Shule ya Msingi Nyakadete iliyopo Kijiji cha Nyakadete Kata ya Madibira wilayani Mbarali, mkoani Mbeya inakabiliwa na uhaba wa nyumba za walimu na kupelekea baadhi ya walimu kuishi katika nyumba za familia za walimu wengine, imefahamika.
Hivi karibuni Nipashe ilitembelea shule hiyo na kubaina kuwa kuna nyumba tatu (3) tu za walimu wakati mahitaji ni nyumba tisa (9).
Kutokana na hali hiyo walimu wanalazimika kuishi kilometa 12 toka shuleni, kwa mfano mwalimu anatoka Kijiji cha jirani cha Mkunywa kilichopo katika Kata ya Madibira, wilayani Mbarali.
Walimu wengine wanaishi katika nyumba za familia ya mwalimu mwingine, yaani mwalimu kuwa kama sehemu ya familia ya mwalimu mwingine.
Meshack Salehe ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyakadete, alithibitisha uwepo wa hali hiyo, na kusema kuwa wapo baadhi ya walimu wanaoishi katika familia ya mwalimu mwingine kutokana na uhaba wa nyumba za walimu shuleni hapo.
Nipashe pia ilibaini kwamba shule hiyo pia inaupungufu wa vyumba vya madarasa na ukosefu wa maji safi na salama kutokana na kuaribika kwa kisima cha maji kwa muda mrefu.
Kutokana na hali hiyo ya kutokuwepo maji, wanafunzi wanatumia muda mwingi kutafuta maji toka mitaani na kupelekea kukosa muda wa masomo.
“Wanafunzi hawana muda wa michezo kwa sababu muda mwingi wanatumia kutafuta maji yatumia wao wenyeww na wakati mwingi ya walimu,” alisema Salehe.
Alitaja changamoto zingine kuwa ni kukosekana kwa maji ambapo kumechangia kuwafanya watoto wa kike kuwa katika wakati mgumu hasa wanapokuwa kwenye hedhi.
Alisema matatizo mengi ya miundombinu ambayo huathiri zaidi watoto wa kike, yanatokana na changamoto za mfumo wa bajeti ya sekta ya elimu, hivyo suala la kuboresha miundombinu ya shule linapaswa kuwa kipaumbele zaidi kwa kuongeza fedha za bajeti ya maendeleo.
Shule hiyo inakabiliwa na ukosefu wa vifaa vya kufundishia somo la Teknolojia ya Habari na Mawsiliano (Tehama) kama vile kompyuta na kulazimisha mwalimu wa somo hilo kuchora ubaoni wakati wa kipindi cha somo hilo.
“Somo la Tehama ni somo muhimu katika shule zote za msingi na Sekondari ukizingatia wakati huu wa sanyasi na teknolojia ili kukidhi mahitaji ya dunia ya sasa, hasa kwa nchi yetu Tanzania,” alisema mwalimu mkuu.
Alisema kuwa TEHAMA imebakia katika nadharia tu, kwani walimu wengi wanaofundisha somo hili hawana vifaa vya kufundishia somo hilo na kupelekea mwanafunzi kutoelewa kinachoendelea darasani.
“Somo hili linabakia kukariri msamiati mgumu wa taaluma hii ili mwanafunzi aweze kujibu maswali atakayoulizwa katika mtihani na siyo kumwandaa kwa kuitumia taaluma hii katika maisha yake ya sasa na baadae.,” alisisitiza mwalimu mkuu.
Shule ya msingi Nyakadete ilianza mnamo tarehe 29/06/2004 ina wanafunzi zaid 250, na imeongozwa na walimu wakuu saba (7) tangu kuanzishwa kwake.
No comments:
Post a Comment