Thursday, 24 December 2015

KIJIJI CHA ITENGULE HAKINA OFSI YA MASIJALA YA ARDHI







MKUU wa Wilaya Mufindi, Jowike Kasunga amewataka wananchi wa Kijiji cha Itengule, Kata ya Malangali kuharakisha ujenzi wa ofisi ya masijala ya ardhi unaoendelea katika kijiji hicho ili uweze kukamilika haraka kwa ajili ya kuhifadhi vifaa vya masijala. 

Katika hotuba yake hiyo iliyosomwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi Allan Bernard kwa niaba yake jana, alisema kuwa wananchi kwa kushirikiana na serikali yao ya kijiji wanatakiwa kushiriki katika ujenzi wa ofisi ya masijala ili, kabati la chuma, mhuri wa moto (lakiri) na daftari la usajili wa hati za kimila viweze kuhifadhiwa salama.

Jumla ya wananchi 296 wa kijiji cha itengule wapatiwa hati za hakimiliki za kimila na halmashauri ya wilaya ya mufindi kwa msaada ya taasisi Haki ardhi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo jana.

Kasunga alisema kuwa wananchi wa Kijiji cha Itengule ni lazima watunze hati hizo za kimila vizuri kwa ajili ya manufaa yao wenyewe, ikiwa ni pamoja na kuzitumia hati hizo kama dhamana kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Aliongeza kuwa hati za kimila zinaweza kutumika kama dhamana katika taasisi mbalimbali za kifedha kwa ajili ya kupatiwa mikopo na hatimaye kuboresha maisha yao.

Taasisi ya Hakiardhi imewezesha upatikanaji wa vifaa vya masijala kwa vijiji vinne vya Itengule, Itulituli, Igomaa na Tambalang’ombe.

Aidha, halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa imepima mipaka ya vijiji 113 kati ya 114 vilivyopo katika halmashauri hiyo. 

Akisoma taarifa kuhusu shughuli za ugawaji hati za hakimiliki za kimila katika Kijiji cha Itengule jana Ofisa Ardhi Mteule Leonard Jaka alisema kuwa bado kijiji kimoja (1) cha Mpanga Tazara ambacho kimepangwa kupimwa katika kipindi cha mwaka huu wa fedha.

Jaka alisema shughuli ya urasimishaji wa ardhi wilayani Mufindi kwa madhumuni ya utoaji wa hati za hakimiliki za kimila vijijini ulianza katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011.

Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Hakiardhi ambayo ni taasisi ya inayoshughulisha na masuala ya utafiti na utetezi wa haki za ardhi, wamegawa hati za hakimiliki za kimila 296 kwa wananchi wa kijiji cha Itengule, kata ya Malangali wakiwemo wajane. 

Alisema kuwa vijiji 45 kati ya 114 vinayo mipango ya matumizi ya ardhi ambapo juhudi zinaendelea kwa vijiji vingine kwa kutenga fedha kwenye bajeti kila mwaka na kuwahusisha wadau wengine.

Alisema kuwa halmashauri pia imeandaa vyeti vya vijiji (Village Land Certificate) 92 kati ya 114 ambapo jitihada zinaendelea ili kukamilisha vijiji 22 vilivyobaki kwa kufuatilia ramani za vijiji 19 Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi.

Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa kushirikana na Hakiardhi ilianza kazi ya utoaji wa hati za hakimiliki za kimila ambapo mpaka sasa hati 1,661 zimetolewa katika vijiji mbalimbali wilayani humo.

“Katika kipindi cha mwaka 2015/16 halmashauri imetenga katika bajeti yake kiasi cha 12,000,000/- kwa ajili ya mchakato wa utoaji wa elimu ya sheria za ardhi na hatimiliki za kimila ambapo imeandaa pia mpango wa kuwashirikisha wananchi katika kupima ardhi yao ili mchakato wa utoaji wa hatimiliki za kimila uwe enedelevu,” alisema Jaka.

Wananchi wa Kijiji cha Itengule, Kata ya Malangali waliishukuru Taasisi ya Hakiardhi pamoja na halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa kuwapatia hati za hatimiliki za kimila na kusema pia hati hizo zitasaidia kuondoa migogoro ya ardhi hasa ile ya mipaka.

Venanza George ambaye ni mjane alisema kuwa baadhi ya wanaume kijijini hapo walikuwa na tabia ya kupokonya wanawake ardhi na pengine baada ya kufiwa na wanaume zao, ndugu kwa upande wa wanaume uchukuwa vitu vyote vya marehemu. 

Lakini kwa sasa wameweza kutafuta haki yao hivyo haki ya kumiliki ardhi kwa wanawake hasa wajane imetambuliwa na imeanza kutekelezwa kwa vitendo.

Kwa upande wake, Ofisa ufuatilaji na tathmini wa taasisi ya Hakiardhi Allan Baino alisema kuwa Hakiardhi kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya mufindi imeendesha shughuli ya utoaji wa elimu ya masuala ya ardhi, utawala na mabadiliko ya tabianchi katika vijiji 30.

Baino alisema kuwa lengo la mradi ulikuwa ni kutoa uelewa mpana kwa jamii juu ya sheria ya ardhi, utawala vijijini na mabadiliko ya tabianchi iliweze kuzalisha chakula na kuwa na usalama wa chakula hususani kwa wazalishaji wadogo.

Alisema kuwa jumla ya 15 katika wilaya ya mufindi vimepatiwa elimu ya ardhi, utawala na mabadiliko ya tabianchi ambavyo ni Itengule, Mwilavila, Itulituli, Kihanga, Mninga, Kitiru, Ikimilinzowo na Nyololo-Shlueni.

Vingine ni Nzivi, Ukemele, Ihegele, Ikweha, Uyela, Igeleke na Vikula, sawa na asilimia 100 ya lengo ya mradi.

Hadi mwaka wa fedha 2015/2016 jumla ya mashamba na viwanja 1,554 vimepimwa ambavyo ni Kisasa, Magunguli, Wami-Mbalwe, Itengule, Itulituli, Igomaa na Tambalang’ombe.

Shirika la Hakiardhi liliandaa bajeti ya kazi ya urasimishaji wa mashamba na viwanja Wilaya ya Mufindi 105,960,000/- kwa lengo la kurasimisha ardhi na kununua vifaa vya masijala vijijini.



Aidha, taasisi hiyo imewezesha upatikanaji wa vifaa vya masijala kwa vijiji vinne vya Itengule, Itulituli, Igomaa na Tambalang,ombe.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...