Ofisa Biashara wa Sido Niko Mahinya |
Ofisa Mikopo wa SIDO Mkoa wa Iringa Neserian Laizer
|
KILOLO: SHIRIKA la kuhudumia viwanda vidogovidogo (SIDO) Mkoa wa Iringa katika kuunga juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kupambana na wimbi la umasikini limekikopesha kikundi cha Upendo IR Vicoba cha Kijiji cha Mtandika kiasi cha shilingi milioni kumi na tatu na laki tatu (13.3m/-) kwa ajili ya kuweza kuwasaidia kuendesha shughuli za kilimo.
Akizungumza na viongozi na wajumbe wa kikundi hicho cha wakulima kilichopo wilayani Kilolo, katika hafla fupi ya kukabidhi cheki ya fedha iliyofanyika katika Kijiji cha Mtandika, Kata ya Ruaha-Mbuyuni, Ofisa Mikopo wa SIDO Mkoa wa Iringa Neserian Laizer alisema kuwa wamekikopesha kikundi cha wakulima ili kuwainua kiuchumi na kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo.
Ofisa mikopo huyo alisema kwamba wamebaini katika maeneo mengi ya vijiji kuna fursa nyingi zilizopo katika zao la kitunguu lakini baadhi ya wakulima wanashindwa kutimiza malengo yao waliyojiwekea kutokana na kukosa mtaji wa fedha.
“ …hivyo wakiwezeshwa wataweza kutumia fursa zilizopo za kilimo kwenye maeneo yao ili kuleta mabadiliko chanya ya kukuza uchumi,” alisema Laizer.
Naye Ofisa Biashara wa Sido Niko Mahinya aliongeza kuwa Shirika hilo lengo lake kubwa ni kuwasaidia fedha za mitaji wakulima ili waweze kujiendeleza zaidi sambamba na kuwajengea uwezo wa wakuzalisha kitunguu katika ubora unaotakiwa pamoja kuwatafutia masoko.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi cha wakulima cha Upendo IR Vicoba kilichopo katika kijiji cha Mtandika Salama Maulidi Chowanga alilipongeza shirika la Sido kwa kuwapatia mkopo huo licha ya kukabiliwa na changamoto ya soko la zao la kitunguu.
Mwenyekiti huyo alisema kwamba wanakundi ambao wamepatiwa mikopo wanaitumia kwa malengo yaliyokusudiwa pamoja na kuhakikisha wanachama wanarejesha mkopo kwa wakati.
Naye katibu wa kikundi Zamoyoni Zigo alisema kuwa kikundi cha kinajumla ya wanachama 30 lakini waliopatiwa mikopo ni wanachama 29, mmoja walikosa mkopo kutokana na matatizo ya kifamilia.
Mwsho
No comments:
Post a Comment