Askofu Mteule Mchungaji Blastone Tuluwene Gavile (kushoto) akiwa na Msaidizi wa Askofu Mteule Mchungaji Himid John Sagga.
IBADA ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Mchungaji Blaston Tuluwene Gavile, inatarajiwa kufanyika Jumapili Juni 25, 2017 mjini Iringa.
Ibada hiyo, ambayo itaambatana na kuingizwa kazini kwa Msaidizi wa Askofu, Mchungaji Himid Sagga, itafanyika ikiandika historia kwenye Dayosisi hiyo ambapo Askofu Mteule Gavile anachukua nafasi ya Askofu Dkt. Owdenberg Moses Mdegela ambaye amestaafu.
Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Nayman Chavalla, amesema tukio hilo maalum ni la pili katika historia ya Dayosisi hiyo, kwani Mchungaji Gavile anakuwa ndiye askofu wa pili tangu kuanzishwa kwake.
Aidha, katika ibada hiyo Askofu Mteule Blaston Gavile atamuingiza kazini Msaidi wake Mchungaji Himid John Sagga.
Awali akielezea jinsi ibada hiyo itakavyokuwa, Chavalla alisema itaanza kwa maandamano ya Wachungaji na washarika kutoka Usharika wa Kanisa Kuu Iringa Mjini mpaka viwanja vya Gangilonga ambako ndiko ibada hiyo itafanyika.
"Ibada hiyo inatarajiwa kuongozwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Fredrick Shoo akisaidana na Baba Askofu Mstaafu Dkt. Mdegella," alisema.
Pia katika ibada hiyo viongozi wa Makanisa mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi, Wawakilishi wa vyama vya Kimisionari, Viongozi wa Kiserikali, vyama vya siasa, wageni kutoka nchi mbalimbali, wawakilishi wa makampuni na mashirika mbalimbali watahudhuria.
Katibu Mkuu alitoa wito kwa jamii na Wakristo wote kuendelea kuliombea jambo hilo.
Alimalizia kwa kusema ibada inatarajia kuanza kwa maandamanao yatakayoanza saa mbili kamili asubuhi.
Askofu Mteule Mchungaji Blastone Tuluwene Gavile (kushoto) akiwa na Msaidizi wa Askofu Mteule Mchungaji Himid John Sagga.
No comments:
Post a Comment