Wednesday, 4 November 2015

MWAKALEBELA AFUNGUA KESI YA KUPINGA MATOKEO


Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa , Elisha Mwampashi akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo (Picha na Friday Simbaya)


ALIYEKUWA mgombea ubunge Jimbo la Iringa Mjini, Frederick Mwakalebela, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), amefungua kesi mahakamani ya kupinga matokeo yaliompa ushindi, Mchungaji Peter Msigwa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kesi hiyo ya uchaguzi iliyofunguliwa kwa No. 5 ya mwaka 2015 imefunguliwa katika mahakama kuu kanda ya Iringa inatarajia kuanza kusikilizwa ndani ya siku 14 tangu kufunguliwa shauri hilo.

Mwakalebela alisema kuwa matokeo yaliyompa ushindi Mch. Msigwa yalikuwa ni ya kutengenezwa ili kumbeba mgombea huyo wa chadema kabla ya kufanyika kwa uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana (leo), Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa , Elisha Mwampashi kwa niaba ya mgombea alisema kuwa mgombea huyu atatumia haki ya kikatiba kupinga matokeo hayo mahakamani ili maoni ya wananchi kuheshimiwa na kupata haki zao za msingi.

Alisema kuwa chama hicho kimewashitaki watu wawili ambao ni msimamizi wa uchaguzi jimbo la iringa mjini pamoja na mshindi katika uchaguzi huo Mch. Peter Msigwa ambapo kila mmoja amewkewa bondi ya shilingi milioni tano.

Hata hivyo katika matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Ahmed Sawa alimtangaza Mchungaji Peter Msigwa aliyewania ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa mshindi baada ya kuzoa kura 43,154 dhidi ya kura 32,406 alizopata mgombea wa CCM, Frederick Mwakalebela. 

Wagombea wengine na kura zao kwenye mabano ni Chiku Abwao wa ACT Wazalendo (411), Daudi Masasi wa ADC (123), Paulina Mgimwa wa Chausta (66) na Robert Kisinini wa DP (56). 

Hivi karibuni Chama cha Mapinduzi CCM kilitangaza kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi ya majimbo manne ya Ndanda, Iringa Mjini,Kawe na Mikumi, kutokana na kile ilichodai kuwepo kwa ukiukaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hususan katika kujumlisha matokeo, hali iliyosababisha wabunge wa upinzani kutangazwa washindi.

Chama hicho katika madai yake, kimewatuhumu wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo hayo kuvuruga uchaguzi huo kutokana na ilichosema utata uliokuwa umejitokeza wakati wa zoezi la kujumlisha kura na kwamba licha ya chama hicho kuomba kuhesabiwa upya ilinyimwa haki hiyo, ambayo kimsingi iko kisheria.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni za CCM, January Makamba alipozungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam hivi karibuni.

Akizungumzia hilo, January alisema chama hicho hakijaridhishwa na utaratibu wa kukusanya na kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo ya Kawe, Ndanda, Mikumi na Iringa Mjini kutokana na kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hasa katika kujumlisha matokeo uliowezesha wabunge wa upinzani kutangazwa washindi.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...