Friday, 15 December 2017

HOTUBA YA RC IRINGA UZINDUZI KAMPENI YA UJEZI WA VIWANDA






Mkuu wa mkoa wa iringa amina masenza akimkabidhi mpango kazi mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoani iringa frank leonard (kushoto) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ujenzi wa viwanda mkoa wa iringa leo katika ukumbi wa siasa ni kilimo mjini iringa. (Picha na Friday simbaya)


HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA IRINGA MHE. AMINA JUMA MASENZA WAKATI WA KUZINDUA KAMPENI YA “MKOA WETU VIWANDA VYETU” NGAZI YA MKOA KATIKA UKUMBI WA SIASA NI KILIMO TAREHE 15 DES. 2017

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa,
Wakuu wa Wilaya,
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa,
Waheshimiwa Wabunge Milio hudhuria,
Mheshimiwa Msitahiki Meya wa Halmauri ya Iringa,
Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri,
Waheshimiwa Madiwani
Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya,
Viongozi wa Madhehebu ya Dini,
Wakuu wa Taasisi na Mashirika mbalimbali,
Wanazuoni wa Vyuo Vikuu,
Wadau wa Maendeleo mliohudhuria,
Waandishi wa Habari,
Wageni waalikwa, Mabibi na mabwana

Ndugu wana Iringa,
Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma kwa kutupa Afya njema na kutuwezesha kukusanyika hapa leo. Leo ni siku maalum katika Mkoa wetu wa Iringa kwa ajili ya uzinduzi wa Kampeni ya kuhamasisha ujenzi wa viwanda, Kampeni iliyopewa Kaulimbiu ya “Mkoa wetu, Viwanda vyetu”. Asante sana kwa kuitika wito.
Ndugu wana Iringa,
Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa Mikoa nchini ambayo bado inakubwa na changamoto ya maskini wa kipato. Serikali yetu ya Awamu ya Tano chini ya Jemedari wetu Mheshimiwa Rais John Pombe Maufuli imeazimia kuondokana na aibu hii.  Serikali imebuni Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 inayokusudia kutufanya tuwe taifa ambalo watu wake walio wengi watakuwa na maisha bora; Taifa lenye amani, utulivu, na umoja;
Taifa linaloongozwa kwa misingi ya utawala bora, utawala wa sheria; Taifa lenye watu walioelimika na wanaoendelea kujielimisha; na Taifa lenye uchumi unaohimili ushindani, UCHUMI WA VIWANDA unaokua na kutoa ajira na mapato, uchumi endelevu usioharibu mazingira yetu.
 Ndugu wana Iringa,
Katika kutekeleza azma hii ya Serikali ya Uchumi wa Viwanda, tumepewa mwaka mmoja kuhakikisha Mkoa wetu unaanzisha viwanda si chini ya viwanda 100.  Hayo ni malengo, lakini utekelezaji wake unategemea sana jasho na maarifa ya kila mwana Iringa na wadau wanaopenda Mkoa wetu wa Iringa.
Ni vyema kila mfanyakazi, kila mkulima, kila mfugaji, kila mvuvi, na kila mfanyabiashara, wa kike na wa kiume ni lazima tujizatiti kutumia fursa hii ya kujikomboa kiuchumi kwa kuanzisha viwanda hivi. 
  Ndugu wana Iringa,
Manufaa ya kuanzisha viwanda ni makubwa mno, tutakapo anzisha viwanda tutaweza kupata faida zifuayo:
    i.        Mazao ya Kilimo yanayolimwa katika Mkoa wetu yatapa nafasi ya kusindikwa na kuongezewa thamani na hivyo kuongeza kipato cha mkulima na mapato yake kuboresha Maisha ya mkulima,
  ii.        Wananchi wetu watapata ajira na hasa vijana kwa kuajiriwa katika viwanda vitakavyo anzishwa,
iii.        Serikali Kuu na Halmashauri zetu zitapata mapato yatokanayo na kodi na ushuru wa bidhaa zinazozalishwa viwandani,
iv.        Serikali pia inapata fedha za kigeni kutokana na mauzo ya bidhaa za viwandani zinazouzwa nje ya nchi,
  v.        Uhakika wa soko kwa bidhaa na mazao yanayolimwa katika Mkoa wetu unapatikana,
vi.        Mkoa unapata faida pia kwa kupata wawekezaji wakubwa kutoka nje ya nchi abao watasaidia pia kuleta technolojia mpya na za kisasa katika Uzalishaji viwandani,
vii.        Viwanda pia vinaimarisha Sekta nyingine kama vile usafirishaji, mawasiliano, elimu, afya, huduma za fedha, hali ya usalama inaimarika katika Jamii.
Hizi ni baadhi tu ya faida chache za ujenzi wa viwanda. Lakini jambo kubwa na muhimu ni kuboreka kwa huduma za kijamii ambazo zinasaidia kundi kubwa la watoto na wanawake.
 Ndugu wana Iringa,
Naomba nitumia fursa hii kuwapongeza wawekezaji wananchi na wale wote kutoka nje ya nchi walioamua kuwekeza katika Mkoa wetu. Takwimu tulizonazo, mpaka sasa Mkoa wa Iringa una Jumla ya Viwanda vikubwa 24, viwanda vya kati 35, viwanda vidogo 149 na viwanda vidogo zaidi zaidi ya 3,000. Viwanda vyote hivi vinatoa ajira ya moja kwa moja ya watu 15,000 ambayo ni sawa na asilimia 1.6 ya wakazi wa Mkoa mzima wa Iringa. Lengo letu ni kuongeza kiwango hiki cha viwanda ili viweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika Uchumi wa Mkoa.
Ndugu wana Iringa,
Tunafikaje katika ujenzi wa Viwanda 100. Hii itatokana tu na kila mmoja wetu awe tayari kwa nafasi yake kutekeleza wajibu wake. Halmashauri zetu zitatuongoza chini ya uratibu wa waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, kwa kuwa kila Hlamashauri imepewa jukumu la kujenga viwanda vipya 35. Viwanda 20 hadi kufikia mwezi Juni, 2018 na viwanda 15 ifikapo mwezi Desemba, 2018.
Aidha, tayari Taasisi nyingine nimekwisha zipa malengo ikiwemo SIDO Mkoa kujenga viwanda visivyopungua 20 na taasisi nyingine zimeonesha nia ya kuunga mkono juhudi hii zikiwemo taasisi za madhehebu ya dini, Vyama vya Ushirika na wadau wengine wa maendeleo.
Wito wangu kwa Halmashauri ziweke mazingira bora ya ujenzi wa viwanda na visikwamishe juhudi za wale wenye nia nzuri ya kuwekeza katika viwanda, hii ni pamoja na Mamlaka nyingine za Udhibiti kama vile TANESCO, TRA, IRUWASA, TBS, TFDA  na nyinginezo zote zisaidie kuweka mazingira wezeshi katika kutekeleza Kampeni hii.
Wananchi pia waendelea na waboreshe zaidi Uzalishaji wa mazao ya Kilimo kwa kuwa hakuna viwanda bila malighafi na malighafi nyingi za viwanda ni mazao ya Kilimo.
 Ndugu wana Iringa,
Pamoja na juhudi kubwa hii inayofanywa na Serikali, itakuwa kazi bure kama Uzalishaji wa bidhaa hizi utalenga soko la nje badala ya sisi wana Iringa kuwa ndiyo soko la bidhaa hizi kwanza. Natoa wito kwetu sisi sote tupende na tutumie bidhaa zinazozalishwa katika Mkoa wetu kwanza.
Kwa kuhitimisha, napenda kuchukua fura hii tena kuwashukuru wote mliohudhuria hapa na tuwe tayari sote katika utekelezaji wa dhati wa Kampeni hii. Kila kiongozi atapimwa kwa utekelezaji wake hatua kwa hatua. Baada ya kusema haya, sasa niko tayari Kuzindua Kampeni hii ya “MKOA WETU VIWANDA VYETU” NGAZI YA MKOA” na ninawaagiza baada ya hapa kila wilaya ifanye uzinduzi wake katika ngazi ya Wilaya kwa maana ya Halmashauri.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...