KUJA kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia hususani mtandao wa intaneti kumebadilisha kwa kiasi kikubwa mienendo ya matangazo ya utoaji wa huduma mbalimbali duniani na hii ni kutokana na uwezo wake wa kuwaruhusu wateja kutoa ushuhuda, kukosoa au kutoa maoni juu ya walichohudumiwa na kujionea.
Tofauti na kipindi cha nyuma kidogo ambapo wataalamu wa masoko walikuwa wanatumia zaidi njia za luninga na redio kuwafikia wateja wao, siku hizi mfumo wa intaneti unapewa kipaumbele zaidi kutokana na namna unavyofikia watu wengi zaidi ndani ya muda mfupi, kwa haraka na gharama kidogo.
Matangazo ya luninga na redio yanaweza kuwa hayana ushawishi mkubwa ukilinganisha na mtandao wa intaneti kwani hivi sasa makampuni yanaweza kuwasilisha bidhaa na huduma zao na kupokea majibu kujua kwamba zinakubalika au la. Hali hiyo ni dhahiri kutokana na makampuni mengi kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika teknolojia na rasilimali watu katika kusimamia tovuti na kurasa zao rasmi za mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter, instagram na mingineyo.
Kupitia tovuti na kurasa hizo za mitandao ya kijamii biashara na huduma nyingi zinafanya vizuri kutokana na ushawishi wao kwenye mitandao kutokana na namna ambavyo zinazungumziwa vizuri na watu wengi. Lakini pia husaidia kampuni hizo husika kuwasiliana moja kwa moja na wateja wao kwa sababu wateja huwasilisha maoni yao moja kwa moja mtandaoni tofauti na luninga au redio ambazo hutoa fursa ya kuona au kusikiliza tu matangazo.
Vivyo hivyo hali hii inaweza kusaidia sana ukuaji wa sekta ya utalii na ukarimu kama vile huduma za hoteli na malazi ambazo hujitangaza zaidi kupitia namna wateja wanavyozizungumzia.
Jumia Travel (www.travel.jumia.com) kampuni unaongoza kwa huduma za hoteli mtandaoni barani Afrika umezitunuku vyeti hoteli kadhaa ambazo zilizopendekezwa na kutembelewa ndani ya wateja wengi kipindi cha mwaka mzima wa 2016.
Akizungumzia juu ya umuhimu wa vyeti hivyo Meneja Mkazi wa Jumia Travel Tanzania, Bi. Fatema Dharsee amesema kuwa, “Vyeti hivi vina umuhimu mkubwa kwani ni viashiria vikubwa vya namna hoteli yako inatathminiwa vipi na wateja pindi wanapoitembelea. Siku zote wateja huambizana huduma wanazozipata sehemu za biashara wanazotembelea na kutokana na ushuhuda huo ndio na wengine hushawishika kutembelea pia. Kupitia mtandao wetu wateja wanayofursa ya kutoa maoni juu ya hoteli walizozitembelea, huduma walizopatiwa, mapungufu waliyoyaona na maboresho ambayo wangependa yafanyiwe kazi.”
“Imefikia mahala sasa ni lazima wataalamu wa masoko watambue mchango na ushawishi walionao wateja kwenye kukua kwa biashara zao kwani nguvu yao ni kubwa zaidi ya matangazo wanayoyalipia kupitia luninga na redio au njia nyinginezo. Maneno au ushuhuda unaotolewa na wateja unatosha kwa kiasi kikubwa mtu kutumia bidhaa au huduma yako kwani ni halisi kutokana na mtu kuitumia au kupatiwa huduma hiyo husika. Hivyo ningependa kutumia fursa hii kuwataka mameneja wa hoteli waliokabidhiwa vyeti hivi kuichukulia hali hii kama ni changamoto kwao kwa kufuatilia maoni ya wateja yanayoachwa kwa njia ya mtandao na kuyafanyia kazi.” Alihitimisha Bi. Dharsee.
Hoteli ambazo zimepatiwa vyeti hivyo ni pamoja na Jafferji House & Spa Hotel na Garden Lodge za visiwani Zanzibar, Golden Tulip Hotel, Peacock Hotel na Butterfly Hotel zote za jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment