Sunday, 21 January 2018

KAMATI YA PETS YAIOMBA IRINGA DC IONGEZE USIMAMIZI KATIKA PEMBEJEO ZA KILIMO

DSC02973


Kamati ya Mfumo wa Ufuatiliaji wa Matumizi ya raslimali za Umma (PETS) Wilaya ya Iringa imetoa mapendekezo na maoni kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, mkoani Iringa kuhusu usimamizi endelevu wa pembejeo za kilimo ili kuongeza uwajibikaji, uwazi wa Jamii na viongozi.

Kamati ya PETS Wilaya ya Iringa katika ziara yao waliyofanya katika kata za Kiwere, Maguliwa, Mgama, Ifunda na Wasa hivi karibuni walibaini changamoto mbalimbali na kutoa mapendekezo na maoni katika kuwainua wakulima wadogo wadogo kwa usimamizi endelevu wa pembejeo za kilimo ili kuongeza uwajibikaji, uwazi wa Jamii na viongozi katika Wilaya ya Iringa na Tanzania kwa ujumla.

Katibu wa Kamati ya PETS wilaya ya Iringa kwenye kilimo, Hamida Tanda alisema jana kuwa Kamati ilibaini baadhi ya viongozi wa serikali, bado wana uelewa mdogo kwenye dhana ya ufuatiliaji wa raslimali za umma. 

Alisema kitendo cha wananchi kuhoji mapato na Matumizi kutoka kwa watoahuduma kinaonekana kuwa si jambo jema hususani kwa baadhi ya maofisa na viongozi wa serikali. 

Akisoma mapendokezo katibu wa kamati ya PETS kwenye kilimo wilaya ya Iringa huyo katika mdahalo wa wadau mbalimbali ulioandaliwa na taasisi ya Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Kanda ya Kitapilimwa (MJUMIKK) alisema kuwa mawakala na viongozi wa serikali wasio waaminifu wawajibishwe kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi. 

Pale ambapo viongozi wanapojihusisha na vitendo vya kuhujumu mali za umma au kukiuka maadili ya uongozi na mamlaka wakati wa usambazaji wa pembejeo za kilimo.

Tanda alisema kuwa serikali ni lazima ihakikishe suala la pembejeo za kilimo linaingizwa kwenye mipango kazi ya vijiji, kwa kuwa kilimo ndiyo chanzo kikubwa cha mapato katika vijiji vingi. 

Hivyo, wananchi wanatakiwa kuhamasishwa kuweka masuala ya kilimo kwenye mipango kazi yao. 

Aidha, katibu huyo wa katmati ya PETS alisema kuwa bajeti katika idara ya kilimo, Halmashauri ya Wilaya na serikali kuu iongezeke na kuongeza kuwa Halmashauri za vijiji, Wilaya na Serikali kuu zihamasishwe kuongeza fedha zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo. 

Kamati ya PETS ni Kikundi cha watu maalum waliochaguliwa kupitia mikutano ya vijiji ili kuwa wa wakilishi wa wananchi wao katika ufuatiliaji wa raslimali za umma katika ngazi ya kijiji, Kata, na hata Wilaya ikiwa na lengo la kuhakikisha raslimali mbali mbali zilizotengwa na ngazi yoyote ya serikali kwa manufaa ya umma inakwenda kutumika kama ilivyokusudiwa na serikali husika.

Mradi wa PETS katika Kilimo unaotekelezwa na taasisi ya Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Kanda ya Kitapilimwa (MJUMIKK) katika kata tano (5) ambazo ni Kiwere, Magulilwa, Mgama, Ifunda, na Wasa. 

Mradi huu umefadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali linaloitwa The Foundation for Civil Society (FCS). Kupitia Mradi huu taasisi ya MJUMIKK ilifanikiwa kuunda kamati tano (5) za PETS ngazi ya Kata, na kamati moja (1) ya PETS ngazi ya wilaya. 

Aidha kamati zote za PETS ngazi ya kata na Wilaya zilipata mafunzo maalum ya ufuatiliaji wa raslimali za umma kwenye mradi wowote ule mfano elimu, Afya, Miundombinu na Kilimo.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...