MENEJA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Iringa, Lampson Tulianje amesema kuwa wafanyabiashara wa hoteli mkoani hapa wana mwitikio mdogo wa kutoa risiti za EFD baada ya kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali na kubaini hilo.
Akizungumza mara na wanahabari mara baada ya kufanya zoezi la ukaguzi wa hoteli mbalimbali mkoani hapa, Tulianje alisema kuwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa zao pasipo kuwapatia risiti za mashine za Kielektroniki (Efd) wateja wao mara kwa mara hali inayokosesha TRA mapato.
Alisema kuwa kampeni hiyo imeendelea kufanyika katika hoteli zote mkoani hapa kwa kushtukiza hali ambayo wanakutana nayo ni wafanyabiashara hao kutoa risiti kwa wateja wachache tofauti na wanavyowahudumia wateja wengi kwa siku.
Alisema kuwa kutona na hali hiyo TRA mkoa wa Iringa itaendelea kufanya zoezi hilo kuhakikisha wafanya biashara wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za biashara katika mauzo ya bidhaa zao kwa kutoa risiti kwa kila mteja wanayemhudumia.
Tulianje alisema kuwa kila bidhaa inayouzwa inapaswa kutolewa risiti, zikiwamo bia hivyo, maafisa wa TRA watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wafanyabiashara wote ambao wanahitajika kutumia mashine hizo wanatumia ili kuingizia mapato serikali.
"Lengo la TRA sio kuwafungia biashara hawa wafanyabiashara lakini endapo watashindwa kufata sheria hatua stahiki zitachukuliwa bila hofu yoyote na hatupendi kuwapiga faini lakini italazimika kufanya hivyo, kwani tunasimamia sheria na imeonekana idadi kubwa ya wafanyabiashara mkoani hapa hawatumii mashine za EFD kama ambavyo inatakiwa,"alisema.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kuhakikisha wanatoa na kuchukua risiti wakati wowote wanapouza au wanapofanya manunuzi na endapo wafanyabiashara ambao mashine zao zimeharibika wanapaswa kutoa taarifa TRA kwa barua na sehemu waliyonunua mashine ili kuhakikisha hawatozwi faini kwa kutotumia mashine hizo.
No comments:
Post a Comment