Mmoja wa wananchi wa Kata ya Nduli katika Manispaa ya Iringa, mkoani Iringa akijaribu kuvuta maji kutoka kwenye kisima cha maji. Kisima hicho ni mojawapo ya visima vinne vilivyotolewa msaada na taasisi ya Dhi Nureyn Islamic Foundation Iringa - Tanzania kwa kata hiyo hivi karibuni. (Picha Na Friday Simbaya)
Na Friday Simbaya, Iringa
Wananchi wa mitaa ya Kipululu na Igungandembwe, Kata ya Nduli katika Manispaa ya Iringa, mkoani Iringa wameipongeza taasisi ya Dhi Nureyn Islamic Foundation Iringa - Tanzania kwa msaada wa visima vinne vya maji safi na salama hivi karibuni.
Wananchi hao kupitia Diwani wa Kata hiyo, Bashiri Mtove waliishukuru taasisi hiyo kwa kuwasaidia kupata visima vinne vya maji safi na salama na kuongeza kuwa miaka kwa zaidi ya 50 hawajawahi kupata maji safi na salama, ambapo hapo awali walikuwa wanatumia maji yasio safi na salama kutoka kwenye vikorongo vya maji.
Walisema kuwa kwa miaka mingi wamekuwa wakitumia maji yasio safi na salama kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu ya maji ya bomba, lakini kupitia visima hivyo vya maji maisha yao yataboreka.
Maneno Mtove ni mkazi wa Mtaa wa Igungandembwe katika Kijiji cha Kigonzile alisema kuwa kwa miaka 50 hawajawahi kupata maji safi na salama isipokuwa walikuwa wanatumia maji ya korongoni ambayo si salama kwa afya.
“Tunashukuru sana taasisi ya Dhi Nureyn Islamic Foundation kwa kutusaidia kupata visima vya maji ambavyo vitasaidia kupunguza magonjwa ya homa za matumbo na pia wamejali afya zetu…” alisema Maneno Mtove.
Kata ya Nduli ni mmoja ya kata zilizopo pembezoni mwa Manispaa ya Iringa, mkoani Iringa ambazo hazina miundombinu za maji ya bomba ambapo wananchi wengi hutumia maji ya visima vifupi na kupelekea kuhatarisha maisha yao.
Kwa upande wake, msimamizi wa miradi ya Taasisi ya Dhi Nureyn Islamic Foundation Iringa-Tanzania, Faiz Said Abri alisema jana kuwa taasisi yake kwa kushirikiana na taasisi ile ya Al Muntada Aid ya Uingereza wameweza kuchimba visima vinne vyenye thamani ya shilingi 10,400,000/-, ambapo kisima kimoja kiligaharimu shilingi 2.6m/-.
Alisema kuwa taasisi yake kwa kushirikiana na Al Muntada Aid wameweza kuwachimbia visima vinne vya maji safi na salama wananchi wa mitaa ya Kipululu na Igungandembwe katika Kata ya Nduli, Manispaa ya Iringa, mkoani Iringa.
Manispaa ya Iringa inaundwa na kata 18 na mitaa 192. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, kulikuwa na wakazi 151,345, wanaume wakiwa 71,932 na wanawake 79,413.
No comments:
Post a Comment