwili vya kupigiakura ambapo vitakuwa ‘A’ na ‘B’, ” alisema Myuyu.
Alisema kuwa vituo vyote vya kupigiakura vitafunguliwa kuanzia saa 1 asubuhi na kufungwa saa 10 jioni ambapo vitageuzwa kuwa vituo vya kuhesabia kura.
Aidha, alisema kuwa orodha ya majina ya wapigakura itabandikwa siku nane kabla ya uchaguzi mkuu, ili kuwapa fursa watu kuangalia majina yao katika vituo walivyojiandikishia.
Alisema kuwa kanuni za uchaguzi mkuu za mwaka 2015 zinavitaka vyama vya siasa kuwaelimisha wanachama wake namna ya kupigakura na baada ya kupigakura hawaruhusiwi kusubiri matokeo ili kuepusha msongamano.
Mkoa wa Iringa ulianza uandikishaji ya wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura Aprili 29 na kukamilika Mei, 29 mwaka huu.
“Kwa mujibu wa sheria, matokeo ya udiwani yanatangazwa na msimamizi msadizi wa kata, ya ubunge msimamizi wa wilaya na urais ni tume,” alisema.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Damian Lubuva aliagiza waratibu na wasimamizi wa uchaguzi pamoja na makamanda wa polisi kutenda haki wakati wa Uchaguzi Mkuu kwa kuwa usalama wa Taifa upo mikononi mwao na kuonya kuwa kosa lolote linaweza kuiingiza nchi matatizoni.
NEC ilisema hayo katika kikao kilichohudhuriwa na wasimamizi wa uchaguzi wa halmashauri zote nchini pamoja na makamanda wa mikoa wa Jeshi la Polisi, ambalo liliongozwa na mkuu wake, IGP Ernest Mangu, pamoja na makamishna wake- Diwani Athumani (Upelelezi wa Makosa ya Jinai), Paul Chagonja (Operesheni), Mussa Ali Mussa (Polisi Jamii) na Suleiman Kova (Kanda Maalumu Dar es Salaam) pamoja na baadhi ya wakuu wa vikosi.
No comments:
Post a Comment