Mkoa wa Iringa unakabiriwa na tatizo la hosteli kwa wanafunzi kwa kiasi kubwa si tu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, bali hata kwa wanafunzi wanaosoma katika shule za sekondari.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Sekta za Uzalishaji, Fikira Kisimba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza wakati wa akifungua semina ya elimu kwa uma kuhusu mikopo ya nyumba Tanzania.
Alisema kuwa wanafunzi wengi hasa vijijini wanakaa mbali na maeneo ya shule hivyo huwapasa kutembea muda mrefu na kufika shuleni wamechoka na kushindwa kufuata vizuri mosomo yao.
Aidha Kisimba alisema kuwa Mkoa wa Iringa umejipanga vyema kuwa kitovu cha utalii na uwekezaji, juhudi hizo zote zinahitaji ukuaji wa haraka wa sekta ya nyumba. Alisema kuwa wanahitaji kuwa na hoteli za kisasa, super markets za kisasa, kumbi za mikutano na hasa kwa kuzingatia makao makuu ya serikali sasa yamehamia mjini Dodoma, mji ambao ni jirani na Iringa.
“Tunajukumu kubwa la kuendeleza nyumba na makazi yetu ili kukidhi azma hii,” alisema Kisimba.
Kisimba alitoa wito kwa Benki Kuu kuhimiza mifuko hiyo ya mikopo midogo midogo ya nyumba isogeze huduma zake ndani ya mkoa, manispaa na halmashauri ili kusaidia kuboresha makazi hasa kwa watumishi na wakazi wa Mkoa wa Iringa.
Naye Mratibu wa Mafunzo Elimu ya Mikopo ya Nyumba Tanzania, Dkt Felician Komu alisema serikali inatekeleza mradi wa mikopo ya nyumba kupitia Benki Kuu ya Tanzania.
Alisema kuwa madhumuni makuu ya mradi ni kuandaa mazingira rafiki ya kukuza soko la mikopo ya nyumba nchini na yenye riba nafuu.
Komu alisema kuwa mkopo wa nyumba ni utaratibu wa utoaji wa mkopo kati ta taasisi za fedha au benki na mkopaji mwenye kuhitaji fedha kwa ajili ya ama kugharamia ununuzi wa nyumba, ujenzi wa nyumba au maboresho na ukarabati wa nyumba kwa ajili ya mkopo wa muda mrefu.
Aidha, Manispaa ya Iringa ni kati ya miji minane iliyopewa nafasi maalum katika kuenza elimu ya mikopo ya nyumba nchini. Kampuni ya Tanzania Real Estate Settlement and title Assurance Co Ltd (TRESTA) ya jijini Dar es Salaam inasimamia utekelezaji wa mafunzo ya mikopo ya nyumba Tanzania.
Aliongeza kuwa mwananchi yeyote anastahili kupata mkopo ilimradi athibitike; ana uwezo wa kurejesha mkopo kwa kiwango kitakachokubaliwa kwa kila mwezi pamoja na kuwa na historia nzuri kurejesha madeni.
No comments:
Post a Comment