WANANCHI wa kijiji cha Lyamko kilichopo katika Kata ya Bomalang’ombe Wilayani Kilolo wamepatiwa hati miliki za kimila 350 baada ya kupimiwa mashamba yao na shirika linalojishughulisha na masuala ya ardhi nchini (HakiArdhi) kwa kushirikiana na halmashauri hiyo.
Akizungumza kijijini hapo juzi mara baada ya wananchi hao kupatiwa hati miliki zao, Ofisa Ardhi Mteule Elinaza Kiswaga alisema kuwa kijiji hicho kimekuwa kijiji cha nane ndani ya wilaya hiyo kupatiwa hati miliki za kimila tangu zoezi la upamaji mashamba kuanza mwaka 2013.
Kiswaga alisema kuwa taasis ya haki ardhi ilianza kufanya kazi za utafiti wa awali mwaka 2012, na mwanzoni mwa mwaka 2013 taasisi hiyo kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya hiyo ilianza rasmi kutoa mafunzo ya sheria ya ardhi, utawala vijijini na mabadiliko ya tabianchi.
Kiswaga alisema kuwa lengo la mradi ulikuwa ni kutoa uelewa mpana kwa jamii juu ya sheria ya ardhi, utawala vijijini na mabadiliko ya tabianchi hususani kwa wazalishaji wadogo.
Naye Ofisa ardhi mteule wa wilaya hiyo alisema kuwa taasisi hiyo ya hakiardhi ilitoa mafunzo ya sheria ya ardhi na utawala vijijini pamoja na mabadiliko ya tabianchi katika vijiji 55, kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwa vijiji 11 ambavyo ni Kihesamgagao, Kidabaga, Kiwalamo, Kitelewasi, Kipaduka, Uhambingeto, Lugalo, Lyamko, Ibofwe, Itonya na Ilamba.
Kwa upande wake Mejuzi Mgeveke ambaye ni makamu mwenyekiti wa halmashauri ya kilolo aliishukuru taasisi hiyo kwa kuendesha shughuli hizo katika wilaya ambazo zimeleta mafanikio makubwa.
“Ni dhahiri kuwa mafunzo hayo yamesaidia kuleta chachu ya mabadiliko kwa jamii ya watu wa kilolo katika ngazi zote hasa juu ya uelewa wa masuala ya ardhi, utawala bora na mabadiliko ya tabia nchi.”alisema Mgeveke
Hata hivyo mkurugenzi mtendaji wa haki ardhi Yefred Myenzi, amesema katika utekelezaji wa shughuli hizo kumekuwepo na mafanikio makubwa ambayo ameshuhudia vijiji 11 kuandaliwa mipango ya matumizi bora ya ardhi, kiasi ambacho kimesadia kupunguza migogoro mingi ya ardhi.
Myenzi alisema kuwa migogoro hiyo ni ile inayotokana na mwingiliano wa matumizi baina ya uhifadhi wa misitu asili.
Alisema kuwa taasisi ya hakiardhi imefanyika na kufika vijiji 55 kati ya zaidi ya vijiji 106 vya wilaya hiyo na bado mwamko ni mkubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo kutakifiwa na zoezi la upimaji mashamba.
“Hivi Kwa mfano, katika kijiji cha Lyamko kililengwa kupima mashamba 350 lakini wananchi waliojitokeza kwa wingi kiasi cha kufikia wananchi 351 na wengine ilishindikana kupimiwa na tutajitahidi hadi kuwafikia wote na kuwapimia.”alisema Myenzi
Maria Nzala alisema kuwa mume wake alikuwa hataki yeye kumiliki ardhi lakini ameweza kutafuta haki yake na kuipata kisawasawa,hivyo haki ya kumiliki ardhi kwa wanawake imetambuliwa na imeanza kutekelezwa kwa vitendo,pia itasaidia kuondoa migogoro baina ya wanaumeambao hawataki wanawake kutumia ardhi.
No comments:
Post a Comment