Wakati dunia ikisherehekea siku ya Utalii Duniani, Jumia Travel imebainisha kwamba matumizi ya tekinolojia za kisasa hususani mtandao wa intaneti una manufaa makubwa katika kuvitangaza vivutio vya kitalii kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati alipotembelea nchini Tanzania, Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel Kimataifa, Bw. Abdesslam Benzitouni ameweka wazi kwamba Tanzania haina budi kutumia ipasavyo njia zote za kidigitali ikiwemo mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Youtube na Instagram kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watumiaji.
“Intaneti imekuwa na mchango mkubwa kwenye sekta ya utalii na ukarimu hususani kwenye kutoa taarifa. Tofauti na kipindi cha nyuma hivi sasa watu wanaweza kupata taarifa muda wowote na mahali popote walipo bila ya kutembelea moja kwa moja eneo husika. Jumia Travel inazitumia njia zote za mtandaoni kuzionyesha na kuzitangaza hoteli pamoja na vivutio vya kitalii nchini. Tovuti na kurasa za mitandao yetu ya kijamii tuzipatia hoteli tunazoshirikiana nazo fursa kubwa ya kujitangaza na kuonekana mtandaoni ambapo kwa kiasi kikubwa huongeza idadi ya wateja,” alisema Benzitouni.
“Wakati dunia ikisherehekea siku ya Utalii Duniani, bara la Afrika limeshuhudia idadi ya watalii kufikia milioni 58 mwaka 2016. Na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka maradufu ndani ya miaka 15 ijayo na kufikia milioni 130. Mafanikio hayo yamechangiwa na ukuaji wa kasi wa sekta ya usafiri wa anga, ambapo mashirika ya ndani na kimataifa yana mchango mkubwa kwenye kuwasafirisha watalii ndani na nje ya nchi, ” aliongezea Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel Kimataifa.
Aliendelea na kufafanua zaidi kwamba kwa Tanzania kutajwa kuwa ni miongoni mwa nchi ambazo zinatembelewa zaidi barani Afrika, sawa na nchi zingine kama vile Morocco, South Africa, Rwanda na Namibia, ni dalili nzuri kwamba utalii unaleta tija kubwa na inaweza kunufaika nao kwa kutumia mbinu tofauti ili kuvutia wageni wa kimataifa zaidi.
“Kupitia ripoti ya Utalii na Ukarimu ambayo Jumia Travel tuliiwasilisha mapema mwaka huu, tuligundua kwamba idadi ya watalii kwa mwaka 2016 iliongezeka kwa 16%. Pia kuongezeka kwa idadi ya watanzania wanaotumia mtandao wa intaneti kunaashiria matumizi ya mifumo mipya ya kidigitali.
Tunaweza kuitumia katika kuvitangaza vivutio vyetu, kutoa taarifa za kutosha zaidi, pamoja na bei nzuri na zenye ushindani kwenye soko ili kurahisisha shughuli za kitalii. Tafiti zinaonyesha idadi kubwa ya watalii wanaotembelea Afrika wanatokea nchi za bara la Asia zaidi. Kwa mfano, 10% ya Wachina wanaosafiri duniani hutembelea zaidi nchi za Afrika,” alihitimisha Benzitouni.
Kati ya mambo ya msingi ambayo Jumia Travel inajitahidi kuyaangazia kwenye sekta ya utalii na ukarimu nchini Tanzania pamoja na kwingineko ilipo Afrika ni gharama za juu za malazi. Kwa waafrika wengi, malazi yamekuwa ni kati ya changamoto kuu inayokwamisha shughuli za kitalii kwa miaka kadhaa sasa.
Kulipatia ufumbuzi hilo kampuni hiyo imejizatiti kuhakikisha kwamba inaweka aina zote za malazi kwenye mtandao wao ili yafikiwa kwa urahisi na wateja. Lengo kuu ni kumuwezesha kila mtu aweze kupata huduma ya malazi kwa gharama nafuu licha ya uwezo alionao.
No comments:
Post a Comment