Afisa Tarafa ya Pawaga, Nasson Mwaulesi (Picha na Friday Simbaya)
OFISA Ardhi na Maliasli wa Wilaya ya Iringa, Donald Mshauri amepongeza Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) kwa kuanzisha Jukwaa la wakulima na wafugaji wa tarafa la Pawaga linaloshughulikia migogoro baina ya makundi hayo.
Mshauri alisema hayo jana wakati wa mkutano wa wadau wa masuala ya ardhi katika Wilaya ya Iringa, mkoani Iringa uliyoandaliwa na Jumuiko la Maliasili Tanzania.
Alisema kuwa kuanzishwa kwa jukwaa hilo kumepunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika Tarafa ya Pawaga tatizo ambalo limekuwepo muda sasa.
Alisema kuwa zipo sababu zilizopelekea migogoro ya ardhi katika wilaya yake, zikiwemo ongezeko la mifugo na ongezeko la wahamiaji kutoka wilaya zingine kuja Pawaga.
“Wafugaji wamekuwa wakiishi nyanda kame zisizo na maji na malisho ya kutosha wakati wakulima wakiishi mabondeni ambako kuna maji na shughuli za kilimo kufanyika…,” alielezea ofisa ardhi na maliasili huyo.
Mshauri alisema kuwa mambo hayo huchochewa na kukosekana kwa taratibu na mazingira rafiki yanayowezesha wafugaji kunufaika na rasilimamali zinazopatikana mabodeni.
Naye, Mratibu wa Mradi wa Ardhi Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF), Godfrey Massey alisema kuwa TNRF imeunda Jukwaa la wakulima na wafugaji wa tarafa ya Pawaga kwa lengo la kuwaleta pamoja ili wajadili chanagmoto zinazowakumba na kutafuta namna yakukabilianazo kwa pamoja.
Alisema kuwa mradi huo umetoa mafunzo ya haki za ardhi na utwala vijijini kwa wanavijiji na viongozi wa vijiji vinne katika tarafa ya Pawaga ambapo wanavijiji 200 na viongozi 200 wamepatiwa mafunzo.
Massey alisema kuwa vijiji hivyo ni Itunudu, Mbolimboli, Kisanga na Isele pamoja na kutoa mafunzo kwa waangalizi nane, wawili kila kijiji kwa kuzingatia jinsia walipatiwa mafunzo zaidi ili waendelea kuwa walimu na washauri wa masuala ya ardhi katika vijiji vyao.
Hata hivyo, hivi karibuni TNRF ilifanya mafunzo ya hadhara juu ya haki za ardhi na utawala vijijini na kutoa msaada wa sheria kwa wanajiji katika vijiji vitatu katika tarafa ya Pawaga.
Vijiji hivyo ni Mkumbwanyi, Magombwe na Mkombilenga ambapo jumla ya wanavijiji 334 kati yao wanaume 215 na wanawake 119 walinufaika na mafunzo hayo.
Wakati huohuo, Afisa Tarafa ya Pawaga, Nasson Mwaulesi aiitisha kikao na watumishi wote wa serikali wanaofanya kazi ndani ya tarafa hiyo kwa kuwakumbusha kuhusu uwajibikaji kazini kila mmoja kwa nafasi yake.
Afisa tarafa huyo pamoja na mambo mengine aliwatabulisha watumishi wapya ili wafahamiane na kuwaasa watumishi kuwa na maadili mema katika kuishi na jamii.
Mwaulesi alisema kuwa watumishi wanatakiwa kuwa na kikao na afisa tarafa kila baada ya miezi mitatu na kuwaonya watumishi hao kutojihusisha na masuala ya siasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Alisema kuwa watumishi hao wanatakiwa kuzingatia maadili mema katika kuishi na jamii, kujipenda pamoja na unadhifu.
Kikao hicho kulihudhuriwa na watendaji wa kata, walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, waratibu elimu kata, maofisa ugani, maofisa maendeleo ya jamii na ofisa umwagiliaji wa tarafa.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na polisi tarafa ya Pawaga, mkuu wa gereza la Pawaga, mkuu wa kituo cha afya Kimende-Pawaga na hakimu wa mahakama ya mwanzo Pawaga.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment