MAHAKAMA ya hakimu mkazi mkoa wa Iringa imewapandisha kizimbani watuhumiwa 83 raia wa nchini Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Wakisomewa mashataka yao mbele ya hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Iringa David Ngunyale wakili wa serikali Godfrey Ngwijo alisema kuwa Februari 23 katika tarafa ya Mazombe wilaya ya Kilolo mkoani hapa watuhumiwa hao walikamatwa na maofisa uhamiaji kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Ngwijo alisema kuwa kosa la pili linamkabidhi utingo wa gari hilo Hassan Ferooz (18) mkazi wa Tukuyu mkoani mbeya kwa kosa la kusafirisha watuhumiwa hao kuwapeleka nchini Afrika kusini lakini mtuhumiwa huyo alikana shitaka hilo.
Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza ambapo mara baada ya kusomewa mashtaka hayo hakimu Ngunyale alisema kwa kosa la kuingia nchini bila kibali ni kwamba kesi hiyo itatajwa tena Machi mbili mwaka huu hadi watakapopata mtafsiri ambaye atatafsiri raia hao huku kosa la pili likiwa ni kwamba mtuhumiwa kosa lake linadhaminika.
Awali kabla ya kuanza kwa kesi hiyo raia hao walionekana wakiangua vilio mahakamani hapo hali ambayo ilimlazimu hakimu kumtaka mwanasheria wa serikali kumtafuta kiongozi wao kwa lengo la kuwatuliza jambo ambalo lilifanikiwa.
Ngwijo alisema Februari 23 mwaka huu raia hao wasio na vibali walikamatwa wakiwa na gari aina ya lori lenye namba za usajili T.903 AKH ,Mali ya Gabriel G.Mwakyambiki wa tukuyu mkoani Mbeya.
Hata hivyo Februari 21 mwaka huu raia wengine wanne wa nchini Ethiopia walikamatwa na idara ya uhamiaji wakiingia nchini bila kibali ambapo ofisa uhamiaji wa Iringa Hope Kawawa alisema kuwa Iringa sio uchochoro wa kupitisha raia wasio na kibali.
No comments:
Post a Comment