Monday, 12 October 2015

SALIM ASAS ALIA NA UTITIRI WA KODI


Mkurugenzi wa makampuni ya Asas, Salim Abri akisoma risala fupi kwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na  Uvuvi Dkt Titus Kamani hivi karibuni. (Picha na Friday Simbaya)


IRINGA: Mkurugenzi wa makampuni ya Asas, Salim Abri ameiomba serikali kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mazao ya maziwa ambayo ni siagi, jibini, samli, cream na maziwa yenye ladha za matunda.

Salim alitoa kilio hicho mbele ya Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Titus Kamani alipotembea kiwanda cha kusindika maziwa cha ASAS DAIRIES LTD mjini Iringa, mkoani Iringa kupitia mradi wa Uendelezaji Sekta ya Maziwa Afrika Mashariki (EADD II).

Alisema kuwa kuondoa kodi hizo hakutaathiri sana pato la serikali kwa sababu sekta ya usindikaji wa maziwa nchini bado ni changa.

Alisema kuwa viwango vya kodi ni vikubwa na vingi kulinganisha na uwezo wa uzalishaji wa viwanda vya kusindika maziwa.

“Kwa ujumla mfumo mzima wa kodi unakwamisha mafanikio ya viwanda vya maziwa nchini,” alisema Salim.

Alisema bidhaa za maziwa toka nje ya nchi, zinauzwa kwa bei ndogo ukilinganisha na bidhaa za maziwa zinazosindikwa nchini.

Hii inatokana na ukweli kwamba wigo wa kodi hapa nchini ni mkubwa mno ukilinganisha na nchi nyingine,” aliongeza mkurugenzi.

Alisema kuwa kiwanda hakijafikia kiwango cha uzalishaji na kwa sasa kinazalisha lita 12,000 kwa siku na sababu kubwa wananchi wengi kutokuwa na tabia ya kunywa maziwa pamoja na kuwa viwango vikubwa vya kodi kama vile VAT.

Mradi wa Uendelezaji Sekta ya Maziwa Afrika Mashariki (East Africa Dairy Development) in mradi wa miaka mitano (2013-2018) unaotekelezwa kwa awamu ya pili katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania kwa kutumia mfumo wa kitovu cha maziwa (Dairy Hub). 

Nchini Tanzania mradi huu unatekelezwa katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe.

Mwisho









No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...