Saturday, 23 September 2017

WANAFUNZI NA WALIMU WA SHULE YA UFUNDI IFUNDA WAMPONGEZA JPM KWA UKARABATI


makamu mkuu wa shule Peter Mbata (kulia) na Amon Chota (mtaaluma).


mwalimu mkuu wa shule ya sekondari ya ufundi Ifunda, Mpambwe Paul 



mafundi wakiendelea na ukarabati wa shule kongwe ya ifunda ufundi kama walivyokutwa na mwandishi wetu jana (Picha na Friday Simbaya)




Wanafunzi na walimu wa shule ya ufundi Ifunda (Ifunda Technical Secondary School) mkoani iringa wameipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufufua na kuboresha miundombinu ya shule yao.

Walisema kuwa baada ya mpango wa serikili kuamua kuanza ukarabati wa shule kongwe nchini ikiwemo Ifunda utachangia ufaulu bora kwa wanafunzi pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kufundishia na kujisomea.

SIMBAYABLOG jana ilitembea shule hiyo kongwe ya Ifunda na kujionea ukarabati unaondelea kwa kusimamiwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST). 

Derika Makoi ni mwanafunzi wa kidato cha tatu alibainisha kuwa ukarabati huo unaoendelea utachangia wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao kwani hapo awali wakati miundombinu ilikuwa mibaya wanafunzi walikuwa wanatumia mishumaa kujisomea.

Alisema kuwa ukabarati ambao unaendelea katika madarasa na mabweni umeboresha mazingira ya wanafunzi ya kujisomea kwani hata madarasani kumekuwa na umeme wakati hapo awali wanafunfuzi walikuwa nasomea mabwenini.

Makoi alisema kujisomea mabwenini hakukuwa rafiki sana kwa kujisomea kwani kulikuwa na mchanganyiko wa wanafunzi wanaolala humo na pengine makelele kutoka kwa wanafunzi wa madarasa ya chini.

“Tulikuwa tunalazimika kutumia mishumaa kujisomea madarasani kwa vile madarasa hayakuwa na umeme lakini kwa sasa tunashukuru serikali kwa kukarabati pamoja na kuboresha miundombinu ya shule yetu,” alisema Makoi.

Alisema kuwa katika ukarabati unaoendelea umekuwa na faida nyingi kuliko hasara kwa wanafunzi sasa wanajiamini kwa kujisomea muda wote kwa sababu madarasani kuna mwanga muda wote.

Mwanafunzi mwingine wa kidato cha tatu alisema ukarabati huo umeboresha mazingira katika madarasa kwa madarasa mengi hayakuwa na milango na vioo madirishani kipindi cha baridi walikuwa wanapata shida.

Alisema kuwa kuna wakati mwingine upepo ulikuwa unapuliza mpaka kupeperusha makaratasi wakati wa kujisomea lakini baada ya ukarabati mazingira yamekuwa mazuri.

Alisema hapo awali madarasa machache yalikuwa na umeme kwa hiyo wanafunzi wanafanya prepo muda wote kutokana na madarasa mengi kuwa na umeme mpaka wanajisomea hadi usiku.

Alisema kuwa ukarabati pia uangalie suala la maji kwani shule hiyo ina miundmbinu mibovu ya maji kwani wanafunzi wanatumia muda mwingi kutafuta maji kutokana na visima vya maji kuwa vichache.

Alisema kuwa maji ni afya kwa hiyo serikali isaidie pia katika kuboresha miundombinu ya maji shuleni ili wanafunzi watumie muda mwingi kujisomea.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya sekondari ya ufundi Ifunda, Mpambwe Paul aliishukuru serikali kwa kukarabati shule yao kwani mpango utainua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.

Alisema kuwa kupitia mpango huo mazingira ya shule pia utachangia ufaulu bora kwa wanafunzi na pia watakuwa na mazingira bora ya kufundishia kwa vile miundombinu itakuwa rafiki kwa kufundishia na kujisomea kwa upande wa wanafunzi.

Walimu wengine waliounga mkono mpango wa serikali kwa ukarabati huo ni makamu mkuu wa shule Peter Mbata na Amon Chota (mtaaluma).

Mpambwe alisema kuwa ukarabati huo unahusisha madarasa yote, mabweni yote pamoja na jengo la utawala isipokuwa nyumba za walimu.

Hivi karibuni serikali kupitia wizara ya elimu, sayansi, teknolojia na mafunzo imeanza mpango kabambe wa kukarabati shule zote kongwe nchini baada ya shule kongwe za Serikali kufanya vibaya katika mitihani ya taifa kwa kipindi cha takribani miaka mitano mfululizo.

Serikali imeanzisha mpango kabambe wa kufufua hadhi na kuziboresha zaidi shule hizo.

Katika Bunge lililopita, Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Joyce Ndalichako alibainisha kuwa kwenye bajeti ya mwaka 2016/17, Serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 33 kwa ajili ya kukarabati shule kongwe zote nchini na kwa kuanza, jumla ya shule 20 zitakarabatiwa kupitia mpango huo ambapo Sh bilioni 20 zimetengwa kwa kazi hiyo.

Ilisema kuwa shule kongwe 10 Jangwani, Azania, Kibaha, Nangwa, Kigoma, Tosamaganga, Shule ya Wasichana ya Songea, Malangali, Mirambo na Minaki tayari zimekabidhiwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na kazi ya ukarabati imeanza na zinatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu.

Shule 10 nyingine ambazo ni Mpwapwa, Kibiti, Ifakara, Bwiru -Wavulana, Kantalamba, Moshi-Ufundi, Tanga-Ufundi, Musoma- Ufundi, Ifunda - Ufundi na Mtwara- Ufundi zimekabidhiwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST).

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...