Ikiwa bado siku moja kukamilika kwa siku ya arobaini tokea kujitoa muhanga kwake Imam Hussein ambaye pia ni Mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (S.AW), Watanzania wametakiwa kuenzi mafundisho yake kwani enzi za uhai wake Imam alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa utukufu wa mwadamu, heshima yake unaenziwa kwa kiasi kikubwa na pia hakuna ubaguzi wa aina yoyote unao endekezwa.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake, Kiongozi Mkuu wa Waislam Dhehebu la Shia Ithnasheriya Tanzania Sheikh Hemed Jalala amesema Waislamu takribani Milioni 30 watakwenda katika kaburi la Mjukuu huyo wa mtume kuazimisha siku hiyo huku wakikumbuka mafunzo yake matakatifu ya kumtukuza Mwanadamu na kupinga kabisa aina yeyote ya ukandamizaji na unyanyapaa kushamiri miongoni mwa Wanadamu.
“Imam Hussein alikuwa ni mtu aliyependa kuenzi utakatifu, utukufu na kuheshimu utu wa Mwanadamu…darsa zake zote ukizisoma utaona alikuwa akisisitiza kuhusu watu kushirikiana, hakupenda kabisa watu kunyanyapaliana, kuwepo kwa matabaka… nadhani hata sasa dunia inahitaji kuwa na mafundisho kama hayo” Alisema Sheikh Jalala.
Inaelezwa kuwa Imam Hussein (a.s), ambaye ni Mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w), alijitoa Muhanga siku ya Ashura, maisha yake na familia yake na Masahaba zake kwa ajili ya kupigania Haki na Ubinadamu uliokuwa umekanyagwa na Mtawala anayedaiwa kuwa dhalimu Bw. Yazid Ibn Muawiyyah.
KWA UFUPI
Imam HUSSEIN (a.s). Kwa ufupi, Imam Hussein ni kiongozi aliyeonesha dira ya namna ya kupambana na DHULMA ulimwenguni kama Mahatma Gandhi (Baba wa Taifa la India) na Rabindranath Tagore (Indian Nobel Prize in Literature 1913), Thomas Carlyle (Scottish historian and essayist) , Charles Dickens (English novelist) Edward G. Brown (Professor at the University of Cambridge walivyomulezea Imam Hussein katika maandishi mbalimbali wakihusianisha mafanikio ya harakati nyingi za kudai haki na Imam Hussein (A.S).
Kwa huzuni kabisa, tunatoa mkono wa pole kwa Mtume (s.a.w.w) na familia yake (Ahlulbayt), pia kwa waislam wote ulimwenguni na wapenda haki pasina kujali imani zao.
Imam Hussein ni kielelezo cha utu, uadilifu, na amani. Pia ni ishara ya ukombozi wa viumbe na ni kielelezo cha kupinga dhulma ulimwenguni.
No comments:
Post a Comment