Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ni kama imeanza kuingia mchecheto baada ya kuitaka Bodi ya Ligi (TPLB) kusogeza mbele mechi yake dhidi ya Azam iliyopangwa kuchezwe Februari 11 mwaka huu.
Simba yenye pointi 35, inachuana vikali na Azam wenye 30 katika msimamo wa ligi na Mabingwa watetezi Yanga waliovuna 28, katika kuliwania taji hilo la ubingwa la ligi.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Haji Manara alisema ratiba yao inawapa ugumu kutokana na akili na nguvu zao kuzielekeza kwenye michuano ya kimataifa na Simba imepangwa kucheza Gendarmerie Nationale ya Djibouti kati ya Februari 9-11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Manara alisema, ratiba hiyo inawapa ugumu kwani Simba itacheza na Ruvu Shooting Februari 4 na kucheza na Azam kabla ya kwenda Shinyanga kucheza na Mwadui huku wakiusubiria mchezo wao wa kimataifa.
“Mipango ya Simba ni kufika mbali katika michuano ya Afrika na hiyo ndiyo sababu ya sisi kumchukua kocha Mfaransa, Lechantre (Pierre) ambaye amewahi kuipa ubingwa wa Afcon, Cameroon mwaka 2000.
“Hivyo, basi kama uongozi tumeiomba Bodi ya Ligi kusogeza mbele mchezo wetu dhidi ya Azam ili kutupa nafasi ya kujiandaa na mechi yetu ya kimataifa dhidi ya Wadjibout kwa kuwa tunaona ratiba inabana sana.
“Tupo katika hatua ya mwisho kwa ajili ya kuiandikia bodi ya ligi ili kuwafahamisha mchezo huo usogezwe mbele na kikubwa tunataka kuona Simba ikifanya vema katia michuano hii ya mikubwa Afrika, tunaamini busura itatumika,”alisema Manara.
No comments:
Post a Comment