Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela amesikitishwa na vitendo vilivyokithiri vya wanawake kutupa watoto mara baada ya kujifungua ambapo amewashauri kutumia njia za kisheria kupata haki ya matunzo ya mtoto, kwa wanaume wanaowapa mimba.
Mkuu huyo alisema hayo jana wakati akishiriki chakula pamoja na watoto yatima wanaolelewa na kituo cha daily bread life children’s home kilichopo neo la Mkinbizi Bima, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, mkoani Iringa.
Kutokana na hilo amewaagiza watendaji wa vijiji, mtaa na kata kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo katika maeneo yao kuwachukulia hatua wanawake wanaotupa watoto, kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Kasesela ambaye alikuwa mgeni rasmi alitumia pia fursa ya kuwatakia wananchi wa Wilaya ya Iringa na Mkoa wa Iringa heri katika Noeli na Mwaka Mpya 2017.
Alisema kuwa, Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa iliyokithiri kwa vitendo vingi vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, hivyo ameitaka jamii kuunganisha nguvu ili kupunguza vitendo hivyo ambavyo pia ni kinyume na maagizo ya mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ‘Daily Bread Life Tanzania’, Askofu Mpeli Mwaisumbe amewashukuru wadau mbalimbali kwa kuunga mkono huduma ya watoto pamoja na wadau kutoka nje ya Tanzania kwa uaminifu wao kutoa michango yao ili huduma ienedelee na kufika hadi leo.
Askofu Mwaisumbe alisema kuwa huduma hiyo inawasaidia watoto 244 kati yao wakiume ni 126 na wa kike ni 118 nje ya makao ya watoto, watoto hao husaidiwa vifaa vya shule na wengine huchangiwa hela ya chakula familia wanazoishi au wanazolelewa.
Alisema kuwa huduma ya “Daily Bread Life Ministries Tanzania” waliaandaa sherehe za Krismasi na chakula ili waweze kushiriki chakula cha pamoja na watoto yatima.
No comments:
Post a Comment