Sunday, 12 June 2016

MKOA WA IRINGA UNA WATUMISHI HEWA 169

Mkoa wa Iringa iliunda timu ya wataalam kwa ajili ya kupita katika Hospitali Teule zote za Wilaya na kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kuendelea kubaini iwapo wapo watumishi hewa ambao hawakubainishwa katika zoezi la awali. 

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema kuwa timu niliyounda imekamilisha kazi yake tarehe 07/06/2016 na kunikabidhi taarifa yake. Kwa ufupi taarifa hiyo imebainisha masuala mbalimbali.

Akiongea na waandishi wa habari jana alisema kuna watumishi hewa 169 katika Halmashauri ambao wamekuwa wakipokea mishahara pasipo kustahili kutokana na utoro, kustaafu na kufariki. 

Aidha, alisema kuwa upotevu wa fedha kutokana na ulipaji wa mishahara isivyostahili umeisababishia Serikali hasara ya shilingi Milioni 364,028,910.80. 

Timu hiyo pia imebaini kuwa, katika Hospitali Teule ya Ilula inayotoa huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo lipo tatizo la fedha za mishahara isiyolipwa inayofikia kiasi cha Shilingi Milioni 151,583,969.00 kutorejeshwa Hazina tangu Januari, 2008 hadi Februari, 2016. 

Fedha hiyo imetumika kwa shughuli za uendeshaji wa Hosipitali Teule ya Wilaya ya Ilula pasipo idhini ya Serikali. Fedha hiyo ilitumika kugharamia huduma za umeme, ununuzi wa dawa na kulipa mishahara ya watumishi ambao orodha yake haikuwa inafahamika na Serikali kunyume na taratibu. 

Mkoa unaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa katika taarifa ya Tume na ninaahidi kuendelea kutoa taarifa ya utekelezaji baada ya kuyafanyia kazi.

UTEKELEZAJI WA UPATIKANAJI WA MADAWATI

Mkoa una jumla ya shule za Msingi 478 na shule za Sekondari 107 zinazo milikiwa na Serikali. 

Awali Mkoa ulikuwa na upungufu wa Madawati 29,347, ikiwa Madawati 26,046 ni upungufu katika shule za Msingi, na Madawti 3,301 ni upungufu katika shule za Sekondari.

Hadi kufikia tarehe 06/06/2016, Halmashauri zimetengeneza jumla ya Madawati 17,225 kwa ajiri ya shule za Msingi na Sekondari. Hivyo kubaki na upungufu wa Madawati 4,681.

Hadi kufikia tarehe 6/6/2016 Mkoa umetengeneza jumla ya Madawati 442 na bado jitihada zinafanyika kwa ajili ya kuongeza zaidi idadi hiyo. 

HALI YA UPATIKANAJI WA SUKARI KATIKA MKOA WA IRINGA

Mkoa wa Iringa hauna kiwanda cha uzalishaji wa sukari. Kutokana na kukosekana kwa uzalishaji wa sukari kwa Mkoa wetu tunategemea sukari inayozalishwa kutoka mikoa mingine. Sukari hiyo huletwa Mkoani hapa na Mawakala walioteuliwa na Bodi ya sukari. Mahitaji ya sukari kwa Mkoa wa Iringa kwa mwaka ni tani 14,000, kati ya tani hizo, Walaji wa kawaida hutumia tani 9,000 na matumizi ya viwanda ni tani 5,000.

Hali ya upatikanaji wa sukari

Changamoto ya upungufu wa sukari hapa Mkoani imeanza mwezi Machi, 2016 hadi sasa. Kabla ya huu mwezi changamoto haikuwepo na sukari ilikuwa inauzwa kwa bei ya jumla Tsh.88,000 kwa kg. 50 na bei ya reja reja ilikuwa inauzwa Tsh.1,800-2,000 kwa Manispaa ya Iringa na Tsh.2,000-2,200 kwa Halmashauri za Wilaya hususan maeneo ya Vijijini. 

Kwa sasa inauzwa kwa bei ya jumla Tsh.110,000 kwa kg. 50 na bei ya rejareja inauzwa kati ya Tsh. 2,800 na Tshs. 3,000 kwa Manispaa ya Iringa, na Tsh.3,000-3,400 kwa Halmashauri za Wilaya na maeneo ya Vijijini. 

Hatua zilizochukuliwa kukabiliana na upungufu wa Sukari Kuhamasisha Mawakala wa sukari kuleta sukari nyingi.

Kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini wanaouza bei ya juu na kuchukua hatua stahiki.

"Nichukue nafasi hii kuwatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Iringa na hasa waumini wa dini ya Kiislamu ambao wameanza mfungo mtukufu wa Ramadhani kuwa, katika kipindi chote cha Mfungo Mtukufu na baada ya mfungo kuwa sukari itaendelea kupatikana," alisema Masenza. 

Mawakala wataendelea kuleta Sukari ya kutosha kukidhi mahitaji ya wananchi.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...