Saturday, 19 November 2016

TAGRODE: MIGOGORO YA ARDHI KILOLO INATOKANA UGOMVI WA MIPAKA












Mkazi wa Kijiji cha Mawambala wilayani Kilolo, mkoani Iringa, Mzee Dominikus Mgogosi akitoa maoni wakati wa mdahalo wa nini kifanyke kumalizi migogoro ya ardhi ulioandaliwa shirika la TAGRODE chini ya mwavuli wa mashirika (PELUM Tanzania) kupitia ufadhili wa watu wa Marekani jana. (Picha: Friday Simbaya)




Na Friday Simbaya, Kilolo



MRATIBU wa shirika lisilo la kiserikali la TAGRODE yenye makao yake makuu mjini Iringa, Dickson Mwalubandu amesema migogoro yote ya ardhi wilayani Kilolo mkoani Iringa inatokana na ugomvi wa mipaka katika maeneo ya vijijini.



Alisema alishauri kuwa ni lazima mipaka ya vijiji ihakikiwe upya ili kupunguza migogoro ya ardhi na mipaka inayovikumba baadhi ya vijiji wilayani Kilolo.



Mwalubandu alisema hayo jana (Ijumaa) wakati akiwasilisha mada katika mdahalo uliofanyika katika kijiji cha Mawambala wilayani humo ukilenga kutafuta mambo yakufanya ili kupunguza malalamiko ya migogoro ya ardhi. 



“Katika kuhakikisha wananchi wanakabiliana na changamoto hiyo shirika lake linaendesha midahalo na kuimarisha kamati za ardhi za vijiji na mabaraza ya ardhi ya vijiji ili yaweze kutatua migogoro pindi inapojitokeza kwenye maeneo yao,” alisema mratibu huyo.



Alisema midahalo hiyo inalenga kuwaongezea wananchi wa wilaya hiyo, hasa vijiji vya mradi uelewa juu ya sheria za ardhi, haki za ardhi kwa wanawake na makundi maalum pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi.



Alisema kuwa kwa ufadhili wa shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID), kupitia mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yanayofanya kazi na wakulima na wafugaji wadogo nchini Tanzania (PELUM Tanzania) shirika hilo linaendesha midahalo hiyo katika vijiji vya Ikuka,



Mbigili, Mawala, Mawambala na Masalali kwa wilaya ya kilolo na vijiji vya Usokami, Ugesa, Makungu, Magunguli na Isaula wilaya ya Mufindi kupitia mradi wake wa CEGO unaohusisha jamii ya vijijini katika uwajibikaji wa masuala ya ardhi ya kijiji.



akichangia mada, mkazi wa Kijiji cha mawambala alisema migogoro ya ardhi katika maeneo yao itakoma kama serikali itatakiwa kuhakiki mipaka ya vijiji,hatua ambayo pia itaimarisha amani na utulivu na kuifanya sekta hiyo kuwa na tija kwa jamii.



Kwa upande wake, Mzee Dominikus Mgogosi alisema serikali za vijiji ni chanzo cha migogoro kwa sababu zina baadhi ya viongozi wanaoshindwa kusimamia sheria hizo baada ya maamuzi kufanywa.



Kwa upande wake Expedito Lusoko ambaye ni mwenyekiti wa Kijiji cha Mawambala aliomba serikali kwa kutumia sheria hizo kutenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji hatua itakayosaidia kuepukana na migogoro kwa kuwa makundi yote mawili yanategemeana.



Ushiriki wa Wananchi katika kusimamaia sekta ya Kilimo yaani Citizens Engaging in Government Oversight in Agriculture (CEGO-Agriculture) ni mradi wa miaka minne unaofadhiliwa na USAID na kutekelezwa na PELUM Tanzania. 



Mradi una lengo la kuongeza maarifa, kujenga ushahidi, na kuongeza uelewa wenye nia ya kuimarisha haki za ardhi kwa wakulima wadogo kwa maendeleo ya kiuchumi, maisha bora, na kilimo endelevu ili kuboresha utawala bora na uwajibikaji. Mradi unatekelezwa katika mikoa ya Morogoro, Iringa, na Dodoma.



PELUM Tanzania inatekeleza mradi wa kuhusisha jamii ya vijijini katika uwajibikaji wa masuala ya ardhi ya kijiji. Mradi huo unajulikana kwa jina la CEGO na unatekelezwa kwa ufadhili kutoka kwa watu wa Marekani.











No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...