Na Dotto Mwaibale
UONGOZI wa Shule za Feza nchini umeibuka na kukanusha taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii, kuwa wao hawana uhusiano na Fethullah Gulen wala serikali ya Uturuki kwa vile hawajawahi kupokea misaada toka pande hizo mbili za uendeshaji na kuwa shule hizo hazitafungwa.
Kauli hiyo imetolewa baada ya hivi karibuni kuenea kwa uvumi kuwa shule za Feza zipo hatarini kufungwa kwa madai kuwa mmiliki wake ni yule aliyejihusisha na jaribio la kuipindua serikani nchini Uturuki.
Mwenyekiti wa Bodi wa Shule hizo, Habibu Miradji aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanahabari Kawe jijini Dar es Salaam leo asubuhi.
Alisema Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa Shule za Feza ni kama asasi zingine zilizosajiliwa kishera na serikali, hivyo ni mali ya watanzania.
“Shule za Feza zitabaki kuwa kiwanda cha kuzalisha wazalendo wa kitanzania na raia bora wa duniani, hivyo wazazi wanapaswa kuondoa hofu,” alisema.
Alisema toka mwaka 1995 shule hiyo imepata mafanikio ya kujenga shule za awali tatu, shule za msingi mbili, sekondari tatu na shule ya kimataifa moja.
Aliongeza kuwa huo ni uwekezaji wenye mchango katika kukuza pato la taifa, kutoka awamu ya pili, tatu, nne hadi awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli.
\Alisema shule ya Feza ni hazina kwa Tanzania kwani shule zake zimekuwa zikishika nafasi ya 10 bora toka mwaka 2004 hadi leo.
Alisema wanatoa wito kwa wazazi kuwasiliana na uongozi wa shule hiyo kujua kinachoendelea kwenye shule husika kwa manufaa ya wanafunzi wetu na taifa bila kusikiliza uvumi huo unaoenezwa na watu wasiopenda maendeleo ya shule hizo.
No comments:
Post a Comment