Na Friday Simbaya, Kilolo
OFISA Tathimini na Ufuatiliaji wa Shirika la MMADEA kupitia mradi wa afya bora kwa ustawi wa jamii, Hezron Kalolo amewataka viongozi wa serikali za kijiji na wananchi kwa ujumla kujenga mazoea ya kuweka akiba ya fedha zitakazowasaidia pindi wanawake wanapo karibia kujifungua na baada ya kujifungua badala ya kusubiri serikali.
Alisema kuwa pamoja na changamoto zilizopo zinazowakabili wananchi wa vijiji mbalimbali, lakini shirika la MMADEA linatoa elimu juu ya afya ya uzazi na madhara ya mimba za utotoni katika vijiji kumi na moja (11) vya mradi.
Hezron alisema haya jana kuwa mradi huo unatekelezwa katika kata za Idete, Nyanzwa na Ibumu kupitia ufadhili wa shirika la Foundation for Civil Society (FCS), huku wakifanya kampeni ya kuibua uelewa wa watu juu ya changamoto za sekta ya afya.
Alisema kuwa Wilaya ya Kilolo ni moja ya wilaya ya Mkoa wa Iringa yenye changamoto ya mimba za utotoni na ndoa za utotoni ambapo wasichana wengi hupata mimba kabla yakifikisha miaka 18.
Aidha, Afisa Tathimini na Ufuatiliaji wa Shirika lisilo la kiserikali la MMADEA huyo alizitaja baadhi ya visababishi vya mimba za utotoni kuwa ni kiwango kidogo cha elimu ya uzazi, umaskini, tamaa, ngono zembe, shinikizo rika, ndoa za utotoni na utamaduni.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Idete wilayani Kilolo, mkoani Iringa wameiomba serikali kuwajengea zahanati kwa ajili ya kuweza kuboresha huduma za afya ya uzazi kijijini hapo.
Walisema kijiji hicho hakina zahanati ya serikali kunakopelekea kuongezeka kwa vifo vya wajawazito na watoto vitokanavyo na uzazi, kumbe kungekuwepo na zahanati ya serikali huduma za afya zingetolewa kwa gharama nafuu kupitia mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF).
Wakizungumza jana katika nyakati tofauti wakati wa mkutano wa hadhara, wananchi hao walilipongeza shirika lisilo la kiserikali la Mazombe Mahenge Development Association (MMADEA) la mkoani Iringa kwa kutoa elimu ya masuala ya afya ya mama na mtoto, huku wakisema kumekuwa na hali yasintofahamu katika kutetea afya zao.
Walisema kuwa wanatumia gharama kubwa za huduma za afya kutokana na zahanati iliyopo ambayo sio ya serikali kutoza gharama kubwa za matibabu na kuongeza kuwa kungekuwepo na zahanati ya serikali gharama hizo zingekuwa nafuu.
Wananchi hao walisema kuwa wamekuwa wakilazimika kutembea mwendo mrefu kutoka Kijiji cha Idete hadi Kituo cha Afya cha Kidabaga kilichopo katika kata nyingine wilayani kilolo, mkoani Iringa.
Walisema kuwa kukosekana kwa kituo cha afya katani kwao ni sababu inayopelekea wananchi hao kutembea kwa mwendo mrefu kufuata huduma ikichangia na miundombinu mibovu ya barabara, ambapo magari mengi yanashindwa kufika na kulazimika kukodi gari ya kanisa katoliki kwa gharama kubwa kutokana na kutokuwepo gari la wagonjwa katika zahanati ya inayomilikiwa na kanisa la KKKT.
Walisema kuwa kungekuwepo na mfuko wa afya wa CHF kungesaidia katika kupunguza gharama za huduma za afya huku wa kihoji kwanini wachangie gharama kubwa ya gari ya wagonjwa kutoka halmashauri wakati serikali inatoa huduma bure za afya ya uzazi.
Wananchi hao wa Kijiji cha Idete, wilayani Kilolo mkoani Iringa wapo hatarini ya kukumbwa na changamoto ya kuwapoteza wanawake wajawazito na watoto kutokana na umbali wa kituo cha afya, huku wakilazimika kuchangia gari la wagonjwa kutoka halmashauri na la kanisa katoliki.
Tumpe Mwadisa ni mkazi wa Kijiji cha Idete, akiongea na mwandishi wa habari wa Nipashe wakati akishuhudia akipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Iringa ya Rufaa ambako alikwenda kujifungua kwa kupata msaada wa gari la halmashauri lililofika kijijini hapo kwa shughuli zingine.
Alisema kuwa changamoto ya kuwapoteza wanawake wajawazito na watoto inatokana na kutokuwepo zahanati ya serikali na kituo cha afya kwa kata nzima ya Idete.
Kwa upande, wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Idete, Bimas Mkemwa pamoja na Diwani wa Kata ya Idete Bruno Kauku wamesema kuwa elimu inayotolewa na shirika la MMADEA imewafungua kwa kiasi kikubwa wananchi, kwani hawakuwa na elimu ya kutosha juu ya mfuko wa afya jamii na upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi. huku wakiiomba serikali kuwajengea zahanati ili kunusuru maisha ya mama na mtoto.
Kufuatia hali hiyo wakazi na viongozi wa Kijiji cha Idete katika kata Idete, wilayani Kilolo mkoani Iringa wameiomba serikali kusaidiana kujenga zahanati ili waweze kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu hususan wajawazito ya kufuata huduma za afya.
Hata hivyo, wananchi wamelia na viongozi wa kitaifa kutofika kijijini hapo kwa miaka mingi ili kujionea adha wanazozipata wananchi wa kijiji hicho pamoja na kijiji hicho kuwa ni makao makuu ya kata.
Mwisho
No comments:
Post a Comment