Sunday, 27 November 2016

Padri Fred Njuguna: Elimu Ya Ufundi Stadi Inaweza Kutatua Tatizo La Ajira Nchini




Mmliki wa SIMBAYA BLOG Friday Simbaya (kulia) akimpongeza mmoja wa wahitimu Pelegrin Kilwa katika Mahafali ya 25 ya Chuo cha Wasalesiani wa Don Bosco mkoani Iringa hivi karibuni. 












VIJANA wameshauriwa kujiajiri kupitia elimu ya ufundi stadi ili kusaidia serikali kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Don Bosco (DYTC) cha mkoani Iringa, Padri Fred Njuguna wakati wa Mahafali ya 25 ya chuo hicho jana.

Chuo hicho kipo chini ya shirika la Waslesiani wa Don Bosco, ambalo ni shirika la kimataifa la kidini linalofanya kazi katika nchi 125 duniani kote kwa sababu ya vijana.

Padri Njuguna alitoa rai hiyo kwa vijana nchini wanaomaliza kidato cha nne na cha sita kwamba wanatakiwa kujiunga na vyuo hivyo vya elimu ya ufundi stadi baada ya kukosa kujiunga katika vyuo vya kawaida kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema wapo wanafunzi wanaomaliza elimu hiyo ya sekondari ambao wanabweteka na kujikuta wanakaa bila kazi yakufanya, kumbe wangejiunga na vyuo hivyo vya ufundi stadi wangepunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.

Alisema kuwa ili kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano ya sera ya viwanda, wahitimu hao wa elimu ya sekondari hawanabudi kujiunga na vyuo hivyo vya ufundi stadi.

Aidha, mkuu wa chuo hicho ameipongeza serikali kwa kuboresha mifumo ya utoaji mafunzo katika vyuo vya ufundi stadi nchini kunakopelekea wahitimu wengi katika vyuo hivyo kuajirika au kujiajiri wenyewe.

Alisema kuwa baada ya mamlaka ya vyuo vya elimu ya ufundi stadi nchini (VETA) kuboresha shughuli za mafunzo wahitimu wengi wamekuwa wakijiajiri wenyewe.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Vijana cha Don Bosco Pd. Njuguna alisema kuwa chuo hicho kinakabiliwa na chamgamoto nyingi ikiwemo ya kukosekana kwa hosteli za wanafunzi ambapo wengi wao huishi mitaani na kusababisha utoaji wa malezi kwa vijana hao kuwa ngumu.

“Tunaweza kutoa malezi bora kwa vijana wanapokuwa shuleni lakini pindi wanaporudi nyumbani anaendelea na tabia zao zilezile, kumbe wangekuwa wanakaa hosteli inakuwa rahisi kutoa malezi kwa vijana…,” alisema Pd. Fred Njuguna.

Alisema kuwa changamoto nyingine ni kwamba chuo hicho kinatumia gharama kubwa ya kuendeshaji kwa kukosekana kwa ruzuku kutoka serikalini pamoja na wanafunzi wengi kushindwa kulipa ada kwa wakati.

Alisema kuwa kwa kawaida serikali inatakiwa kuchangia asilimia 70 ya uendeshaji wa vyuo vya ufundi stadi na asiliamia 30 inayobaki inachangiwa na chuo husika, “…lakini fedha hizo haziji mara nyingi,” aliongeza Pd. Njuguna.

Alisema pia kuwa changamoto nyingine ni kwamba kumekuwepo na idadi ndogo ya wanafunzi wa kike wanaoujiunga na chuo ukilinganisha na idadi yawavulana kutokana ukosefu wa hosteli.

Alitoa mfano kwa wahitimu wa mwaka huu, kwamba jumla ya wanafunzi 63 waliohitimu mwaka huu lakini ni wasichana nane tu ndio waliohitimu kutokana sababu mbalimbali ikiwemo mimba mbili za wanafunzi wa kike kwa kukosekana kwa mabweni ya shule.

Alisema kuwa chuo hicho kina zaidi ya wanafunzi 200, kati yao wasichana ni 47 kati ya wanafunzi wote wa chuo kutokana kutokuwa na mabweni.

Kituo cha mafunzo ya vijana cha Don Bosco kipo chini ya Wasalesiani wa Don Bosco ambalo ni shirika la kimataifa la kidini linalofanya kazi katika nchi 125 duniani kote kwa sababu ya vijana. 

Medrick msamila ni mhitimu katika mahafali ya 25 ya chuo hicho katika fani ya uashi amemshukuru mungu kwa kumaliza salama lakini akaweka msisitizo kuwa chuo hicho kione haja ya kupunguza ada ili wanafunzi wengi wajiunge na chuo.

Alisema kuwa wanafunzi wengi wanatoka kwenye familia zenye kipato kidogo lakini wanashindwa kujiunga kutokana na ada kubwa na kuongeza kuwa wasichana wengi wajiunge na vyuo vya ufundi stadi kwani ufundi sio tu kwa wanaume.

Wasalesiani wa don bosco waliwasili mkoani Iringa mwaka 1980 na walianzisha kituo cha vijana na shule ya kiufundi. 

Chuo hicho cha ufundi kinatoa jumla ya kozi za aina saba na kinasimamiwa na mamlaka ya elimu ya ufundi stadi nchini (VETA), ambapo asilimia 88 ya wahitimu wake wanajiajiri au kuajiriwa. 

Kozi zifuatazo zinatolewa katika Chuo cha Don Bosco Iringa ni pamoja na kozi ya kompyuta, uchapishaji, uchomeleaji, ushonaji, ufundi magari, umeme, na uashi.

Hata hivyo, mkuu wa chuo huyo amewashauri wahitimu kutoridhika na elimu walioipata na badala yake wajiendeleze mpaka wafike ngazi ya juu zaidi ili kuweza kuleta ubora na ufanisi katika kazi zao.


No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...