CHUNYA: MADIWANI na viongozi wa vijiji wilayani Chunya katika Mkoa Mpya wa Songwe,wametakiwa kusimamia na kulinda Sheria za misitu ili kuweza kupunguza tatizo la uvamizi wa maliasili hiyo mhimu unaofanywa na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu.
Hayo yalisemwa Mwishoni mwa Wiki na Mkuu wa wWlaya hiyo, Elias Tarimo, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo ambapo alisema kuwa haiwezekani wavamizi wa misitu wanavuna misitu mpaka kufikia hatua ya kuhatarisha uwepo wake wakati viongozi hao wanaangalia.
Aliwaagiza madiwani pamoja na viongozi wengine wa vijiji kuwa walinzi kwa kuanzia katika maeneo yao kabla ya wavamizi hawajakamatwa na uongozi wa Wilaya kwa madai kuwa hali hiyo inapunguza hali ya uwajibikaji.
Alisema inatakiwa kuchukua hatua madhubuti za kuzuia vituo vilivyo wekwa vya kuzuia mazao hayo kupitisha, na wale ambayo wamekuwa ni wazembe kwa kushindwa kuzuia katika vizuizi wafukuzwe na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
“Inasikitisha misitu inaharibiwa kwa kiasi kikubwa wakati madiwani na viongozi wa vijiji mkiwa mpo katika maeneo hayo, hamuwezi kuwa na kisingizio cha kwamba hamuwaoni maana mpaka viongozi wa Wilaya wanakuja kuwakamata wahalifu kwenye maeneo yenu pamoja na kuwa wanakuwa ni wageni, hivvyo nawaagiza kuwa walinzi wa misitu hiyo na sitarajii uhalifu huo kuendelea,” alisema Tarimo
Aliwataka wananchi wa wilaya hiyo hasa wale wa vijijini kusaidia Serikali katika kutoa taarifa juu ya waharifu hao wa misitu ili kuweza kuwadhibiti kwa madai kuwa endapo misitu hiyo itakwisha madhara yatawakumba wao.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Chunya, Bosco Mwanginde, alisema pamoja na kupitisha bajeti hiyo mapato ya ndani yakikusanywa kiuhakika kwa kuanza kuzuia wezi wa mazao ya mistu mapato yataongezeka zaidi.
Alisema kumekuwepo na tabia ya kuvuna Mbao na kupitishwa usiku hali ambayo ni wizi wa kuiibia Halmashauri mapato, ambapo aliwambia madiwani kusaidia kuinua mapato ya halmashauri kwa kuzunguka maeneo yote ambayo mazao ya misitu yanavunwa ili wenye vibali vya kufanya shughuli hiyo walipe ushuru na wasio navyo wakamatwe na kuchukuliwa hatua.
Akisoma mapendekezo ya bajeti hiyo katika kikao cha baraza la madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Sophia Kumbuli, alisema bajeti hiyo imependekezwa kwa lengo la kuiinua wilaya hiyo.
Kumbuli alisema katika bajeti hiyo wamependekeza kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 35.9 na kwamba matumizi ya kawaida na Mishahara watatumia shilingi Bilioni 24.4 miradi ya Maendeleo bilioni 7.8 na matumizi mengineyo Bilioni 3.6.
Alisema kiasi cha shilingi bilioni 1.1 zitakuwa kwa ajili ya maendeleo ngazi ya wilaya na vijijini, mpango wa kilimo wilaya milioni 179, program ya maji (RWSSP) kiasi cha milioni 899.9, mpango wa maendeleo ya Elimu milioni 566.3 na miradi mingineyo.
Madiwani walisema bajeti hiyo imelenga kukamilisha miradi ya barabara, maji, kilimo, mpango wa kuendeleza mfuko wa ngozi, ukarabati wa soko, ujenzi wa jengo jipya la utawala, afya, ikiwa ni pamoja na kuendeleza shughuri za wananchi.
No comments:
Post a Comment