Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe na Naibu wake Joseph Lyata,
Na Frank Leonard, Iringa
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe na Naibu wake Joseph Lyata, wote kutoka Chadema, wamekutana na wanahabari kwa mara ya kwanza ofisini kwao hii leo na kuainisha mikakati yao mbalimbali inayolenga kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Jimbo la Iringa Mjini katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Viongozi hao wanaunda halmashauri hiyo baada ya chama chao, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujizolea viti 14 kati ya 18 vya udiwani mjini Iringa huku nafasi ya ubunge ikichukuliwa na chama hicho kwa mara nyingine tena kupitia kwa mbunge yule yule wa 2010-2015, Mchungaji Peter Msigwa.
Kuhusu watendaji wa kata, mitaa na vijiji
1. Ni marufuku kuchukua fedha kwa wananchi wakati wakihitaji huduma ya muhuri kwa ajili ya barua za utambulisho, mikopo na zinginezo. Huduma hiyo ni bure sio ya kibiashara
2. Ni marufuku kwa watendaji na wenyeviti kujishughulisha na uuzaji wa viwanja katika maeneo yasio rasmi kama milimani na mabondeni ili kutoelendelea kuwapa hasara wananchi pindi mamlaka zinapolazimika kuwaondoa
Kuhusu barabara
1. Kwa kuwa ina greda kwa ajili ya kazi hiyo, halmashauri hiyo itajenga barabara katika maeneo yote ambayo ramani ya mipango mingi inaonesha kuna barabara zinapita ili wananchi wasirubuniwe na kuuziwa maeneo hayo kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo
2. Barabara ya samora, kijiweni hadi hospitali ya manispaa ya Iringa Frelimo imeanza kujengwa kwa kiwango cha lami
Mwaka wa masomo 2016
1. Wanafunzi wa darasa la kwanza wanatakiwa kuandikishwa bure na inawataka walimu wa shule zote za msingi hadi sekondari kidato cha nne wasithubutu kuwabugudhi wanafunzi kwa kuwadai michango yoyote ile kwasababu serikali imekwishatoa maelekezo kwamba elimu hiyo itatolewa bure bila michango yoyote
Iringa kuwa jiji
1. Halmashauri ya Chadema itahakikisha inazifanyia kazi taratibu zote zinazotakiwa ili mji wake upate hadhi ya jiji.
2. Ili kufanikisha ndoto hiyo sheria zote za mipango miji zitasimamiwa na kutekelezwa kwa umakini mkubwa
3. Halmashauri mji wa Iringa unakuwa mji wa maghorofa na kwamba wale wote waliopewa likizo ya kujenga maghorofa katika maeneo yanayotakiwa kisheria kujengwa nyumba hizo (katikati ya mji) watatakiwa kufanya hivyo kama muda waliopewa umekwisha. Vibali vya ujenzi wa maghorofa na nyumba nyingine za kisasa vitaendelea kutolewa
4. Ili malengo hayo yafikiwe, wafanyakazi wa halmashauri hiyo (wataalamu) watatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa majukumu yao, kuzingatia sheria kanuni na taratibu zote za kazi ikiwa ni pamoja na muda wanaotakiwa kuwepo au kuondoka kazini
Kuhusu kodi
1. Kodi za halmashauri zinazotozwa kwa wananchi wa halmashauri hiyo zitaangaliwa upya, ili zile zinazoonekana kuwa kero kwa wananchi wa kawaida zifanyiwe marekebisho
2. Kodi za lazima ambazo hazina kero kwa wananchi zitakusanywa kwa nguvu ili kufidia nakuongeza mapato ya halmashauri hiyo; kodi hizo ni pamoja na za majengo.
Kuhusu matumizi ya halmashauri
1. Halmashauri hiyo mpya imeahidi kusimamia na kupunguza matumizi yote ya halmashauri yasio ya lazima ili fedha zitakazookolewa zitumike kuboresha huduma za kijamii
Kuhusu Gari la kubeba wagonjwa na taka
1. Mapato yatakayokusanywa, yakiwemo yale kutoka kwa wale wanakwepa kodi za majengo yatatumika kununua gari la kubeba wagonjwa na hivyo kufuta ule mpango wa kuuza gari la Meya ili fedha zitakazopatikana zitumike kununua gari hilo
2. Mapato hayo pia yatatumika kununua gari lingine la kubeba taka ili kukidhi mahitaji ya kuung’arisha mji wa Iringa
Kuhusu Mikopo ya Vijana na Wanawake
1. Halmashauri hiyo ya Chadema itafuatilia marejesho ya mikopo yote iliyotolewa kwa makundi hayo ili makusanyo yake yaendelee kuwanufaisha wananchi wengine
Kuhusu uwekezaji
1. Maeneo yaliyopendekezwa kwa ajili ya uwekezaji vitega uchumi vitakavyoiongezea mapato halmashauri hiyo kama ujenzi wa miradi mikubwa ya vitega uchumi katika maeneo ya Tembo Bar na Kilabu cha Kijiweni yatafanyiwa kazi kwa haraka.
Mapema mwaka 2011, halmashauri hiyo kwa kupitia aliyekuwa Meya wa Manispaa hiyo, Amani Mwamwindi iliahidi kuyabomoa majengo hayo ili kupisha uwekezaji mkubwa utakaoongeza mapato ya halmashauri hiyo.
Wakati Tembo Bar ipo pembeni mwa stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani, mjini Iringa, kilabu cha Kijiweni kipo karibu na Chuo cha Ufundi Stadi cha Veta.
Katika eneo la Tembo Bar, mpango wa halmashauri hiyo ulikuwa ni kujenga jengo la ghorofa tano na kituo cha mafuta huku katika kilabu cha Kijiweni mpango ulikuwa ni kujenga maegesho, ukumbi wa muziki, sherehe, bar, hoteli, maduka makubwa, ukumbi wa mazoezi na bwawa la kuogolea.
Kuhusu wamachinga
1. Halmashauri itakaa ili kuyapitia maamuzi ya halmashauri iliyopita yaliyowaondoa machinga katika gulio la Jumamosi na Jumapili katika eneo la mashine tatu ili wafanyabishara hao wapate fursa hiyo.
2. Ahadi hiyo itakwenda sambamba na kutafuta maeneo mengine kwa ajili ya wafanyabiashara hao
Kuhusu Michezo
1. Halmashauri itaangalia uwezekano wa kuwa na timu moja itakayosaidiwa kwa nguvu ya halmashauri na wadau wake ili kiu ya watu wa Iringa ya kuona wana timu inayoshiriki ligi kuu ifanikiwe
Kuhusu Mazingira
1. Halmashauri itatumia rasilimali zake, wakiwemo wananchi wenyewe kuhakikisha wanaufanya mji wa Iringa kuwa Mji wa Kijani kwa kupanda miti mingi huku mazingira yake yakiwekwa safi siku zote.
Kuhusu Biashara
1. Halmashauri ya Chadema itahakikisha wafanyabishara wanatengenezewa mazingira mazuri yatakayowafanya wafanye biashara zao bila kuvunja sheria, taratibu na kanuni zingine.
Kuhusu huduma za afya na maji
1. Halmashauri hiyo imeahidi kuziimarisha huduma hizo kwa kushirikiana na wadau wengine wote muhimu ili afya za wakazi wa Iringa ziimarike
Huduma zinginezo
1. Zitatekelezwa kwa kushirikiana pasipo kupindishwapindishwa na serikali ya awamu ya tano ya Dk John Pombe Magufuli
Kuhusu wanahabari
1. Halmashauri hiyo itahakikisha wanahabari wanashirikiana nao vyema ili kufikia malengo yao. Kutakuwepo na utaratibu wa kukutana na wanahabari wote kila baada ya miezi mitatu au pale inapohitajika kulingana na mahitaji yenyewe
No comments:
Post a Comment