Wednesday, 9 December 2015

MANISPAA YA IRINGA YAELEMEWA NA TAKA


Mstahiki Alex Kimbe – Meya Manispaa ya Iringa


Mhandisi Omary Said – Mtumishi NHC Iringa

Emmanuel Kileka – Mkazi Manispaa ya Iringa

George Mwai – Mkazi Manispaa ya Iringa

Humphrey Kishimbo – Meneja wa NHC Iringa 
(Picha zote na Friday Simbaya)





LICHA ya wakazi wa Manispaa ya Iringa kuitikia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais John Pombe Magufuli la kuadhimisha siku ya Uhuru wa Tanganyika kwa kufanya usafi, wakazi hao wameitaka Manispaa hiyo kutii agizo hilo kwa kuondoa taka zinazozagaa mitaani.

Hata hivyo,Manispaa hiyo imesema kuongezeka kwa taka mitaani hususan katika vituo maalum vya kukusanyia taka ni kutokana na wananchi kuitikia kwa wingi agizo la Rais la kufanya usafi.

SIMBAYABLOG ilishuhudia baadhi ya vituo vya kukusanyia taka katika Manispaa ya Iringa vyombo vyake vikiwa vimejaa na wakazi wake kulazimika kumwaga chini hali inahatarisha zaidi afya za wakazi wa Manispaa hiyo.

Wakizungumza na SIMBAYABLOG wakazi wa Manispaa wa Iringa, Emmanuel Kileka na George Mwai kwa nyakati tofauti walilalamikia Manispaa hiyo kutokuwa na makontena ya kutosha kwa ajili kuwekea taka, ambapo kunawalazimu wananchi hao kutopa taka chini.

Walisema pia kuwa Manispaa ya Iringa imezidiwa na mrundikano wa taka kunakotokana na kuchelewa kuzoa taka katika vituo vilivyotengwa.

Pamoja na kasoro hizo, Mitaa ya Manispaa ya Iringa imeshuhudia pilika pilika za kufanya usafi ambazo hazijawahi kutokea huku kila mtu sehemu alipo na hata watumishi wa ofisi mbalimbali za serikali na mashirika ya umma wameonekana kuwa katika harakati kubwa za kufanya usafi.

Naye Meneja wa Shirika la Nyumba (NHC) Iringa, Humphrey Kishimbo alisema kuwa ni jambo zuri kwa Rais John Pombe Magufuli kuamua kufuta sherehe za Uhuru za miaka 54 ya Tanzania Bara na badala yake siku kuu hiyo kuwataka wananchi nchini kote kutumia kufanya usafi katika maeneo yao ya kazi na makazi.

Alisema kuwa siku kuu sio lazima kufanya masherehe badala siku kuu kama hizo zitumike kufanya kazi za kujitolea.

Mtumishi NHC Iringa, Mhandisi Omary Said aliongeza kuwa watanzania ni lazima wajijengea tabia ya kufanya usafi wa mara kwa mara na sio mpaka kusubiri mpaka rais atangaze kufanya usafi.

Alisema kuwa ili nchi iweze kuondokana na magonjwa ya milipuko kama kipindupindu ni lazima kujenga tabia ya kufanya usafi wa mazingira ya kiwemo maeneo ya kazi na makazi.

Akizungumzia changamoto ya taka kurundikana katika vituo vya kukusanyia taka hizo, Meya wa Manispaa ya Iringa, Mstahiki Alex Kimbe alisema kuwa Manispaa hiyo inakabiliwa na uhaba wa magari ya kubebea taka baada ya magari matatu kuharibika lakini pia akasema kujitokeza kwa wingi kwa wananchi katika siku hiyo ya usafi kumeongeza mara dufu taka zilizopelekwa kwenye vituo hivyo zikisubiri kusafirishwa kupelekwa dampo.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...