KATIBU Tawala wa Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu amesema katika maadhimisho ya Siku ya wanawake watazindua Jukwaa la uwezeshaji wanawake Kiuchumi Kimkoa ambapo washiriki ni wawakilishi wa Vikundi vya Wanawake kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa.
Alisema kuwa wanawake na jamii kwa ujumla wajitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya wanawake ili kujumuika na wanawake wengine kubadilishana mawazo na kupeana uzoefu wa masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Aidha, Wamoja anaomba wadau mbalimbali kujitokeza kutoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu ya ujasiliamali na kuelezea fursa zilizopo kwa wanawake kama Mchango wao katika maadhimisho haya.
Alisema kuwa lengo la Jukwaa ni kuwaweka Wanawake pamoja ili waweze kutambua na kujadili fursa zilizopo katika maeneo yao na kuweka mikakati ya namna ya kuzitumia kwa maendeleo.
“Huu ni utekelezaji wa Maelekezo ya Serikali kupitia baraza la uwezeshaji Wanawake Kiuchumi. Baada ya uzinduzi huo kwa ngazi ya Mkoa, utafanyika pia uzinduzi katika kila Halmashauri,” alisema Wamoja.
Tarehe 8 Machi, kila mwaka siku ya wanawake Duniani huadhimishwa ikiwa ni muitikio wa Azimio la Umoja wa Mataifa.
Tanzania ikiwa ni Mwanachama wa Umoja wa Mataifa inaungana na Mataifa mengine kuadhimisha siku hiyo.
Lengo la kufanya maadhimisho hayo ni kutambua na kuheshimu mchango wa Wanawake katika maendeleo ya Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii na kutoa fursa kwa Wanawake kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo yao.
Maadhimisho ya mwaka huu 2017, yataongozwa na kaulimbiu isemayo; TANZANIA YA VIWANDA, WANAWAKE NI MSINGI WA MABADILIKO YA KIUCHUMI.
Kauli mbiu hii inakwenda sambamba na mipango na Sera za nchi zinazolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Vilevile, anapenda kuikumbusha jamii kwamba wanawake wana mchango mkubwa katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda, hivyo kuna haja ya kuwapa nafasi ya kutosha katika kushiriki katika kuendeleza viwanda.
“Sote tutambue kwamba viwanda vinaharakisha maendeleo na mabadiliko ya kiuchumi katika jamii. Na umuhimu wake mkubwa unaonekana katika kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa na wananchi,” alisema.
Alisema kuwa kwa wanawake ndiyo kundi kubwa linalojishughulisha na kilimo uwepo wa viwanda ni muhimu sana kwa kuwa utawasaidia katika kuongeza thamani mazao mbalimbali wanayozalisha.
Viwanda vilevile, vitawawezesha kupata nyenzo za kurahisisha kupunguza mzigo wa kazi unaowaelemea wanawake.
Kutokana na mnyororo huu, uwepo wa viwanda utawawezesha wanawake kutoa mchango wao zaidi katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi wao wenyewe, familia zao na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Wakati huohuo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Wamoja Ayubu alitumie fursa kutoa wito kwa Wanawake katika Utumishi wa Umma kutumia fursa mbalimbali zilizopo kujiendeleza kielimu ili kujiongezea uelewa zaidi.
Fursa zipo nyingi kupitia Nchi mbalimbali ambazo zinatoa ufadhili wa masomo ya Uzamili na kutumia elimu hiyo kusaidia Wanawake wengine kwenye maeneo yao ya kazi kupitia huduma wanazozitoa, lakini pia kusaidia kujenga uwezo wa Wanawake wengine walio nje ya Utumishi wa Umma ambao ni kundi kubwa sana na wengi wao wakijishughulisha na shughuli mbalimbali za kukuza kipato na kujiletea maendeleo yao.
No comments:
Post a Comment