HALMASHAURI ya Wilaya ya Mufindi itatumia jumla ya shilingi Milioni Mia nne (400) kujenga na kufanya ukarabati mkubwa wa kituo cha Afya Malangali, kilichopo kata ya Malangali Halmashauri ya Wilayani Mufindi, ikiwa ni mkakati wa Serikali kuimarisha sekta muhimu ya Afya hususani Afya ya Mama na Mtoto.
Profesa Riziki Shemdoe, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi alisema ujenzi na ukarabati wa kituo hiki cha Afya, unaotarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa, unafanyika baada ya Ofisi ya Rais – Tamisemi, kutoa kiasi cha Shilingi Milioni mianne (400) kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya kituo hicho ili kiweze kukidhi haja ya kutoa huduma bora za Afya kwa zaidi ya Wananchi elfu arobaini na nane (48,000) wa Tarafa ya Malangali watakao pewa rufaa kutoka kwenye Zahanati za Vijiji.
Alisema matumizi ya kiasi hicho cha fedha, ni pamoja na kujenga jengo la kisasa la Maabara, Nyumba ya Mganga, kukamilisha ujenzi unaoendelea wa chumba cha upasuaji sanjari na kufanya ukarabati mkubwa wa Wodi maalum ya wazazi / Mama na Mtoto.
Profesa Shemdoe, alisema ujenzi na ukarabati wa kituo, utatekelezwa kwa mfumo wa (Force Account) ambapo, Halmashauri itatumia Mafundi wenyeji watakaothibitishwa kuwa na uwezo unaokubalika wa kutekeleza jukumu hili kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu, badala ya mtindo uliozoeleka wa kutumia Wakandarasi.
Pia, ili kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika, Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji, imeunda Vikosi kazi vitatu (03) vikijumuisha Maofisa kutoka idara mbalimbali maalum kwa kuratibu na kusimamia mradi huu kwa kuzingatia wakati na ubora.
Kwa upande wake, Ofisa Habari na Mawasiliano Halmashauri ya (W) Mufindi, Ndimmyake Mwakapiso, alisema kwa kuwa uboreshaji wa kituo hicho, utatekelezwa kwa mfumo wa (Force Account), Mkurugenzi Mtendaji anawahamasisha wananchi wote wa Tarafa ya Malangali kujitolea nguvu kazi pindi itakapohitajika wakati wa utekelezaji wa mradi huu kwa ustawi wa Afya ya kila mkazi wa Tarafa ya Malangali na Halmashauri ya Mufindi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment