Mchungaji wa kanisa la Umoja wa Makanisa ya Ubatizo Lucas Machibya akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani ) kuhusu baadhi ya shughuli za uraghabishi katika kijiji cha Pandagichiza
Na Krantz Mwantepele ,Shinyanga
Si mara nyingi viongozi wa kidini hujihusisha moja kwa moja na harakati za kisiasa ila wamekuwa mstari wa mbele kukemea matendo yanayofanywa na wanasiasa. Hawafanyi hivyo kwa bahati mbaya ila kutokana na nafasi yao katika jamii, hususani kuwaongoza waumini wao kwenda mbinguni.
Hata hivyo, hii haimaanishi hakuna kabisa viongozi wa dini waioamua kujiingiza katika harakati za siasa ili kuleta maendeleo ya watu kwa haraka na ufanisi. Mchungaji Lucas Machibya ni mmoja kati ya viongozi wachache wa dini wanaoingia katika siasa.
Huyu ni mchungaji wa kanisa la Umoja wa Makanisa ya Ubatizo lililopo katika kijiji cha Pandagichiza chenye wakazi wanaokadiriwa 2,481, idadi kubwa ikiwa ni ya wanawake wanaokadiriwa kufikia 1,476. Hiki ni moja ya vijiji vilivyopo wilaya ya Shinyanga Vijijini, jimbo la Solwa.
Machibya ni mmoja wa wachungaji waraghbishi toka mkoa wa Shinyanga ambao uraghbishi wao umepelekea wananchi kumchagua kuwa mwenyekiti wa kijiji. Kujibainisha kwake kama mtu mwenye uwezo wa kusimamia anachokiamini na kushawishi wananchi kutambua majukumu na haki zao na jinsi ya kuzidai vimekuwa nguzo yake kubwa ya kukubalika.
Kama walivyo wananchi wengi wa kijiji chake, yeye ni mkulima mdogo ambaye pia ni mwanachama wa Mtandao wa Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA). Kupitia mwaliko wa mkulima mwenzake, Elizabeth Edward, Machibya amefanikiwa kupata maarifa ya uraghbishi na jinsi ya kufanya uraghbishi; uwezo wa kuwashawishi na kuwahusisha ama kuwachokoza watu ili waweze kujitambua na kutojiona wao ni wa jamii ya chini.
Sifa iliyomfanya aalikwe kwenye mafunzo ya uraghbishi ni uwezo wake wa kuhoji mambo mbalimbali pasipo kukata tamaa kama anavyosema mwenyewe:
“Mimi ni mtu wa kuhoji vitu na si mtu wa kuridhika ama kukaa kimya n’napoona kuna jambo sijalielewa. Kwa kweli yale mafunzo yalinifanya kujiona mtu tofauti sana nikijilinganisha na nilivyokuwa awali. Nilijihisi tayari nimekuwa mtaalamu wa masuala ya uwajibikaji na utawala
bora.”
Kwa kuwa wao ni wakulima, walianza uraghbishi wao kwa kutaka kujua nini kinaendelea kuhusu bei ya pamba. mchungaji Machibya anaeleza ilivyokuwa:
“Kule tulifundishwa jinsi ya kuuliza maswali. Na cha kwanza tulichotaka kujua ni kwa nini bei ya zao letu la pamba imeshuka sana. Hili tuliliuliza sisi sote, mimi na waraghbishi wengine.”
Hawakuishia hapo tu bali wakaanza pia kufuatilia mapato na matumizi ya fedha za kijiji toka kwa viongozi wao. Walifanya hivyo kwa kuwatembelea ofisini na kuomba kupatiwa taarifa hizo na pia walitaka kufanyika mikutano ya hadhara. Baada ya harakati hizo kushika kasi, iliwabidi waongeze watu wengine zaidi kwa kuwatembelea majumbani kwao na kuwaraghbisha.
“Mchungaji aliomba kunitembelea nyumbani na alipofika alinipatia elimu. Kimsingi, alitaka nijitambue kwa kujua wajibu na haki zangu. Alinitaka nisiogope kuuliza maswali kwenye mikutano kwa
kuwa tuna uhuru wa kufanya hivyo. Nikajua kuwa nina wajibu kuuliza na kujua mapato ya fedha za kijiji na na matumizi yake kuwa hiyo ni haki yangu,” anaeleza Bw. Daudi
Denis toka kijiji cha Pandagichiza.
Baadhi ya waraghabishi wa kijiji cha Pandagichiza wakiwa na waandishi wa habari za mtandaoni katika moja ya jengo la jiko la shule ya msingi Pandagichiza ambalo limetoakana na juhudi zao za uraghabishi
Kufanikisha haya yote kumewajengea uaminifu mkubwa sana waraghbishi na baadhi yao wamekuwa wakishirikishwa katika
vikao muhimu vya maendeleo na serikali yao ya kijiji. Baadhi yao wametokea kuaminika zaidi na jamii kiasi cha kuombwa wagombee nyadhifa mbalimbali za uongozi wa serikali na ndani ya vyama vya siasa kama ilivyokuwa kwa mchungaji
Machibya.
No comments:
Post a Comment