Gari la Jeshi la zimamoto na uokoaji la mkoa wa Iringa likiwa limepinduka na kujeruhi watu watano katika kijiji cha Ikengeza, Kata ya Isimani wilayani Iringa, mkoani Iringa juzi.
Jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Iringa halina gari la zimamoto baada ya gari hilo kuacha njia na kupinduka na kujeruhi askari wanne wa jeshi hilo akiwemo raia mmoja katika Kijiji cha Ikengeza tarafa ya Isimani wilayani Iringa usiku wakuamkia jana, kilometa tano kutoka barabara kuu ya Iringa-Dodoma.
Akiongea na nipashe jana kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Iringa Kennedy komba alisema askari watatu kati ya wanne wa kikosi cha zimamoto na uokoaji Manispaa ya Iringa walipata ajali ya gari jana usiku saa 4:45 wakati wakielekea kuzima moto kijiji cha Ikengeza.
Alisema raia huyo ambaye alikuwa kwenye gari hilo aliombwa na askari hao ili kuwaongoza kufika katika kijiji hicho lakini hata hivyo gari hilo halikufanikiwa kuzima moto baada ya dereva gari la zimamoto lenye mzigo wa maji ya Lita 7500 baada ya gari kumshinda kwenye kona kali.
Alisema kuwa majeruhi hao walikimbizwa mara moja katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa ambako walilazwa kwa matibabu na baadaye kuruhusiwa.
Kamanda komba alisema askari hao walikuwa wakienda kufanya kazi ya kuokoa maisha na mali ya mkazi mmoja wa Mkungugu ambaye nyumba yake ilikuwa ikiwaka moto majira ya usiku lakini safari yao ikaishia Ikengeza.
Alisema kuwa tayari ofisi ya mkuu wa mkoa wa iringa imekwisha shughulikia suala la kuvuta gari hilo kutoka eneo la tukio ili kuileta mjini Iringa kwa matengenezo (TEMESA), kwani alisema gari hilo ni pekee mkoa wa Iringa hivyo bila kulifanyia matengenezo ni hatari kwa usalama wa mkoa iwapo moto utatokea .
Katika kuendeleza juhudi za kupunguza na kutokomeza majanga ya moto yanayoikabili jamii, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea na zoezi la utoaji elimu juu ya Kinga na Tahadhari dhidi ya Majanga ya Moto mkoani.
“Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linajukumu kubwa la kutoa huduma kwa jamii katika Nyanja mbalimbali zikiwemo Kuokoa maisha ya watu na mali zao, Kuzima moto, Kutoa elimu ya kinga na tahadhari ya majanga moto, Kufanya ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto, Kusoma ramani za majengo na kutoa ushauri, Kutoa huduma ya kwanza katika majanga na ajali barabarani, Kutoa mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto, Kufanya uchunguzi kwenye majanga ya moto na Kutoa huduma za kibinadamu,” alisema.
Huduma ya Zimamoto inatolewa bure na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji hivyo basi wananchi kutumia namba ya dharura 114 mara tu wapatwapo na majanga ili kurahisisha uokoaji wa Maisha na Mali kwa haraka.
Aidha, Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza amewatembelea askari wa jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Iringa jana ambao walipata ajali ya gari juzi usiku wakati wakielekea kuzima moto kijiji cha Ikengeza.
Akizungumza na majeruhi watatu ambao wameruhusiwa jana kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa ambako walilazwa kwa matibabu ,mkuu wa mkoa alisema amepokea kwa masikitiko makubwa juu ya ajali hiyo na kuwa bado anamshukuru Mungu kwa kuwaepusha salama katika ajali hiyo.
Pamoja na kuwapa pole askari hao waliojeruhiwa bado mkuu huyo wa mkoa alimpa pole kamanda wa jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Iringa Kennedy Komba kwa askari wake kupata ajali.
No comments:
Post a Comment