Monday, 14 March 2016

SHULE YA KIBUGUMO YAPOKEA MSAADA KUTOKA BANGO SANGHO WENYE THAMANI YA MIL. 20



Meza kuu kwenye uzinduzi wa kambi ya upimaji afya kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano iliyofadhiliwa na Umoja wa Watu kutoka Bengali, India wanaoishi Tanzania (Bango Sangho) katika shule ya Msingi Kibugumo iliyopo Kigamboni jana jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Mratibu wa kambi hiyo ya upimaji kutoka Kliniki ya Al Hilal, Dk.Ali Mzige, Mwenyekiti wa Umoja wa Jamii ya watu kutoka India, Bengali waliopo Tanzania (Bango Sangho), Kunal Banerjee, Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Kibugumo, Mzamilo Ally, Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile.(Picha na Zainul Mzige wa Modewjiblog).

Umoja wa Watu kutoka Bengali, India wanaoishi nchini (Bango Sangho) umetoa msaada wa kompyuta, printa, tanki la maji la lita 5000, umeme, madarasa saba yaliyofanyiwa ukarabati, madaftari na kalamu katika Shule ya Msingi Kibugumo iliyopo Kigamboni ulio na thamani ya shilingi Milioni 20 pamoja na huduma ya kupima afya kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano.

Akizungumzia msaada huo, Mwenyekiti wa Bango Sangho, Kunal Banerjee alisema wameamua kutoa msaada huo kwa shule ya Msingi Kibugumo na huduma ya kupima bure kwa kutambua umuhimu wa afya na elimu bora kwa maendeleo ya sasa na baadae kwa taifa.

Alisema wamekuwa wakitoa misaada katika shule hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo na mwaka huu waliamua kuwaletea tena na huduma ya upimaji afya bure kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano ili wazazi wapate fursa ya kutambua hali ya afya za watoto wao lakini pia kuwajengea utaratibu wa kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya ili kujua hali zao za kiafya,

“Sisi tunapenda kuona hali nzuri ya elimu na tumeshasaidia kwa muda shule hii tumeshatoa madawati 100 na tulijenga madarasa mawili na leo tumeleta msaada mwingine na pia awamu hii tena tumeleta huduma ya afya ili watoto wapimwe afya zao,” alisema Banerjee.



Mwenyekiti wa Bango Sangho, Kunal Banerjee akisoma risala ya Umoja huo mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema na Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile.

Nae mgeni rasmi katika halfa hiyo ya kupokea msaada kutoka Bango Sangho, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Bi. Sophia Mjema aliwashukuru Bango Sangho kwa msaada huo ambao wameotoa katika shule hiyo na huduma ya kupima afya kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano na kuwaomba kama ikiwezekana wawapelekee huduma hiyo ya kupima afya kila baada ya miezi mitatu.

Alisema wilaya yake bado ina changamoto nyingi katika sekta ya elimu na kupitia msaada huo utaweza kusaidia kuboresha elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo na kuwaomba kuendelea kuwasaidia.

“Wilaya yetu bado ina changamoto nyingi na kwa msaada huuu naomba niwashukuru sana na ninaomba muendelee kuwa na moyo huo,” alisema Bi. Mjema.

Aidha Bi. Mjema aliwataka wananchi wa wilaya yake ya Temeke kuwa na utaratibu wa kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka ili waweze kutambua magonjwa waliyonayo kabla hayajaanza kuwasumbua na hata wengine kupelekea kupoteza maisha kutokana na kutokuwa na utaratibu wa kupima hadi wanapoanza kusumbuliwa.

Nae Mratibu wa kambi ya upimaji, Dkt. Ali Mzige alisema kupitia huduma hiyo ya upimaji wa afya kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano wanataraji kupima watoto sio chini ya 400 na huduma zitakazotolewa ni kupima uzito, wingi wa damu, ushauri kuhusu lishe, afya ya kinywa na watoto watakaobainuka kuwa na matatizo watapewa rufaa kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke.

Alisema kupitia huduma hiyo wataweza kutambua magonjwa waliyonayo watoto lakini pia kuwapa elimu wazazi jinsi ya kuwalea watoto katika mfumo bora wa kiafya.

“Tunafanya huduma hii kwa watoto sababu asilimia 32 ya watoto nchini walio na umri chini ya miaka mitano wamedumaa na pia tutaweza kuwapa vipeperushi wazazi ili wajue jinsi ya kulea watoto na wanapougua wajue nini cha kufanya,” alisema Dkt. Mzige.

Nae mwalimu wa afya katka shule ya Kibugumo, Tatu Mhina aliwashukuru Bango Sangho kwa misaada ambayo wamekuwa wakiwapatia tangu mwaka 2014 mpaka sasa na kuwaomba kuendelea na moyo huo wa kusaidia elimu katika shule hiyo na kuzidi kuwapelekea huduma za kiafya katika jamii inayozunguka shule hiyo ili wanafunzi waweze kuwa na afya njema.


Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile akisisitiza jambo kwenye uzinduzi huo kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema kutoa nasaha katika ufunguzi wa kambi hiyo.


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema akitoa neno la ufunguzi wa kambi ya upimaji afya kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano iliyofadhiliwa na Umoja wa Watu kutoka Bengali, India wanaoishi Tanzania (Bango Sangho) katika shule ya Msingi Kibugumo iliyopo Kigamboni jana jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema (katikati) akimpima uzito mtoto Shafii Haji (mwaka mmoja na nusu) mkazi wa Kibugumo Darajani, kama ishara ya kuzindua kambi ya huduma za upimaji afya kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano iliyofadhiliwa na Umoja wa Watu kutoka Bengali, India wanaoishi Tanzania (Bango Sangho) katika shule ya Msingi Kibugumo iliyopo Kigamboni jana jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mratibu wa kambi hiyo kutoka Kliniki ya Al Hilal, Dk. Ali Mzige, Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile (wa kwanza kulia) pamoja na Muuguzi wa Zahanati ya Kibugumo, Agnes Mokiwa (wa pili kulia) wakishuhudia tukio hilo.


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema (katikati) akiwa amembeba mtoto Shafii Haji (mwaka mmoja na nusu) mkazi wa Kibugumo Darajani, baada zoezi la kumpima uzito wakati akizindua kambi ya huduma za upimaji afya kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano iliyofadhiliwa na Umoja wa Watu kutoka Bengali, India wanaoishi Tanzania (Bango Sangho) katika shule ya Msingi Kibugumo iliyopo Kigamboni jana jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema akikagua kadi ya kliniki ya maendeleo ya mtoto Shafii Haji (mwaka mmoja na nusu) mkazi wa Kibugumo Darajani (hayupo pichani) mara baada ya kuzindua kambi ya upimaji afya kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano iliyofadhiliwa na Umoja wa Watu kutoka Bengali, India wanaoishi Tanzania (Bango Sangho) katika shule ya Msingi Kibugumo iliyopo Kigamboni jana jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mratibu wa kambi hiyo kutoka Kliniki ya Al Hilal, Dk.Ali Mzige na Kulia ni Muuguzi wa Zahanati ya Kibugumo, Agnes Mokiwa.


Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kibugumo iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam wakigaiwa madaftari yaliyotolewa kama zawadi na Umoja wa Watu kutoka Bengali, India wanaoishi Tanzania (Bango Sangho).


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema akielekea kuzindua moja ya madarasa yaliyokaribatiwa na kuwekewa umeme na Bango Sangho.


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema akikata utepe kuzindua moja kati ya madarasa yaliyokarabatiwa na Bango Sangho huku Mwenyekiti wa Bango Sangho, Kunal Banerjee (kushoto) na Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile wakishuhudia tukio hilo.


Muonekano wa vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Kibugumo baada ya kupakwa rangi na kuwekwa umeme na Umoja wa Watu kutoka Bengali, India wanaoishi Tanzania (Bango Sangho).


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema akikagua moja ya darasa lililokarabatiwa na Bango Sangho. 


No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...