Katibu Mkuu Msaidizi wa Mkoa wa Iringa wa Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Hoteli, Majumbani na Huduma za Jamii na Kazi zinginezo (CHODAWAU), Silvester Mshana Mfumu amewataka waajiri mkoani hapa kuwalipa mikataba ya ajira wafanyakazi wao kabla ya sheria haijakuchua mkondo wake.
Alisema kuwa mkataba wa ajira ni makubaliano yanayofanywa na mtu au taasisi inayoitwa mwajiri kwa upande mmoja, na mtu anayefahamika kama mwajiriwa kwa upande mwingine kwa lengo la kuainisha haki na wajibu wa pande hizi mbili.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, namba 6 ya 2004, mwajiri ni mtu au taasisi inayomlipa mtu mwingine ujira kwa ajili ya kutoa huduma, ujuzi au nguvu kazi inayofanikisha shughuli zake.
Mshana alisema kuwa mwajiriwa, kwa upande mwingine, ni mtu mwenye sifa na uzoefu anayefanya kazi chini ya mamlaka ya mtu mwingine au taasisi akilipwa kwa minajili ya kutumia uzoefu na sifa .
Alisema kuwa mwaka wa fedha wa kiserikali umeanza na kuwataka waajiri kutoka sekta zinazohusu CHODAWAU kuwatapitia mikataba ya ajira waajirwa na wanachama kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini na Kanuni zake za Mwaka 2004.
Katibu msadizi huyo wa CHODAWAU alisema hayo jana wakati wa mahojiano maalum na NIPASHE na kuongeza kuwa kuwepo kwa mikataba hiyo kutasaidia kupunguza migogoro isio ya lazima pamoja na kuleta ufanisi katika kazi.
Mshana alisema kuna waajiri bado hawajanza kulipa kima cha chini cha mishahara baada ya serikali kupitia bodi ya mishahara iliyotangaza kwa sekta zote mwezi wa saba mwaka 2013.
Haki hizi ni pamoja na kupatiwa mkataba wa kazi, kufahamu ameajiriwa katika nafasi gani na majukumu yake ni yapi, ili asije akafanya majukumu yasiyomhusu.
Alisema kuwa mfanyakazi ana haki ya kwenda likizo, kupatiwa likizo ya matibabu pamoja na likizo ya uzazi.
Alisema kuwa kuna baadhi ya waajiri ambao bado hawajaanza kutekeleza agizo la Serikali la kupandisha mishahara ya wanafanyakazi kwa sekta binafsi kama ilivyopendekezwa na bodi ya mishahara nchini ya mwaka 2013.
“Tutaanza kuwahesabia waajiri mapunjo kwa wafanyakazi kwa wanachama wote wa CHODAWU kwa sababu Serikali kupitia bodi ya mishahara nchini litangaza viwango mbalimabli vya mishahara ikiwemo sekta binafsi, ambapo walitakiwa kuanza kulipa viwango hivyo kuanzia tarehe moja mwezi wa saba mwaka 2013, ” alifafanua Mshana.
Mfanyakazi ana haki ya kulipwa malipo stahiki yanayoendana na kazi anayofanya na kiwango kilichowekwa na Serikali kwa mujibu wa sheria.
Sheria pia imeweka wazi wajibu wa mfanyakazi kuwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii, kufikia malengo ya mwajiri, usiri, utii, nidhamu na uaminifu.
“Msingi wa uhusiano wa kiajira baina ya mfanyakazi na mwajiri ni mkataba wa ajira. Mkataba wa ajira unaweza kuwa wa mdomo au wa maandishi. Ili kuhakikisha mambo ya msingi yanawekwa wazi Sheria inamtaka mwajiri kumpa mfanyakazi maelezo ya ajira yake kwa maandishi,” alisema Mshana
Waajiriwa wengi, hususani kwenye sekta binafsi, wanafanya kazi bila kuwa na mikataba. Utendaji na usalama wa wafanyakazi hawa, kwa kiasi kikubwa, unategemea hisani na uaminifu wa mwajiri.
Kufanya kazi bila mkataba kuna hatari kadhaa. Kwanza, panakosekana ushahidi wa kisheria kuwa umeajiriwa. Katika mazingira haya, inapotokea unapata matatizo kazini, itakuwa rahisi zaidi kupoteza kazi yako.
Vile vile, kutokuwa na mkataba kunakuweka kwenye hatari ya kupoteza haki zako za msingi kama mfanyakazi anayelindwa na sheria za nchi.
No comments:
Post a Comment