Thursday, 26 November 2015

MKOA WA IRINGA UNA KIWANGO KIKUBWA CHA MATUKIO YA UKATILI WA KIJINSIA


 Msanii kutoka Kikundi cha Sanaa cha Mundu Cultural Groups maarufu kwa jina la Mussa Manyoka akionyesha umaili wake wa kucheza na nyoka wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliyofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa jana.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu (wa tatu kushoto) akipitia hotuba yake kabla ya kuisoma huku wageni wengine wakifuatilia burudani iliyokuwa ikitolewa na Kikundi cha Sanaa cha Mundu Cultural Groups wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliyofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa jana. (Picha zote na Friday Simbaya)

Mkoa wa Iringa ni mojawapo ya mikoa ambayo ina kiwango kikubwa cha matukio ya ukatili wa kijinsia, kutokana na utafiti uliyofanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Shirika la Taifa la Takwimu (NBS) mwaka 2012.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa (RAS), Wamoja Ayubu wakati wa uzinduzi siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliyofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa jana.

Alisema kuwa utatifi unaonyesha kuwa kiwango cha ukatili wa kijinsia katika Mkoa wa Iringa ni asilimia 54, na kuongeza kuwa kiwango hiki ni kikubwa ukilinganisha na wastani wa kitaifa wa asilimia 44.

RAS alisema kuwa utafiti huo unaonyesha kuwa kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya uwepo wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na ongezeko la Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi.

“Mkoa wetu wa Iringa ni mojawapo ya mikoa ambayo ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU na Ukimwi kwa kuwa na asilimia 9.1 (wanawake 10.9 na wanaume 6.9); na kufanya kuufanya kuwa mkoa wa pili Tanzania kwa kuwa na maambukizi ya VVU na Ukimwi baada ya Mkoa wa Njombe wenye asilimia 14.9 ya maambukizi,” alisema Ayubu.

Alisema kuwa uhusiano wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuongezeka kwa VVU na Ukmwi ni kutokana na ukweli kwamba vitendo vingi vya ukatili hasa wa kingono vinafanyika bila kutumia kinga, hivyo kuongeza kasi ya maambukizi VVU na Ukimwi.

Kadhalika mila na desturi hatarishi kama kurithi wajane, kuwa na wapenzi wengi, umasikini na ulevi uliopindukia huchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa ukatili wa kimwili na ukatili wa kingono, hivyo kupelekea kuongezeka kwa VVU na UKIMWI.

Ukatili wa kijinsia ni tatizo linalohitaji kuunganisha nguvu za pamoja kati ya serikali na Asasi zisizo ya kiserikali, madhehebu ya dini, vyama vya siasa na mtu binafsi kwa kuwajibika ipasavyo ili kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Mkoa wa Iringa.

Uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia hufanyika kila mwaka tarehe 25 Novemba, siku 16 za kupinga utakili wa kijinsia hujumuisha Siku ya Ukimwi duniani tarehe 01/12, Siku ya watu wenye ulemavu duniani tarehe 03/12 na Siku ya haki ya haki za binadamu tarehe 10/12 kwa kufanya shughuli mbalimbali yenye lengo la kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Aidha mashirika kama vile USAID, Engender Health, JHPIEGO-SAUTI, AFRICARE, WCS na UNICEF pamoja na maafisa kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii, Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Jeshi la Polisi na mahakama walishiriki katik kuandaa uzinduzi huo dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia mkoani Iringa jana.

Uzinduzi huo wa pamoja pia ulikwenda sambamba na kauli mbiu ya mwaka 2015 ya “FUNGUKA: Chukua hatua mlinde mtoto apate elimu” ilikuweza kuwafikia wananchi walio wengi zaidi.

Mwisho

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...