Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Magu, George Lutengano akifungua warsha ya Amsha Viwanda iliyoandaliwa na shirika la Voluntary Service Oversea (VSO) kupitia mradi wake wa TLED iliyofanyika wilayani hapo hivi karibuni.
Judith Ferdinand, Mwanza
Katika kuunga mkono juhudi za Rais Dkt.John Magufuli ya nchi kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda, wadau mbalimbali nchini wanajukumu la kubuni mbinu tofauti za kuhakikisha wanawainua wajasiriamali na hatimaye kufanya vizuri katika shughuli zao kuanzia uchakataji wa bidhaa mpaka masoko.
Kwani wajasiriamali wengi nchini wanahitaji elimu ya namna ya kutunza fedha na biashara zao, kujua teknolojia bora wanazotakiwa kutumia ili wawaweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na kwa wingi na urahisi,sehemu watakapo pata huduma za kifedha ( mikopo) kwa ajili ya kukuza na kuendeleza biashara zao pamoja na kutambua taasisi zinahusika na utoaji vibali na udhibiti ubora ili waweze kurathimisha biashara zao na bidhaa kwa ajili ya kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi.
Shirika la Voruntary Service Overseas (VSO), kupitia mradi wake wa Kuwasaidia na Kuendeleza Wajasiriamali Tanzania (TLED), wakishirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO), Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, wamekuja na mafunzo ya Amsha Viwanda, ambapo wajasiriamali 844 kutoka wilaya nne za mkoa wa Mwanza ikiwemo Magu, Kwimba, Ilemela na Nyamagana wamenufaika na mafunzo hayo ya awamu ya kwanza.
Akizungumzia namna wajasiriamali hao walivyo nufaika na malengo ya mafunzo hayo ambayo yana kauli mbiu ya Amsha Viwanda, Afisa Mradi wa TLED wa shirika la VSO Elvis Chuwa anasema katika mafunzo hayo kwa wilaya hizo nne walilenga kufikia wajasiriamali 720 hivyo wamefanikiwa kwa kuvuka lengo na kufikia 844 ongezeko la asilimia 17, hivyo inaonyesha jinsi watu walivyo na utayari ingawa walikua hawajapata mtu wa kuwaelekeza nini wafanye kufikia ndoto zao.
Chuwa anasema, katika mafunzo hayo wanaume wamejitokeza zaidi kwani jumla walikuwa 472 sawa na asilimia 56 kuliko wanawake ambao walikua 372 sawa na asilimia 44, hali hiyo inaweza kuwa imetokea kutokana changamoto mbalimbal zinazowakabili au mfumo dume katika wilaya zao.
Anasema lengo la mafunzo hayo, nikuwaonyesha wajasiriamali fursa mbalimbali zinazopatikana katika mkoa wa Mwanza ikiwemo teknolojia,mafunzo ya kibiashara, mamlaka za udhibiti za serikali ili wazitambue na kuweza kuthubu na kurathimisha biashara zao na taasisisi za kifedha kwa ajili ya kupatiwa mikopo ambayo watatumia kukuza na kuendeleza biashara sambamba na kupata kiwanda.
Aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo TLED itawasaidia kuboresha baadhi ya sehemu zao ambazo zinachangamoto ili waweze kupiga hatua katika biashara zao, ambapo awamu hii ya kwanza itakamilika kwa kumalizia wilaya tatu za mkoa wa Mwanza zilizo baki ikiwemo Ukerewe, Sengerema na Misungwi, ambapo wanatarajia kuanza mwezi januari 2018.
Pia anasema ili kuhakikisha wanafanya vizuri, awamu ya pili na tatu ya ambayo itaanza mwakani watawashika mkono moja kwa moja kwa kuwapa mafunzo kulingana na mahitaji husika kwa makundi ikiwemo wajasiriamali 120 ambao wanahitaji mafunzo kutoka TFDA na TBS ambapo watawaunganisha ili waweze kupatiwa elimu ya namna ya kuzalisha bidhaa zenye ubora na kiwango kinachostahili katika soko la ndani na nje ya nchi pamoja na kuhakikisha wanapata nembo ya ubora, 287 watapatiwa mafunzo kutoka SIDO na TLED, 426 waliunganishwa na huduma za kibenki, 55 huduma za teknolojia, TWCC 229 wanawake na TCCIA 114.
Aidha anasema, kwa kushirikiana na serikali ya mkoa ya Mwanza na Shinyanga ambapo mradi unafanya kazi na wilaya zake anaimani agizo la Rais la kila mkoa kuwa na viwanda mia litafanikiwa endapo wote wataweka nguvu kwa pamoja, kwani wajasiriamali wanachangamoto nyingi ambazo serikali pekee haiwezi kuzimaliza, ili kufikia na kuona kile tunachokitarajia.
Vilevile anasema, wajasiriamali wanatakiwa kukimbilia fursa ya kupata mafunzo kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo SIDO, TCCIA, TWCC, TFDA, TBS, wadau wa teknolojia na taasisi za kifedha, ikiwa ni lengo lao la kuona mjasiriamali anapata uelewa na taarifa sahihi ili kuboresha bidhaa zake na mwisho kuweza kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi jambo litakalosaidia kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda kwani vitafanya kazi kila siku na hatimaye kufanikisha ndoto ya Rais.
Kadhalika anasema , katika mafunzo hayo wamekumbana na changamoto ambayo watatumia muda kuiondoa ni ya wajasiriamali kutokuwa na uelewa kuhusu fursa zinazowazunguka katika biashara zao sambamba na kuwa na mtazamo hasi na fikra mbovu kwa mashirika yanayojitolea kuwasaidia pamoja na taasisi za serikali.
Msimamizi Mkuu mradi wa TLED wa shirika la VSO Frank Girabi anasema, kampeni hiyo ni sehemu ya kutekeleza mradi wao ambao unafanyika kwa miaka mitano katika mikoa 6 nchini ikiwemo Mwanza na Shinyanga.
Girabi anasema, wamejikita katika kutoa mafunzo na ushauri,kwani wanawasaidia wajasiriamali wadogo katika nyanja tofauti tofauti ambazo wanazokutana na changamoto mbalimbali ikiwemo soko,usimamizi wa fedha na biashara zao.
Pia anasema, kupitia mradi huo wanatarajia kuwafikia wajasiriamali 1760 nchi nzima, hasa wakina mama ambao wanatoka katika maeneo wanayowasaidia kwa kuwakutanisha na masoko, kuwapa mafunzo pamoja na kuwapeleka kwenye fursa mbalimbali zilizopo ndani na nje ya nchi,ili kukuza biashara zao,kuchangia pato la taifa na kutoa ajira kwa vijana na wengine.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa TLED wa shirika la VSO Mwanza Nelson Musikula anasema, mradi huo wa miaka 5 umelenga kuwawezesha watu kiuchumi na fursa za ajira, hivyo wanawaunganisha wajasiriamali na watoa huduma mbalimbali wanaohusika katika kuendeleza biashara, masoko sambamba na kuwapa mafunzo na ushauri.
Musikula anasema,kilicho wasukuma kufanya mradi huo ni kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wajasiriamali wengi nchini ikiwemo masoko, ukosefu wa elimu juu ya usimamizi wa biashara na fedha,ubora wa bidhaa.
Hivyo anasema, anaimani kupitia mafunzo hayo, wajasiriamali wataweza kutatua changamoto zilizokua zinawakabili na hatimaye kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuziuza katika masoko ya ndani na nje ya nchi, hali itakayosaidia kukuza biashara zao, uchumi na kutoa fursa za ajira.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhandisi Mtemi Msafiri anasema, mamlaka na taasisi za serikali zinatakiwa kuunga mkono juhudi za TLED kwa kuwasaidia wajasiriamali kupiga hatua ili kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa na viwanda.
Mhandisi Msafiri anasema, mafunzo hayo ya Amsha Viwanda ni muhimu katika kuwezesha wananchi kiuchumi, kuendeleza biashara na viwanda vidogo, imefanyika wakati muafaka ambapo serikali ya awamu ya tano imejipanga kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuleta maendeleo ya haraka kupitia viwanda kwa wananchi.
Pia anasema, idadi ya wajasiriamali wa uchakataji wa bidhaa mbalimbali wanakumbana na changamoto ya masoko ya ndani na nje ya nchi kutokana na bidhaa wanazozalisha kupata ushindani kwa vile zinakua na ubora hafifu hii inatokana na kutokuwa na uelewa wa matumizi sahihi ya teknolojia, ukosefu wa mtaj i, mafunzo na ushauri wa biashara sambamba na ufahamu wa namna ya kufikia huduma zinazotolewa na mamlaka ya udhibiti ubora wa bidhaa.
Meneja wa SIDO mkoa wa Mwanza Bakari Songwe anasema, wanampango wa kuanzisha viwanda kila wilaya,hivyo baada ya kampeni hiyo ya amsha viwanda wajasiriamali wataendelea kupatiwa mafunzo,ili kuhakikisha kunakuwa na viwanda vidogo vilivyosajiliwa sambamba na bidhaa zenye ubora na zilizorathimishwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Pendo Malabeja anasema, fursa hiyo ni chachu ya kufanya wajasiriamali wa Kwimba na taifa kukimbia na kwenda haraka katika kufikia uchumi na kuleta maendeleo, ikizingatiwa Rais Magufuli anataka kila Mkoa kuwa na viwanda 100,ambapo Mkuu wa Mkoa John Mongella ameagiza kuanzia desemba mpaka juni 2018,wilaya hiyo iwe na viwanda 10,hivyo wanauwezo wa kufikisha na zaidi hasa kupitia mafunzo hayo ambayo itakuwa nafasi ya kutekeleza agizo hilo.
Afisa Masoko wa TCCIA Mwanza Joshua John alisema, wanashawishi na kutetea wafanyabiashara,wenye viwanda na kilimo kwa serikali, pia wanawakutanisha wajasiriamali na wachakataji wa bidhaa na wanunuzi kwa kuwatafutia fursa za kibiashara kupitia maonyesho sambamba na kutoa mafunzo kwa wenye viwanda kulingana na mahitaji.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Magu George Lutengano anasema,ili kufikia uchumi wa kati,watu wanatakiwa kubadili fikra na kuanzisha viwanda,kwani wajasiriamali ni wengi lakini hawana uelewa,hii ni kutokana na watu kudhani ya kuwa kuanzisha kiwanda mpaka uwe na fedha nyingi.
Lutengano anasema, watatumia kampeni hiyo vizuri ili kuhakikisha wanafikia uchumi wa kati,hivyo aliwataka wanamagu walioshiriki katika warsha kupokea mafunzo hayo kwa umakini na yawe na tija kwao kwa ajili ya kuendeleza biashara zao.
Pia aliwataka wajasiriamali kutumia taasisi za mikopo kupata fedha kwa ajili ya kuendeleza biashara zao sambamba na taasisi hizo kuangalia hali za wajasiriamali ili kuwapunguzia masharti.
Naye Afisa Udhibiti Ubora wa TBS mkoa wa Mwanza Ramadhan Hassan anasema,serikali imetenga fedha kwa ajili ya wajasiria wadogo kupimiwa bidhaa pamoja na kupatiwa nembo ya ubora ya TBS bure,ambao wamepitia SIDO kwa kuandika barua ya maombi.
Hassan anasema, bidhaa yenye nembo ya ubora inamfanya mteja kuwa na uhakika na usalama wa afya yake sambamba na mzalishaji kuingia katika soko la ushindani
Hata hivyo Mwenyekiti wa TWCC Mwanza Mariam Munanka anasema, siri ya mafanikio kwa wajasiriamali ni kujituma na kufanya vitu kwa malengo kwani alianza na cherehani moja na sasa anazo 7 na ameajiri watu 10,pia bado anaendelea na miradi mingine ikiwemo ufugaji. wa ng’ombe wa maziwa na kuku.
Munaka anasema,lengo la chemba yao ni kuwawezesha Wanawake kupambana kikamilifu ili kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini na kuona fursa mbalimbali za kibiashara na kuzitumia sambamba na kuwaelekeza jinsi ya kupata taarifa za kukuza soko la ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ilemela John Wanga anasema, amsha viwanda ni fursa kwa wajasiriamali wa Ilemela,hivyo watumie mafunzo hayo kutoka hatua moja kwenda nyingine ili waweze kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi pamoja na kutoa fursa ya ajira kwa wengine.
Wanga anasena serikali imeweka mikakati ya wajasiriamali kuzalisha bidhaa na kuuza nje ya nchi, ili kuongeza pato la taifa na fedha za kigeni,hivyo kampeni hiyo iliyofanywa na TLED na SIDO ni jitihada za kuiunga mkono.
Aidha anasema, viongozi wa halmashauri hiyo, watahakikisha wanaunga mkono kampeni hiyo ili wajasiriamali wapige hatua moja kwenda nyingine,sambamba na kuomba taasisi za fedha kupunguza riba kwa wafanyabiashara hao.
Meneja wa Banki ya Posta Tanzania tawi la Pamba Mwanza Alex Minai anasema,wanatoa mikopo kwa wajasiriamali kuanzia wadogo ambao tayari wana biashara ili fedha atakazozipata zikamsaidie kukuza mtaji.
Kadhalika Afisa Biashara Mkoa wa Mwanza Anthony Yesaya anasema, mafunzo ya amsha viwanda yamewasaidia wajasiriamali kurasimisha bidhaa zao na kuwakutanisha na taasisi za kifedha na taasisi ya VIGUTA inayotoa mkopo kwa kuwasaidia ujenzi wa viwanda wajasiriamali wadogo ili waweze kukidhi vigezo vya TFDA.
Yesaya anasema, wajasiriamali wengi hawana uelewa juu ya taasisi zipi zinazohusika kwa ajili ya utoaji vibali na kurathimisha ili bidhaa na biashara , kama GS1, TBS,TFDA na Blela,wanadhani wakisha pata mafunzo SIDO au wakipewa kibali na mamlaka moja wamemaliza.
Anasema, wajasiriamali wengi wanaamini mafunzo ni kuletewa fedha wakati lengo la TLED na serikali ni kuweka mazingira ambayo yatasaidia kupata huduma muhimu katika biashara zao.
Vilevile Mratibu wa Muunganiko wa Vikoba Tanzania (VIGUTA) Kanda ya Ziwa Gerimina Kabola anasema, wanashughulika na wajasiriamali wadogo ili waweze kujitegemea na kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda kwa kuwasaidia kuwajengea viwanda vinavyokidhi vigezo vya TFDA kwa bei nafuu na kulipa kidogo kidogo kwa miaka 5.
Hata hivyo baadhi ya wajasiriamali ambao walipata fursa ya kushiriki mafunzo hayo walikua na yakusema.
Mwakilishi wa Vijana Saccos wilaya ya Ilemela Charles David anasema,warsha ya amsha viwanda imempatia elimu ya kuwa ili kupata soko la ndani na nje lazima usajili bidhaa,hivyo atatumia kama fursa katika Kuendeleza biashara zake na hatimaye haweze kufikia ndoto yake ya kuwa mfanyabiashara mkubwa.
Vilevile Mercy John anasema, ametambua umuhimu wa nembo na kusajili bidhaa zao,ili waweze kuuza nje ya nchi, pia ataenda kuhamasisha wanawake wenzie kuhusu umuhimu wa kuhudhuria mafunzo mbalimbali sambamba na kuwaelimisha.
Gertruda Mdungile kutoka wilaya ya Kwimba anasema, ni fursa ya kujiimarisha katika ujasiriamali na kujengewa uwezo wa kitaalamu na kisayansi katika kutumia teknolojia.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mhandisi Mtemi Msafiri akizungumza katika ufunguzi wa kampeni ya Amsha Viwanda wilayani humo iliyoandaliwa na Shirika la VSO kupitia Mradi wake wa TLED.
Baadhi ya wajasiriamali walioshiriki katika warsha ya kampeni ya Amsha Viwanda iliyoandaliwa na VSO kupitia mradi wake wa TLED iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment