Maofisa wa Chama hicho wakiwa meza kuu wakati wa mkutano na wanahabari.
Wabunge wa chama hicho wakiwa kwenye mkutano huo.
Baadhi ya wanahabari wakiwa kwenye mkutano huo.
Wapiga picha kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
Na Dotto Mwaibale
CHAMA cha Wananchi (CUF), kinatarajia kumfikisha mahakamani Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kukiuka taratibu za sheria ya wadhamini kwa kutojiridhisha juu ya uhalali wa majina ya Bodi ya Wadhamini yaliyofikishwa kwake kama yalipitishwa na kikao halali cha chama kwa mujibu wa katiba.
Kauli hiyo ameitoa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif jijini Dar es Salaam leo wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema wanachukua hautua hiyo kutokana RITA kushindwa kutumia mwongozo na weledi katika kutekeleza majukumu yao na badala yake wamesukumwa na utashi binafsi kwa ajili ya hujuma dhidi ya chama hicho.
“Chama chetu kimepatwa na mshituko mkubwa sana, kuona taasisi kubwa na yeti yenye dhamana kubwa katika nchi inaweza kufanya vitendo vya ovyo. RITA ni taasisi inayobeba maisha ya watu ya kila siku. Licha ya kusajili Bodi za Wadhamini, inasajili vizazi na vifo, ndoa, talaka na inatunza wosia kwa ajili ya mirathi,” alisema Maalim.
Alisema michakato wa kufungua kesi hiyo inaanza leo ambapo alieleza kuwa tayari wamekwisha agiza mwawakili kulishughulikia. Kutokana na matarajio ya ufunguzi wa kesi hiyo watawasilisha maombi mbele ya Mahakama Kuu kuitaka isimamishe kesi nyingine zote walizofungua kuhusiana na kadhia hiyo hadi hapo shauri linalohusu uhalali wa maamuzi ya RITA litakapoamuliwa.
Maalim alisema kusajiliwa kwa bodi hiyo ambayo aliiita kuwa ni bodi feki, alieleza kwamba ni mwendelezo wa kukihujumu na kukidhoofisha chama kunakofanywa dola kupitia kwa Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na Profesa Ibrahim Lipumba na kundi lake.
Alitaja mambo manne ambayo yalikuwa msukumo wa kusajiliwa kwa bodi hiyo. Alisema kuwa ni kwa ajili ya kufuta kesi zote zilizofunguliwa na ambazo zinawaelemea licha ya kutumia nguvu kubwa ya dola, kufungua akaunti mpya ya benki ili kumwezesha Profesa Lipumba kupata ruzuku.
Aliongeza mengine kuwa ni Bodi hiyo kuwezesha udhibiti wa Ofisi za Makao Makuu, Zanzibar pamoja na kumwondoa madarakani Katibu Mkuu Maalim Seif Hamad na hivyo kufanikisha njama za kuwapokonya haki Wazanzibar kwa maamuzi yao ya Oktoba 25 mwaka 2015.
Hamadi alisema kamwe haki ya Wazanzibar haitapotea na kuahidi kuwa ndani ya miezi mitatu haki hiyo itakuwa imepatikana.
No comments:
Post a Comment