IRINGA: Viziwi mkoani Iringa wameishukuru Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kuendesha mafunzo ya elimu ya umma ya utambuzi wa alama za usalama za noti halali.
Walemavu hao walitoa kauli hiyo jana kwenye risala iliyosemwa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza, ambapo jumla ya viziwi 50 walipatiwa mafunzo ya utambuzi wa alama za usalama za noti halali.
Walisema kuwa semina hiyo ni muhimu sana kwao kwa sababu itawawezesha kutambua noti halali na halisi kwa walemavu wa kusikia mkoani Iringa.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na kituo cha sanaa na utamaduni kwa viziwi Tanzania (KISUVITA) kwa kushirikiana na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) mkoa wa Iringa.
Akisoma risala mwenyekiti wa KUSUVITA, Habibu Mrope kwa niaba ya walemavu alishukuru BOT kwa kuwezesha mafunzo ikiwa ni mwendelezo wa zile, ambazo zimekwishafanyika katika mikoa ya Lindi, Dodoma, Singida, Ruvuma, Njombe, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Mara, Kigoma, Tabora na Kagera tangu mwaka 2010.
KISUVITA ni asasi isiyo ya kiserikali na isiyolenga faida, iliyoanzishwa kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya viziwi pamoja na upatikanaji wa haki za katika Nyanja mbalimbali za maisha kupitia sanaa ya utamaduni.
Mrope alisema kwa wakati asasi, mashirika binafsi, vyama vya siasa, serikali na taasisi zake zikiendesha semina, makongamano, mikutano ya hadhara kwa ajili ya masuala mbalimbali katika tasnia ya afya, eleimu, utamaduni, uchumi na kijaamii, viziwi hawafikiwi na program hizo.
Alisema kuwa mbaya zaidi hawashirikishwi katika masuala mbalimbali ikiwamo ya utoaji wa maamuzi katika ngazi mbalimbali za kiserikali, kifamilia na kadhalika na kwa sababu hiyo wanaendelea kubakia nyuma kulinganisha na makundi mengine ikiwamo ya ulemavu mwingine.
Kwa upande wake, Meneja msaidizi, Idara ya uhusiano wa umma kutoka BoT makao makuu Vickoria Msina, alisema waliona ni muhimu kulielimisha kundi hilo, ili kuwawezesha kuepuka kubambikiziwa noti bandia kisha kuchukuliwa hatua za kisheria.
Msina aliwataka viziwi na jamii nzima kuzingatia njia tatu za utambuzi wa noti halisi na bandia.
Njia hizo ni pamoja na kuangalia, kushika na kutumia vifaa vinavyonunuliwa katika maduka ya umeme.
Alisema kuwa, katika kuangalia noti halisi picha ya baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere huonekana vizuri na nywele nyeupe, lakini katika noti bandia haonekani vizuri na picha huwa na weusi, na kuwa pia noti halisi mstari wake hung’aa na kucheza cheza huku katika noti bandia hauchezi hukaa tu.
Alisema kuwa, katika alama ya kuangalia noti halisi ikiwekwa sambamba inaonyesha maua, lakini ikiinuliwa hayo maua huonyesha alama ya thamani ya noti husika.
“Mfano kama ni noti ya shilingi 10,000 maua hayo ukiinua yataonyesha tarakimu ya shilingi elfu kumi, lakini bandia hata ukiinua itaonyesha maua tu” anasema.
Aidha alisema kuwa, katika alama ya kuangalia, nyuma ya noti katika kichwa cha twiga, hela halali ukiichezeshachezesha kichwa hicho kinabadilika na kuwa kijani kisha dhahabu, lakini hela bandia inabaki dhahabu tu haibadiliki.
Kuhusu njia ya pili ambayo ni ya kushika, anasema noti hushikwa sehemu mbili tu, ambazo ni kwenye pembe, ambapo hela halisi ikishikwa kwenye pembe itakwaruza lakini bandia itateleza tu.
“Pia sehemu iliyoandikwa fedha halali kwa malipo ya shilingi fulani nayo hukwaruza ukipitisha dole gumba tofauti na bandia ambayo huteleza tu,” anasema.
Mtaalam huyo anataja njia ya tatu ya utambuzi wa noti halisi na bandia kuwa ni ya kutumia vifaa vinavyouzwa katika maduka ya vifaa vya umeme ambavyo ni taa ya rangi (bulb) na taa maalum ya kuangalia noti bandia.
Msina alisema kuwa, mbali na kuwafundisha viziwi namna ya kuzitambua na kuzitofautisha noti hizo, pia walemavu wasioona nao kuna alama zao ambazo wanazitambua pindi wanapogusa noti yoyote halali.
Pamoja na elimu hiyo pia aliwataka wananchi kuzitunza vizuri fedha hizo ili zisichakae, maana zikichakaa husababisha serikali kushindwa kutekeleza kwa wakati miradi mbalimbali ya jamii, maana hulazimika kuchukua noti zilizochakaa kwenda kutengeneza hela nyingine, badala ya kuzipeleka kwenye matumizi ya miradi. Na Friday Simbaya, Iringa
No comments:
Post a Comment