Sunday, 4 December 2016

…KUVUNJIKA KWA KOLEO SIO MWISHO WA UHUNZI












WANANCHI na wadau mbalimbali wa mazingira wameshauriwa kutunza mazingira hata baada ya wafadhili kumaliza mradi wao kwani kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi.

Kauli hiyo imetolewa na maofisa maendeleo jamii wa shirika la kuhifadhi la mazingira duniani (WWF-Tanzania), Martha Sanga na Evergris Makfura wakati wakifunga warsha ya wadau ya usimamizi wa rasilimali za maji na mazingira  mjiini Makambako, mkoani Njombe.

Walisema katika nyakati tofauti kuwa wananchi na wadau mbalimbali wa mazingira wanabudi kuendelea hata baada ya programu ya maji Ruaha kumaliza muda wake, kwani utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mtu.

Walisema kuwa suala la usimamizi wa rasilimali za maji na mazingira sio la wafadhili, bali ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha mazingira yanatunzwa.

Shirika la WWF kwa kupitia Programu yake ya Maji Ruaha (RWP) kwa kushirikiana na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB), halmashauri, wananchi na wadau mbalimbali wa mazingira walitekeleza mradi wa miaka mitano wa katika usimamizi wa rasilimali za maji na mazingira ambao ulikuwa na lengo la rudisha hali ya Mto Ruaha Mkuu ili uweze kutiririsha maji kwa mwaka mzima. 

Martha na Makfura walisema kuwa bado mapambano ya  utunzaji wa rasilimali za maji na mazingira  yanaendelea hata bila kuwepo wafadhili .

Warsha hiyo ililenga kutathmini shughuli zilizotekelezwa na wadau mbalimbali wa mazingira kwa kipindi cha miaka mitano cha utekelezaji ulioratibiwa na shirika la WWF kupitia Programu yake ya Maji Ruaha kwa kushirikiana na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB).

Maafisa maenedeleo ya jamii kutoka Shirika la WWF Tanzania kupitia Programu yake ya Maji Ruaha wamewataka wadau kuendelea kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji kwa kutumia dhana ya ushirikishwaji.

Maafisa hao wa jamii walisema kuwa Serikali ilishaweka sawa mahitaji ya kisheria (legal framework) kama vile kupitishwa kwa Sheria Mama ya Mazingira (2004), kutolewa kwa Sera ya Maji (Julai 2002) na Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Namba 11 ya mwaka 2009.

Naye Roy Kadege ambaye pia ni Mhasibu wa Jumuiya ya Watumiaji Maji (WUA) katika Bonde dogo la Mto Mpando wilayani Wanging’ombe, mkoani Njombe, alisema kuwa jumuiya hiyo atahakikisha inasimamia kikamilifu suala zima la usimamizi wa rasilimali za maji na mazingira.

Alisema kuwa pamoja kuwa mradi kumaliza muda wake, wataendelea kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa vile vyanzo vingi vya maji vipo katika ukanda wao na ambako vyanzo vya mito vinakoanzia.

Alisema kuwa kupitia programu ya Maji Ruaha, jumuiya hiyo ya watumiaji wa maji imeweza kutoa elimu ya usimamizi wa rasilimali za maji na mazingira katika vijiji 20 vinavyozunguka bonde dogo la Mto Mpando.

Alisema kuwa baada ya kuwepo mradi huo wameweza kutunza vyanzo vya maji na kulikopelekea kurudisha Mto Mbarali mkoani Mbeya. 

Mto huo ulikauka kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi zisizo endelevu lakini na kwa uwepo wa mradi huo wameweza kutunza mazingira.

Naye Adamson Msigala ambaye pia ni Mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji (WUA) katika bonde la mto Mpando alisema kuwa ili zoezi la usimamizi wa rasilimali za maji na mazingira ziweze kuwa endelevu halmashauri hazinabudi kutenga fedha kwenye bajeti zao kwa ajili ya shughuli za utunzaji mazingira kuliko kutegemea wafadhili.

“Kwa mfano, wadau wetu wa maendeleo wanamaliza mradi wao haina maana kwamba shughuli za usimamizi wa rasilimali za maji na mazingira zatasimama rahasha, sasa ni jukumu letu wananchi kwa shirikiana na halmashauri zetu kuweka mikakati yakuweza kuendelea pale wadau wetu walipoishia,” alisema Msigala.

Alisema kuwa kigezo cha umaskini kisiwe chanzo cha kuharibu mazingira ni lazima watu wafanya kazi kutunza mazingira bila kusukumwa bali kwa moyo.

Aliongeza kuwa wakati WWF wanaleta mradi huo kwa mara ya kwanza, wananchi walikuwa wagumu kuuelewa kwa vile walikuwa wamezoea kulima kwenye vinyungu ambavyo ni vyanzo vya maji.

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe Michael Haule ambaye pia ni timu ya wawezeshaji ya wilaya (DFT) alilipongeza shirika la WWF kupitia programu ya maji Ruaha pamoja na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB) kwa kuwaunganisha wadau mbalimbali wa mazingira ili kuweza kupanga mipango yao kwa pamoja. 

Alipendekeza pia kuwa kwa siku za usoni kunapokuwa na warsha kama hizo washirikishe na vyombo vya usalama na mahakama ili waweze kutambua jumuiya za watumia maji kuwa zipo kisheria.

Alisema kuwa bila kushirikisha vyombo hivyo usimamizi wa rasilimali za maji na mazingira utakuwa mgumu kwa vile kutakuwa na na mwingiliano wa shughuli baina ya vyombo hivyo na jumuiya za watumia maji.

Alisema kuwa kuna wakati fulani jumuiya za watumia maji zilikuwa zikiwakamata waharifu wa uharibifu wa vyanzo vya maji na wakipelekwa polisi wanatolewa.

Kumbe kungekuwa na ushirikishaji wa vyombo hivyo na vikatambua kuwa jumuiya za watumia maji zipo kisheria wangeweza kwenda pamoja.

Aliongeza kuwa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji wanapoitisha mikutano yao wahakikishe wanawaalika taasisi ya kupambana na rushwa (TAKUKURU), polisi na mahakama ili waweze kuvitambua vyombo hivyo vya watumia maji ili kusimamia kikamilifu suala zima la rasilimali za maji na mazingira.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...