Kaimu Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Iringa, Lucas Gama akiongea na Nipashe jana. (Picha na Friday Simbaya) |
Wajasiriamali washauliwa kuunda vikundi ili waweze kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na hatimae waweze kurahisisha upatikanaji wa matibabu pindi wanapoenda hospitali kutibiwa.
Akizungumza na Nipashe jana Kaimu Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Iringa, Lucas Gama alisema kuwa watu wasio watumishi wa serikali wanaruhusiwa kujiunga na mfuko wa bima ya afya kupitia vikundi vya ujasiriamali.
Alisema kuwa wajasiriamali toka vikundi mbalimbali mkoani Iringa wamehamasishwa kujiunga na mfuko wa NHIF, ili kurahisisha matibabu wawapo katika shughuli zao za kawaida, na kuongeza kuwa wajasiriamali watakaojiunga na mfuko huo na kuwa wanachama watalipia shilingi 76,800/- kila mmoja.
Gama alisema kuwa mfuko wa NHIF ni mfuko wa kijamii unayotumia dhana ya ‘mshikamano wa kijamii’ kwa maana ya kuwa wanachama wote ni sawa mbele ya jamii, yaani, mchangiaji mdogo na anayechangia hela kubwa wote ni sawa.
Alisema kuwa majukumu ya NHIF ni pamoja na kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya zinajitosheleza kwa kuwa na mahitaji yote muhimu kwa kutoa huduma bora kwa wanachama wake.
“Kwa kweli ugonjwa hauna siku wala hodi ni vizuri mtu ukajiandaa kwa maisha ya baadaye kwa kujiunga na mfuko wa bima ya afya…,” alisema Gama.
Alisema kuwa mfuko wa bima ya afya umejipanga kuhakikisha mwanachama anapata matibabu stahiki kwa kutumia kadi zao za bima kwa kuwa gharama zote za matibabu zimelipiwa na mfuko.
Akizungumzia uhaba wa dawa katika vituo vya afya na hospitali ambazo zimeteuliwa kutoa matibabu kwa kupitia mfuko huo, alisema kuwa, tatizo la ukosefu wa dawa hospitalini litamalizika, endapo kaya nyingi zitajiunga na mfuko wa NHIF, kwani serikali nayo itaweka mkono wake ili kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa.
‘’Tunahamasisha na kutoa Elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kujiunga na mfuko wa bima ya Afya makanisani, misikitini, kwa waendesha pikipiki (bodaboda), kwa viongozi wa dini na jamii kwa ujumla’’alisema Gama.
MWISHO
No comments:
Post a Comment