Friday, 4 March 2016

SHEHENA ZA SAMAKI ZAKAMATWA...

Na Esther Macha,Tunduma

SHEHENA za samaki ambao wameingia Nchini kinyemela zimekamatwa katika miji mbalimbali mkoani Mbeya, kupitia Oparesheni maalum inayotekelezwa na Idara za Uvuvi za wilaya kadhaa zilizoko pembezoni mwa mkoa wa Mbeya.

Msimamizi mkuu wa Oparesheni ya kukamata samaki wasiolipiwa kodi,Bakari Lulela alisema kuwa samaki hao wanatokea Nchini China kupitia nchi jirani ya Zambia, ambao bado uhakika wa matumizi yake haujathibitishwa.

Alisema kwamba oparesheni ya msako wa duka hadi duka kuondoa samaki wanaodaiwa kuingia kwa njia za panya na kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya kanda ya nyanda za juu kusini unaendelea.

“Samaki hawa wameingia nchini kupitia mpaka wa Tunduma,kwa kusafirishwa kisiri hadi kwa walaji hali ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya wananchi”alisema Ofisa huyo.

Kwa upande wake Ofisa Mfawidhi wa Idara ya Uvuvi Mpaka wa Tunduma Francis Mpatama alisema maeneo mawili tu mjini Mbeya tayari idadi ya samaki wasiolipiwa kodi wamekamatwa, na kusema kuwa kuna wafanyabiashara wengi wanadaiwa kukwepa kodi.

Alisema wapo kwenye oparesheni hiyo ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote ambao wanajihusisha na ukwepaji wa kodi na kuingiza biashara zao kwa njia ya panya wanakamatwa haraka.

Kwa upande wake Ofisa wa Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) kanda ya Nyanda za juu kusini Rodney Alananga ,alisema samaki hao hawana shida kwa matumizi kwa binadamu .

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...