Monday, 2 November 2015

Watahiniwa 15,818 mkoani Iringa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya sekondari leo



Picha/Maktaba



Kaimu afisa elimu mkoa wa Iringa, Euzebio Mtavangu amesema kuwa jumla ya watahiniwa 15,818 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya sekondari mwaka huu.

Mgawanyo wa watahiniwa hao katika halmashauri ni halmashauri ya Manispaa (4,785), halmashauri ya wilaya ya Iringa (3,368), halmashauri ya wilaya ya Kilolo (2,784) na halmashauri ya wilaya ya Mufindi (4,881).

Akiongelea matarajio ya ufaulu katika mkoa, Mtavangu alisema kuwa mkoa unatarajia kufanya vizuri na kupindukia matarajio ya BRN ya 80%.

Alisema kuwa matarajio hayo yanatokana na mkoa kuwa uliboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Sababu nyingine alizitaja kuwa ni wanafunzi wa masomo ya sayansi kufanya majaribio halisi baada ya kuwa na maabara za kutosha na kufanya ufaulu kwa masomo ya sayansi kuwa mzuri.

Aidha, wingi wa walimu wenye shahada umeongeza chachu ya mafanikio katika sekta ya elimu mkoani Iringa.

Mkoa wa Iringa umekamilisha maandalizi ya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka 2015 na mitihani yote imefikishwa vituoni.

Kauli hiyo ilitolewa na kaimu afisa elimu mkoa wa Iringa, Mwalimu Euzebio Mtavangu alipokuwa akiongelea maandalizi ya mitihani ya kumaliza kidato cha nne kwa mkoa wa Iringa ulionza leo nchini kote ofisini kwake.

Mwalimu Mtavangu alisema kuwa mkoa wa Iringa una jumla ya vituo 196 vya kufanyia mtihani huo.

Alivitaja vituo hivyo kwa kila halmashauri kuwa ni halmashauri ya Manispaa ya Iringa (44), halmashauri ya wilaya ya Iringa (33), halmashauri ya wilaya ya Kilolo (49), halmashauri ya wilaya ya Mufindi (70) na mitihani yote imefikishwa katika vituo husika.

Akiongelea idadi ya wasimamizi, alisema kuwa mkoa unao jumla ya wasimamizi 527.

Alisema kuwa kwa mujibu wa muongozo wa mitihani hiyo msimamizi mmoja anatakiwa kusimamia wastani wa watahiniwa 40.

Aliongeza kuwa wasimamizi hao miongoni mwao ni walimu kutoka katika shule za mkoa wa Iringa.

Utaratibu wa kuwapata wasimamizi hao ni pamoja na kuwafanyia upekuzi wa kina na kula kiapo cha kutunza siri kwa mujibu wa sheria Namba 3 ya mwaka 1970.

Alisema kuwa semina kwa wasimamizi wa mitihni hiyo zilianza kutolewa kwa halmashauri zote kuanzia tarehe 28-30/10/2015. 

(Na Friday Simbaya, Iringa)  

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...