IRINGA: JESHI la polisi mkoani Iringa linawashikilia watu wawili kuhusiana na tukio la kifo cha kiutatanishi cha mwanafunzi wa shule ya sekondari Mwembetogwa kilichotokea juzi maeneo ya mtaa Kisiwani kata ya Mwangata manispaa ya Iringa.
Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa ACP, Juma Bwire akizungumzia tukio hilo juu ya tukio la kifo cha mashaka kilichotekea majira ya saa 12 asubuhi ambapo mwanafunzi wa kidato cha sita Sudi George (22) mkazi wa Kisiwani alikutwa amefariki dunia kwenye miti ya kugema pombe ya ulanzi huku mwili wake ukiwa na kamba maeneo ya shingoni.
Kamanda Bwire alisema majina ya watu hao hawezi kuwataja lakini inaonyesha kuwa taarifa za awali zinaonyesha kuwa Machi 12 marehemu akiwa na sare za shule alitoka kwao kuelekea shuleni lakini hakurudi hadi mwili wake ulipopatikana katikamaeneo hayo.
Alisema kuwa baada ya taarifa za tukio hilo kufika jeshi la polisi walifanya msako mkali kuhusiana na tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata watu wawili ambao wako nje ya familia kutokana na mazingira ambayo yalijitokeza na taarifa walizopata.
Alisema kuwa jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi mkali kubaini chanzo cha tukio kilichopelekea mwanafunzi huyo kukutwa katika hali hiyo pamoja na kupata taarifa za kitibabu hivyo taarifa kamili itafuata baada ya kukamilisha upelelezi.
Kamanda Bwire alitoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuweza kubaini nani anahusika zaidi na tukio hilo na kuwataka wananchi kuachana na matendo ambayo yanahusiana na imani za kishirikina.
No comments:
Post a Comment