SIMBA NA YANGA ZAKUTANA MARA 81, NANI ATASHEREHEKEA!
Na Daniel Mbega
JUMAMOSI hii Februari 20, 2016 bingwa wa ‘kucheka na nyavu’ wa miaka yote Uingereza, James Peter ‘Jimmy’ Greaves, atakuwa anasherehekea miaka 76 ya kuzaliwa kwake, lakini kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kutakuwa na habari nyingine wakati mahasimu wakuu wa soka Tanzania, Yanga na Simba watakapokuwa wakivaana kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Timu hizo zinapambana katika siku ya 51 ya mwaka, lakini ni baada ya siku ya 112 tangu zilipopambana mara ya mwisho – katika mchezo wa kwanza wa msimu wa 2015/2016 – Septemba 26, 2015 kwenye uwanja huo huo na Yanga wakaibuka washindi kwa mabao 2-0 wakilipa kisasi cha kufungwa ‘bao la kizembe’ na pekee Machi 8, mwaka huo lililopachikwa kimiani na Emmanuel Okwi.
Achana na akina Alan Shearer, Wayne Rooney na Thierry Henry, mkongwe Greaves ndiye mchezaji pekee aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye ligi ya juu (top flight) wakati huo ikiwa Ligi Daraja la Kwanza, ambapo alipachika wavuni mabao 357 dhidi ya 260 ya Shearer.
Jambo la kufurahisha zaidi, mabao 268 kati ya hayo yalifungwa na Greaves akiwa na Tottenham Hotspurs pekee, wakati yale ya Shearer alifunga katika klabu za Blackburn Robers na Newcastle United.
Greaves pia ndiye mchezaji pekee katika ligi ya Uingereza kuibuka mfungaji bora kwa misimu sita na alicheza ligi hiyo kati ya mwaka 1957 hadi 1972.
Kwamba ni timu gani kati ya Yanga na Simba itakayosherehekea ushindi na kuungana na Greaves kwenye ‘birthday’ yake Jumamosi hii ni jambo lililo gumu kutokana na rekodi ya timu hizo mbili, ambazo kimsingi ndizo zilizoleta mwanga wa soka nchini.
Tangu Simba ilipozinduka kutoka katika kufanya vibaya kwenye ligi na hatimaye kukalia usukani mpaka sasa, kumwekuwa na mhemko mkubwa baina ya timu hizo mbili, mashabiki na wanachama wake wakitambiana kwamba timu yao itaibuka na ushindi.
Huku zitasikika kelele za: “Amesimama kidedea, eeeh kidedea!” na kule: “Kitimtimu, mtakiona leo, nyumba ya shetani mwendawazimu kaingiaje!”
Lakini kelele hizo zitahitaji pia kuangalia matokeo ya uwanjani yakoje, vinginevyo upande mmoja unaweza kuzizima.
Hapo hakuna ugomvi, ni burudani ya jukwaani huku mashabiki wakiendelea kutazama buradani nyingine ndani ya uwanja wakati vijana walio katika jezi nyeupe na nyekundu wakipelekeshana puta na wenzao walio kwenye jezi za kijani na manjano.
Matokeo baina ya mechi hizo daima huwa hayatabiriki na tangu Simba ‘walipoikanyaga’ Yanga kwa mabao 5-0 Mei 6, 2012, wamevuna ushindi mmoja tu wa Machi 8, 2015 wakati Okwi alipopachika bao la pekee huku kipa wa Yanga akiwa ametoka langoni.
Itakumbuka kwamba, katika kipindi baada ya kipigo kile cha aibu kwa Yanga, timu hizo zimekutana mara saba, Yanga ikishinda mara mbili na Simba mara moja, huku zikitoka sare mechi nne.
Zilipokutana Oktoba 3, 2012 zilitoka sare 1-1, mechi ya Mei 18, 2013 Yanga wakashinda 2-0, Oktoba 20, 2013 timu zikatoka sare ya 3-3, Aprili 19, 2014 sare ya 1-1 na Oktoba 18, 2014.
Simba inaingia uwanjani ikiwa haina mshambuliaji mwiba wa Yanga – Okwi – lakini Yanga inao wachezaji wake wote wawili walioipa ushindi Septemba 26, 2015 ambao ni Amissi Tambwe aliyefunga dakika ya 44 na Malimi Busungu aliyepachika dakika ya 79 ambaye pia ndiye aliyetoa pasi ya bao la kwanza.
Lakini mechi hiyo ilishuhudia Mbuyi Twite akipewa kadi nyekundu baada ya kupokea kadi ya pili ya njano kwa kuchelewesha muda.
Yanga, bingwa mtetezi, ndiyo ina kibarua kigumu Zaidi kwa sababu licha ya kupitwa mchezo mmoja na Simba, inahitaji kushinda mechi hiyo ili iweze kurejea kileleni.
Simba ina pointi 45 baada ya kushuka dimbani mara 19 wakati Yanga imecheza mechi 18 na ina pointi 43, hivyo ikiwa Yanga itashinda, basi itafikisha pointi 46 na kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa wake.
Kupoteza mechi hiyo kuna maana moja kwa Yanga, itakuwa imeuweka rehani ubingwa wake kwa sababu Simba, ambayo tangu ilipomtimua kocha wake Dyran Kerr na kumwajiri Mayanja Jackson imeshinda mechi sita mfululizo, ina hasira za kuukosa ubingwa huo kwa misimu mitatu na sasa ndio wakati wake.
Matokeo ya sare bado hayatainufaisha Yanga, lakini itakuwa ni faida kwa Simba ambayo itakuwa na uhakika wa kuhamishia ushindani wake kwa Azam inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na mechi mbili mkononi na kukusanya pointi 42.
Mechi baina ya timu hizi mbili kongwe katiba katika historia ya kandanda nchini huwa zinatawaliwa na vituko vingi mno. Kuvunja nazi, kuoga maji ya maiti, kuruka ukuta, kuingia uwanjani kinyumenyume na mengine kama hayo hutajwa kwamba ni sehemu ya kuhanikiza ushindani.
Hata hivyo, kwa sasa hawawezi kuruka ukuta kama ilivyokuwa miaka ile ya zamani, wala hawawezi kuoga maji ya kuoshea maiti au kuvunja nazi hadharani, kwa sababu Sheria za Soka haziruhusu ushirikina na timu hizo mbili zimekwishawahi kutozwa faini kwa vitendo hivyo.
Safari hii timu zote zinatokea visiwani – Simba ilikuwa imepiga kambi Unguja na Yanga, baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius, ilikwenda moja kwa moja kisiwani Pemba.
Mechi zao
Hii itakuwa mechi ya 81 kuzikutanisha Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu tangu mwaka 1965 ilipoanzishwa Ligi ya Taifa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Milan Celebic.
Katika kipindi chote hicho, msisimko wa kuelekea mechi hizi umekuwa mkubwa, bila kujali nani anawania kitu gani.
Hata hivyo, katika mechi 80 zilizopita, Watanzania wameshuhudia Yanga ikitawala zaidi kwa kushinda mara 30, wakati Simba imeshinda mara 23. Timu hizo zimetoka sare mara 27 huku mabao 165 yakifungwa. Kati ya mabao hayo, Yanga imefunga 89 na Simba imefunga 77. Ikumbukwe kwamba, mechi hizi hazihusishi mechi za Ligi ya Muungano wala mashindano mengine.
Msimamo kamili wa Yanga na Simba:
Yanga 80 30 27 23 89 – 77
Simba 80 23 27 30 77 - 89
Azam, ambayo Jumapili Februari 14, 2016 ilipata kipigo cha kwanza iliponyukwa na Coastal Union bao 1-0 jijini Tanga, Jumamosi hii itakuwa ugenini kwa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine ikitaka kufufua matumaini ya kunyakua ubingwa huo kwa mara ya pili.
Lakini Mbeya City nayo inaonekana kuwa imara tangu ilipomuajiri mchezaji wa zamani wa Malawi, Kinnah Phiri, ambapo Februari 14, 2016 iliichabanga Toto African mabao 5-1 hapo hapo Mbeya.
Majimaji, ambayo inashika nafasi ya pili kutoka mkiani, itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar mjini Songea huku ‘Wakata Miwa’ hao kutoka Turiani wakihitaji ushindi kujiimarisha Zaidi kwenye nafasi ya nne nyuma ya Azam.
Maafande wa Mgambo Shooting walio katika nafasi ya 11 huku wakiugulia kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa African Sports ‘Wana Kimanumanu’ Februari 13, 2016, watawakaribisha ‘Wajelajela Gwaa’ Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Wakatisha tiketi wa Shinyanga, Stand United, ambao Februari 13, 2016 walizabuliwa mabao 2-1 na Simba kwenye uwanja wao wa nyumba – Kambarage – Jumamosi hii wanawakaribisha maafande wa JKT Ruvu Stars wakihitaji ushindi ili kuondoka katika nafasi ya saba waliko na pointi 29.
‘Wana Kishamapanda’ Toto African wao watakuwa nyumbani kuwakaribisha jirani zao wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, wakitaka kuwaaminisha mashabiki wao kwamba wako vizuri na wanaweza kuwapiku Mbeya City katika nafasi ya nane ambako wanafungana kwa pointi 21. Kagera Sugar iko nafasi ya 14 na inahitaji ushindi ili iepukane na balaa la kushuka daraja msimu huu.
Mwadui inayoshika nafasi ya sita, itaikaribisha Coastal Union ambayo inashika nafasi ya 13 na iko kwenye hatari ya kushuka daraja kama ilivyo kwa ndugu zao African Sports ambao Jumamosi hii watakuwa ugenini kwa Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Ratiba ya mechi za Jumamosi 20/02/2016:
Majimaji - Mtibwa Sugar
Mbeya City - Azzam
Mgambo - Tanzania Prisons
Stand U. - Ruvu Stars
Toto Africans - Kagera Sugar
Young Africans - Simba
Mwadui - Coastal Union
Ndanda - African Sports FC
Msimamo ulivyo sasa:
P W D L G Pts
1. Simba 19 14 3 2 35:11 45
2. Young Africans 18 13 4 1 42:9 43
3. Azzam 17 13 3 1 31:11 42
4. Mtibwa Sugar 18 9 6 3 21:12 33
5. Tanzania Prisons 18 8 6 4 18:17 30
6. Mwadui 19 8 5 6 19:16 29
7. Stand U. 18 9 2 7 18:15 29
8. Mbeya City 19 5 6 8 20:23 21
9. Toto Africans 19 5 6 8 18:27 21
10. Ndanda 19 4 8 7 17:19 20
11. Mgambo 19 4 5 10 15:24 17
12. Coastal Union 19 3 7 9 12:20 16
13. Kagera Sugar 19 4 4 11 10:22 16
14. African Sports FC 19 4 4 11 6:19 16
15. Majimaji 19 4 4 11 11:32 16
16. Ruvu Stars 19 3 5 11 18:34 14
CREDIT: FIKRAPEVU
No comments:
Post a Comment