Monday, 8 May 2017

ANSGAR CUP 2017 PERAMIHO, NGOMA 'INOGILE'





Na Alex Mapunda, Ruvuma

MWAKILISHI wa Kata ya Peramiho katika Mashindano ya Ansgar Cup ngazi ya Tarafa, timu ya Afya Fc imefanikiwa kuitandika bila huruma Kilagano Fc timu toka Kata ya Kilagano kwa kichapo cha bao 3-0.


Katika mchezo huo ambao Mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Simon Bulenganija, bao la kwanza la Afya Fc liliwekwa kimiani na mshambuliaji machachari Emanuel Kajana dakika ya 39 ambalo liliwachanganya wachezaji wa Kilagano FC na wakaanza kucheza kwa Tahadhari kubwa.

Dakika 15 za kipindi cha pili Kilagano Fc walicheza vizuri mno na walifanikiwa kufanya mashambulizi ya mara kwa mara katika lango la Afya Fc, lakini mambo yalikuwa tofauti baada ya mchezaji wa Afya Fc Shabiru Kinunga kuipatia timu yake hiyo bao la pili lililopeleka majonzi kwa Kilagano Fc mnamo dakika ya 60 ya mchezo.

Lakini Kabla ya mpira kumalizika mfungaji wa bao la kwanza Emanuel Kajana alishindilia msumari wa moto katika vidonda vya Kilagano Fc kwa kuipati Afya Fc bao la tatu kwa njia ya kichwa kunako dakika 88, bao ambalo lilikamilisha ushindi mnono wa bao 3-0 baada ya mwamuzi wa mpambao huo kupuliza filimbi ya mwisho kuashiria kwamba pambano limemalizika.

Katika mchezo wa mapema uliopigwa mishale ya saa nane mchana timu toka Kata ya Parangu ilikumbana na kipigo cha jumla ya bao 2-1 toka kwa Litisha Fc toka kata ya Litisha.

Kata zilizojitosa katika mashindano hayo ni Kata ya Peramiho, Litisha, Parangu, Kilagano, Lilambo, Maposeni, Mpandangindo pamoja na Liganga ambapo mechi za ufunguzi ilikuwa ni kati ya Litisha dhidi ya Parangu mishale ya saa nane mchana kisha saa kumi jioni Kilagano Fc wakakumbana na Peramiho (Afya Fc) kwenye uwanja wa Ansgar uliopo Peramiho B.

Mwaka huu zawadi zimeboreshwa toka shilingi 300,000/= kwa washindi wa kwanza hadi shilingi 400,000/= , 250,000/= washindi wa pili hadi shilingi 300,000 pamoja na 150,000/= washindi wa tatu hadi 200,000/= huku mchezaji bora akiambulia kifuta jasho cha shilingi 50,000/= hali ambayo imesababisha ongezeko la ushindani na kila timu shiriki inatamani kunyakua ubingwa wa mshindano hayo.

Ansgar cup ni moja ya ligi kongwe mkoani Ruvuma na imedumu kwa zaidi ya miaka 20, lengo kubwa la mashindano ya Ansgar yanayoandaliwa na mkurugenzi wa Hospitali ya Peramiho Dkt. Ansigar Stuffe OSB ni kuibua vipaji kwa wachezaji, burudani baada ya kazi, kuongeza soka la biashara kwa wafanyabiashara wa tarafa ya Peramiho n.k.

Baadhi ya wachezaji waliotokea Ansgar Cup ni pamoja ni Pato Ngonyani (MajiMaji na Yanga), Anold Nguruchi na wengineo wengi.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...