Mgombea Ubunge kupitia tiketi ya Chadema katika Jimbo la Iringa Mjini Mch. Peter Msigwa (juu ya gari) akiwatumiza mzuka wafuasi wake ili tume ya taifa ya uchaguzi (NEC) iendelee na mchakato wa kutangaza matokeo ambayo hata hivyo bado hajatangazwa.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Iringa Mjini kimeyapinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Ubunge na Rais jimbo la Iringa Mjini yanayoelekea kukipa ushindi mkubwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Matokeo hayo yameshindwa kutangazwa leo kama ilivyotarajiwa na wafuasi wengi wa chama hicho na wakazi wengine wa jimbo hilo baada ya kutokea wizi wa maboski mawili yaa kura katika kituo cha kupigia kura cha Ipogolo ‘C’, majira ya saa nne usiku, Oktoba 25.
Wakisubiri matokeo hayo leo, mamia ya wafuasi wa Chadema walikuwa wamejazana nje ya ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo Ahmed Sawa toka saa 12.00 asubuhi hadi 11.00 jioni walipotangaziwa kwamba matokeo hayo hayatatangazwa mpaka kesho wapiga kura wa kituo hicho watakaporudia uchaguzi huo.
Akitangaza uamuzi huo katika tukio lililokuwa na ulinzi mkali wa jeshi la Polisi pamoja na magari yake ya washawasha, Sawa alisema uchaguzi katika kituo hicho unarudiwa baada ya kutokea wizi huo na kwamba matokeo ya jumla yatatanngazwa baada ya marudio hayo kukamilika.
Awali Katibu wa CCM Iringa Mjini, Elisha Mwampashi alifanya mkutano na wanahabari na kuwaleza kwamba hawayatambui matokeo ya uchaguzi huo kwasababu ulikuwa na dosari ikiwemo ya wizi wa maboksi hayo ya kura.
Dosari nyingine kwa mujibu wa Mwampashi ni ushabiki wa wazi kwa wagombea wa Chadema uliooneshwa na baadhi ya wasimamizi wasaidizi katika vituo mbalimbali vya kupigia kura.
Akizungumzia wizi wa maboksi ya kura katika kituo hicho, Mwampashi alisema majira ya saa nne usiku, baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika, kituo hicho kilivamiwa na vijana waliokuwa wamevaa nguo zenye nembo ya Chadema, wakawatisha wasimamizi na mawakala wa kituo hicho na kutokomea na maboksi hayo.
“Kwa hiyo tumemuandikia barua msimamizi tukitaka uchaguzi huo jimbo zima urudiwe ili haki iweze kutendeka. Na wakati wa marudio hayo tunamtaka msimamizi kubadilisha wasimamizi wasaidizi wote kwa sababu waliotumiwa katika uchaguzi huo walionesha dalili ya kutokuwa waaminifu baada ya kuonekana wakishabikia wagombea wa Ukawa,” alisema.
Akizungumzia madai ya CCM, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Iringa Mjini, Frank Nyalusi alisema; “madai ya CCM tumeyasikia baada ya kuwasilishwa katika kikao cha pamoja na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo.”
Akikubaliana na uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi wa kurudia uchaguzi katika kituo hicho, Nyalusi alisema madai ya uchaguzi mzima wa jimbo kurudiwa hayakubaliki kwa sababu hayaendani na sheria za uchaguzi na yanakiuka misingi ya demokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa.
“Kwanza nikanushe kwamba walioiba maboksi hayo ya kura ni wafuasi wa Chadema kama inavyodaiwa na CCM kwani kuvaa vazi lenye nembo ya Chadema hakuhalalishi kwamba kila anayevaa vazi hilo ni mfuasi au mwanachama wetu maana katika siasa wapinzani wetu wanaweza kuwatumia watu wao waliowavalisha mavazi yenye nembo yetu ili kufanya jambo litakalohalalisha jambo wanalotaka kulifanya,” alisema.
Nyalusi alisema wakati uchaguzi huo ukitarajiwa kurudiwa katika kituo hicho taarifa walizokusanya toka kwa mawakala wao zinaonesha mgombea wao, Mchungaji Peter Msigwa zinaonesha amepata ushindi dhidi ya mgombea wa CCM, Fredericck Mwakalebela na wagombea wengine wanne walioshiriki kinyang’anyiro hicho.
Pamoja na Mchungaji Msigwa kudaiwa kupata ushindi huo, chama hicho pia kinaongoza udiwani katika kata 14 kati ya kata 18 za jimbo hilo, matokeo ambayo kwa mujibu wa Mwampashi yamekishtua chama chake, CCM.
No comments:
Post a Comment