Monday, 29 May 2017

MKOA WA IRINGA UNA UPUNGUFU WA WALIMU 1,581


 
Afisa ya Elimu wa Mkoa wa Iringa Richard Mfugale (Picha na Maktaba)



Mkoa wa Iringa una upungufu wa walimu 1,581 katika shule za msingi na sekondari kwa shule za Serikali, imefahamika. 


Katika shule za msingi upungufu ni walimu 984 na shule za sekondari ni upungufu wa walimu 597 katika masomo ya sayansi. 


Hayo yalielezwa hivi karibuni na Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Richard Mfugale wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Elimu kwa mwaka 2017, yanakusudia kutumika kutoa msukumo mpya katika kuendeleza elimu hasa uimarishaji wa umahiri wa misingi ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK). 


Aidha afisa elimu huyo alisema kuwa Idadi ya walimu katika Shule za Sekondari za Serikali Mkoa ni jumla ya walimu 3,390 kati ya hao Walimu 837 ni walimu wa sayansi na walimu 2,553 ni wa masomo ya sanaa. 


Wakati idadi ya walimu katika Shule za Msingi za Serikali, mkoa unahitaji kuwa na walimu 6,240, waliopo ni walimu 5,256 na upungufu ni walimu 984. 


Mfugale pia alisema ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sayansi katika shule za sekondari, jumla ya vyumba vya maabara 321 vinahitajika. 


Kwa upande wa nyumba za walimu shule za serikali alisema zilizopo ni 559 mahitaji ni nyumba 2,880 na matundu ya vyoo yaliyopo ni 2,174 ikilinganishwa na mahitaji ya matundu 2679. 


Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya kusoma kwa Mkoa wa IRINGA alikuwa Mkuu wa Wilaya wa Mufindi, Jamhuri William kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza ambayo yalianza tarehe 19/05/2017 na kuihitimishwa kimkoa tarehe 25/05/2017 katika Halmashauri ya Mji wa MAFINGA ambapo Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa zilishiriki kikamilifu baada ya kuwa zimefanya maadhimisho hayo katika ngazi ya Halmashauri. 



Alisema Maadhimisho ya Wiki ya Elimu kwa mwaka 2017 yalikusudia kutumika kutoa msukumo mpya katika kuendeleza elimu, hasa uimarishaji wa umahiri wa misingi ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK). 


Masenza alisema kuwa serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais Dr. John Pombe Magufuli inafanya juhudi za dhati za kuhakikisha kuwa elimu inaboreshwa na kuondoa baadhi ya michango isiyo ya lazima kwa utekelezaji wa Elimu bila Malipo. 


Kaulimbiu mwaka huu inasema: “Ufundishaji bora wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu ni msingi wa maarifa, ujuzi na maendeleo ya elimu katika kufikia uchumi wa viwanda”. 



No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...